Na Kijakazi
Abdalla
Wakala wa Chakula
na Dawa Zanzibar (ZFDA) imekifunga kiwanda cha kutengeneza dawa za kukosha
mikono (SANITIZER) baada ya kubainika dawa hizo hazina kiwango kinachohitajika
pamoja na kutokuwa na usajili rasmi.
Hatua ya
kukifungia kiwanda hicho kinachojulikana kwa jina la OIL CAM kilichopo Kiembesamaki
imekuja baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa Mamlaka hiyo.
Akitoa taarifa
kwa waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi ZFDA Salim Hamad Kassim
amesema kwa hatua ya awali wameamua kukifunga kiwanda hicho na kumpa nafasi
mmiliki kufuata taratibu za usjili na kuwasilisha sampuli ya bidhaa
wanayozalisha ili ifanyiwe uchunguzi katika maabara yao.
Amesema kawaida
bidhaa za viwandani kabla ya kufika kwa watumiaji zinatakiwa zifanyiwe
uchunguzi na zifikie kiwango cha ubora unaokubalika kulingana na muongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuanzia asilimia
75 hatua ambayo bidhaa hiyo haikufikia.
Aliongeza kuwa
walichogundua katika kiwanda hicho ni kuweka nembo bandia inayoonesha bidhaa
hiyo inazalishwa nchini Marekani jambo ambalo sio kweli.
Hata hivyo
amesema kukifunga kiwanda hicho ni kwa mujibu wa sheria ambazo zimewekwa na Serikali kuu pamoja na
Mamlaka husika.
Mkuu wa
Kitengo cha Vipodozi alieleza kuwa kwa mujibu wa uchunguzi waliofanya katika
maduka mbali mbali chupa yenye ujazo wa nusu lita inauzwa shilingi 25,000 kwa
rejareja na jumla inauzwa shilingi 18,000.
Muangalizi wa
Ubora na Usalama na Ufanisi wa Dawa Sokoni Nasir Salum Buheti amesema kuwa watawaagiza
wenye maduka kusitisha kuuza bidhaa za
kiwanda hicho na wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwa waangalifu
wanaponunua bidhaa dukani.
Aidha amesema Wakala wa Chakula na Dawa
Zanzibar itaanzisha msako zaidi katika kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya
corona ili kuhakikisha bidhaa zinazouzwa zinakuwa na kiwango na zimethibitishwa
na Mamlaka hiyo.
Amesema ZFDA
haina nia ya kumuonea mtu bali imewataka wajasiriamali wanaotengeneza sabuni za
kukoshea mikono kwa ajili ya kujikinga na Corona na bidhaa nyengine wahahakishe
kuwa wanafuata taratibu ili kulinda afya za watumiaji.
Mmiliki wa
kiwanda hicho aliejulikana kwa jina moja tu la Mustafa hakuwepo katika maeneo
ya kiwanda wakati wa ukaguzi na baadhi ya wafanyakazi wake walisema kuwa
amesafiri kwenda Dar es salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Vipodozi wa ZFDA Salim Hamad Kassim akiwaonyesha waandishi wa habari Dawa ya Kuoshea Mikono
(SANITAIZER) ambayo haina Kiwango iliyotengenezwa na Kiwanda cha Oil Cam kilichopo Kiembesamaki, Wilaya ya Magharibi 'B' Unguja.
Muangalizi wa Ubora na Usalama na Ufanisi wa Dawa Sokoni, Nasir Salum
Buheti akipima Dawa ya Kuoshea Mikono (SANITAIZER) katika Kiwanda cha Oil Cam huko Kiembesamaki .
Mkuu wa Kitengo cha
Vipodozi ZFDA Salim Hamad Kassim akikaguwa vifaa vinavyotumika katika
kutengeneza Dawa ya SANITAIZER ndani ya Ofisi ya Kiwanda cha Oil Cam
Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi 'B' Unguja.
Mfanya kazi wa Kiwanda cha Oil Cam
kinachotengeneza Dawa za Kuoshea Mikono, Tevin Kiponda akieleza utaratibu wanaotumia kutengeneza
Dawa ya Sanitaizer ambayo imeonekana haina Kiwango katika eneo la Kiembe samaki.
Baadhi ya Vifaa vinavyotumika
kutengeneza na kutiwa Dawa ya Kuoshea Mikono (SANITAIZER) zinazotengenezwa na Kiwanda cha Oil Cam Kiembe samaki.Picha Na
Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...