Na Amiri kilagalila, Njombe
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amewaagiza maafisa tarafa kuwafungia biashara wafanyabiashara watakaobainika wamepandisha bei vitakasa mikono zikiwemo ndoo za maji katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19.
Ametoa agizo hilo hii leo katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Njombe kilichofanyika nje ya ofisi ya wilaya ya Njombe wakati wakipokea taarifa rasmi za kamati za utekelezaji wa mapambano dhidi ya maambukizi ya Corona (COVID -19) wilayani humo.
“Kwa hiyo maafisa tarafa watu wa namna hiyo huko vijijini kwenu awe ni mjini tafadhari ita afisa biashara weka kufuli halafu hatua nyingine zitachukuliwa hapo baadaye”
Aidha amesema kwa mujibu wa maelekezo ya serikali kwa wafanyabiashara wa namna hiyo kwa kipindi ni kumfungia biashara.
“Wako baadhi ya wafanyabiashara ambao kwasababu zao wenyewe wamepandisha bei za vifaa hivi hasa ndoo kwa ajili ya kusafisha mikono,sasa maelekezo tuliyopewa kama kuna mfanyabiashara yeyote anaamua kupandisha bei za vifaa hivi ambavyo vinahitajika sana kwa kipindi hiki ni kumfungia biashara yake ndicho tulichoelekezwa,kwa hiyo maafisa tarafa ukiona kweli mtu amepandisha bei ya ndoo,koki,amepandisha bei ya sabauni za mikono nipe taarifa kinachofuata tunamfungia biashara,hayo tukiyatekeleza vizuri hakuna yeyote atakayekwenda kinyume”alisema tena Ruth Msafiri
Ruth Msafiri ametoa agizo kabla ya kuhitimisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mara baada ya kupokea taarifa ya afisa tarafa wa tarafa ya Njombe mjini Lilian Nyemele kukutana na changamoto hiyo kwa wafanyabiashara.
“Imejitokeza changamoto kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza ndoo hizi za maji kwa ghalama,awali ndoo ya lita kumi iliuzwa kwa shilingi elfu 7 na sasa kufikia shilingi elfu kumi,na ndoo kubwa iliuzwa elfu 12 na sasa imefika elfu 18 lakini tumefanya jitihada na kutoa maelekezo kwamba kupitia ugonjwa huu sio fursa ya kujinufaisha”alisema Lilian Nyemele.
Vile vile katika muendelezo wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha COVID- 19,mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri na wataalamu wa afya mbele ya kamati ya ulinzi na usalama amezindua kipeperushi maalumu chenye maelekezo muhimu juu ya ugonjwa huo pamoja na mashine ya kutakasa mikono pasina kugusa na mikono.
Isdory Kiyenze ni meneja wa shirika la viwanda vidogo vidogo sido mkoa wa Njombe ambaye amesema wao wamelazimika kutengeneza mashine maalumu ya kunawia mikono bila kugusa sehemu yoyote zaidi ya kukanyaga pedali unapohitaji kutoa maji au sabuni wakati wa kunawa mikono, ambayo itakuwa rahisi kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi ambayo itasambazwa kwenye taasisi mbalimbali za umma huku wakipanga kutengeneza na ndogo ambazo zinaweza kutumika hata kwenye ngazi ya familia.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akitoa maelekezo ya kuwafungia biashara mfanyabiashara yoyote atakayepandisha bei vitakasa mikono kwa kipindi hiki cha mapambano ya Corona.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akionyesha kipeperushi cha halmashauri hiyo alichokizindua ili kiweze kugawiwa kwa watu mbali mbali kwa lengo la kuelimisha namna ulivyo ugonjwa wa COVID-19.
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri akifurahia mara baada ya kuzindua mashine ya kunawa mikono bila kugusa kitu chochote iliyotengenezwa na SIDO
Isdory Kiyenze,meneja wa shirika la viwanda vidogo vidogo sido akinawa mikono mara baada ya kuzinduliwa kwa mashine hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...