KATIKA kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya uharakishaji katika ujenzi wa miundombinu ya umeme nchini, Kampuni ya uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya umeme ya Kilimanjaro Cables ‘AFRICAB’ inatarajia kufunga mitambo mipya 10 itakayowezesha uzalishaji wa nyaya za umeme mara mbili kutoka uzalishaji wa sasa.


Hatua hiyo pamoja na mambo mengine inatajwa na Kampuni hiyo kuwa itasaidia usambazaji wa umeme huo inayofanywa kupitia Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) kwenda kwa kasi kama ilivyoagizwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati iliyotembelea kiwandani hapo hivi karibuni kujionea uzalishaji unaofanyika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho Mansoor Moiz, kufungwa kwa mitambo hiyo mipya na ya kisasa, kutakiwezesha kiwanda hicho kufikia uzalishaji nyaya kutoka wastani wa Kms 37,500 za sasa hadi kms 75000 ifikapo Julai Mwaka huu na hivyo kuongeza ufanisi katika miradi hiyo na mengineyo inayotumia bidhaa za kampuni hiyo.

“Tunafanya hivyo ili kuunga mkono juhudi za Serikali yetu ambayo kwa sasa tunashuhudia inafanya kazi kubwa ya kusambaza umeme maeneo mbalimbali ya nchi,tunafanya kazi ya uzalishaji usiku na mchana lengo ni kuhakikisha tunawasaidia wakandarasi wote waliopo katika miradi hiyo kufanya kazi zao kwa uhakika kulingana na muda” alisema Moiz.

Alisema kiwanda hicho kilichoanzishwa Mwaka 2001 kama mtengenezaji wa nyaya za majumbani , kwa sasa kinazalisha wastani wa Mita 6900 za nyaya za kuchoronga(Drawing), nyaya za kuvishwa(Insulting) KMS 18,000 na kusukwa(Stranding) KMS 37,500 pekee na kuongeza kuwa kufungwa kwa mitambo hiyo mipya kutakiwezesha kiwanda hicho kuzalisha mara mbili ya idadi hiyo ya sasa.

Akizungumza wakati wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati ilipotembelea kiwanda hicho hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dustan Kitandula, aliutaka uongozi wa kiwanda hicho cha AFRICAB kuongeza uzalishaji ili kuwawezesha wakandarasi wa miradi ya umeme inayotekelezwa na Serikali kuendana na kasi.

Mbali ya kupongeza juhudi ya kiwanda hicho kwa uzalishaji inaoufanya, alisema kuna haja ya AFRICAB kuona namna ambavyo itazidi kuongeza kasi ya uzalishaji ili kuzidi kuharakisha kasi ya miradi hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Tutaendelea kufanya kazi katika mwelekeo wa kuanzisha vitengo vya viwanda ili kukidhi mahitaji ya soko la umeme Tanzania kwa kuwa tumechagua kuwa kituo kimoja cha suluhisho la utoaji wa mahitaji yote ya umeme nchini na Afrika Mashariki” alisema Moiz

Mbali na uzalishaji wa nyaya, kiwanda cha AFRICAB pia kinazalisha vifaa mbalimbali vya umeme wa majumbani, Isolators pamoja na Transfoma ambazo kwa wastani kiwanda hicho kinazalisha Transfoma 6500 kwa Mwaka.

Aidha Moiz aliwataka wazalishaji wengine kuendelea kushirikiana kwa pamoja kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kulinda soko la ndani na hivyo kulitangaza taifa nje ya mipaka yake kwa kuwa na bidhaa zenye kumlinda mlaji.

Alisema mahitaji la ya bidhaa mbalimbali za umeme katika soko bado ni kubwa hivyo kuna kila sababu ya wazaalishaji wote kufanya kazi kwa umoja ili kuongea tija badala ya kushindana ambapo madhara yake makuu ni kuzalisha bidhaa zisizo na ubora kwa kigezo cha kukimbilia soko.


Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu akiwa na Mwenyekiti wa Kamati wa Kudumu ya Bunge y Nishati Dustan Kitandula kushoto kwake, wakipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda cha AFRICAB David Tarimo kuhusu uzalishaji wa nyaya unaofanywa kiwandani hapo,wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa AFRICAB Mansoor Moiz.

Mkurugenzi Mkuu wa AFRICAB Mansoor Moiz akiwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati Subira Mgalu



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati Dustan Kitandula akipewa maelezo kuhusu uzalishaji kiwandani hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...