By MZEE WA ATIKALI  ✍️✍️✍️


1. Usuli:

Katika miaka ya karibuni, kwenye "social media" kumetamalaki picha na habari za utani dhidi ya Wanyakyusa@ "WANYAKI" zikionesha kwamba Wanyakyusa ni watu ambao hawajaenda shule na ni washamba kupindukia!.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro na Bukoba ndiyo iliyokuwa ikitoa wasomi wengi na wa hali ya juu toka enzi za ukoloni na baada ya uhuru.

Haishangazi basi, tarehe 9.11.1975, mkoa wa Mbeya ulitoa mwanamke wa kwanza na kuweka historia nchini kwa kuwa Waziri wa kwanza Mwanamke hapa nchini. Mwanamke huyo ni Mnyakyusa aitwaye Mh. Mama TABITHA IJUMBA WILFRED MWAMBENJA SIWALE.

Je, alizaliwa lini na alisoma wapi Mwanamama huyu wa kipekee hadi kuaminiwa na Baba wa Taifa?.

2. Bi TABITHA Azaliwa

Bi TABITHA alizaliwa mwaka 1939  katika kitongoji cha Bagamoyo mji wa Tukuyu ambayo ni makao   makuu ya wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.

3. BABU wa Bi TABITHA Alipendwa na Wakoloni

Wakoloni walimtumia babu ya Bi TABITHA aliyekuwa na uzoefu wa mambo mengi ya Kinyakyusa, kama anavyosimulia Bi TABITHA- Wakoloni walimtumia babu yangu mzaa baba kwa mambo mbalimbali na aliwasaidia sana hivyo wakampenda sana .

4. Ukoo wa MWAMBENJA Ulijaa Wasomi

Wakoloni, kutokana na kumpenda babu yake, wakawazawadia watoto wake, akiwemo Mzee WILFRED MWAMBENJA ambaye ndiye Baba yake Bi TABITHA, kusoma shule ya sekondari ya Malangali- "Wakoloni walimzawadia babu kwa kutoa fursa watoto wake, akiwemo baba yangu, kusoma shule ya Malangali. Hivyo, Baba yangu ni kati ya wasomi Wanyakyusa wa kwanza".

Shule ya Malangali, ambayo MZEE WA ATIKALI pia alisoma, ilianzishwa mwaka 1928 na imetoa viongozi wengi maarufu nchini.

Baba zake wengine Bi TABITHA mf HARRIDE MWAMBENJA alikuwa Daktari, ALEXANDER MWAMBENJA na JULIUS MWAMBENJA walikuwa Mahakimu wakati WILLIAM MWAMBENJA alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa TANU baada ya uhuru. "MWAMBENJA Avenue" Katumba, Tukuyu ndipo ulipo ukoo huu.

7. Elimu:

7.1 Elimu ya Msingi (1947-54)

Mwaka 1947, Bi TABITHA alianza masomo katika shule iliyoitwa "Native Authority Primary School" ambayo sasa inaitwa "Tukuyu Primary School". Baadaye, Bi TABITHA alisoma "Tosamaganga Girls Middle School" hadi mwaka 1955. Akiwa hapo, alikutana kwa mara ya kwanza na Bw. EDMUND SIWALE aliyekuwa akisoma "Tosamaganga Boys Middle School".

 "Mwanamke mwingine wa shoka"- Mama MARIA KAMM,  pia alisoma Tosamaganga Girls' School iliyoheshimika nchini kwa kuwaandaa vizuri wasichana kimasomo, kimaadili na kujitegemea.

7.2 Elimu ya Sekondari- (1955-57)

Baada ya kufaulu vizuri masomo ya msingi, Bi TABITHA alichaguliwa kujiunga na "Tabora Girls Secondary school" mwaka 1955 na kuhitimu mwaka 1957.

7.3 Elimu ya Maarifa

Bi TABITHA alipata mafunzo ya maarifa ya jamii katika shule ya sekondari ya wasichana ya Geita na taaluma ya Ualimu, chuo cha Ualimu Mpwapwa. Baadaye alienda Nairobi, Kenya alikopata shahada ya "Home Economics".

8. Bi TABITHA:- "Headmistress" Shupavu

Bi TABITHA alikuwa "Headmistress"  wa shule mbalimbali, kama anavyotiririka-:

"Nilianza kufundisha mwaka 1961, hata siku tunapata uhuru tayari nilikuwa Mwalimu".

8.1 Bwiru Girls Secondary school

Bi TABITHA alikuwa "Headmistress" wa shule hii ambapo mkazo wake mkubwa ulikuwa kumwendeleza mtoto wa kike kwenye nyanja zote.

Akiwa shuleni hapo, Bi TABITHA alikutana tena na Bw. EDMUND SIWALE aliyekuwa Mwalimu wa "Bwiru Boys Secondary School " na wakaoana na kubahatika kupata watoto wanne ambao ni FRED, MARY, ABEL & MAKA.

7.2 Korogwe Girls Secondary School

Baada ya kuiletea mafanikio makubwa shule hiyo, Bi TABITHA alihamishwa na kuwa "Headmistress" wa shule ya Korogwe Girls ambapo aliifanya iwike sana nchini enzi hizo. Bi TABITHA alijulikana nchi nzima kama "Headmistress Mnoko" ingawa alikuwa mfano wa kuigwa katika kuitekeleza siasa  ya ujamaa na kujitegemea kivitendo. Daima,  wanafunzi wa shule hiyo walishiriki vilivyo kwenye kilimo na kazi zingine za mikono. Aidha, Bi TABITHA alisisitiza sana wanafunzi kusoma kwa bidii. Hii ilipelekea wanafunzi wa shule hiyo wawe wanafaulu sana- "Niliweza kuzisimamia vizuri sana shule zile, kwa mfano Korogwe Girls ndiyo iliyokuwa ikiongoza kupeleka watoto wa kike Chuo Kikuu, Dsm. Mimi nilikuwa niko strict sana na sikuwa na simile na wanafunzi wazembe. Sasa nafurahia kuona matunda ya kuwa strict".

8. WAALIMU WAKUU Wapelekwa Chuo cha Kivukoni

Mwaka 1975, Walimu Wakuu wa shule zote nchini, akiwemo Bi TABITHA, walipelekwa kupata mafunzo chuo cha siasa Kivukoni, Dsm kwa mwaka mmoja. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa kuwafunza Wakuu hao ili nao waisafirishe elimu hiyo kwa wanafunzi wao. Bi TABITHA alienda kwenye mafunzo hayo na "Last born" wake MAKA aliyekuwa na umri wa miaka 3 tu.

9. Bi TABITHA Aitwa Ikulu

Jioni ya siku ya Jumatatu, tarehe 3 Novemba 1975,  Bi TABITHA, akiwa na Waalimu Wakuu wenzake kwenye mafunzo hayo darasani, aliambiwa na Mkufunzi kuwa kuna mgeni wake maalum. Bi. TABITHA alipotoka nje ya darasa alimuona Bi PERUZI BUTIKU,mke wa JOSEPH  NYERERE, ambaye alikuwa ni rafiki yake. Bi TABITHA alishtushwa sana na ujumbe aliopewa- "Bi Peruzi aliniambia Mwalimu amemtuma aje kunichukua kunipeleka Ikulu mara moja. Sikuamini!.

Bi TABITHA hakuamini kabisa. Baada ya Bi PERUZI kusisitiza sana ndipo Bi TABITHA alipokubali kwa shingo upande kuongozana nae. "Kwa kweli nilichanganyikiwa. Bi Peruzi aliposisitiza ilibidi niende kwa shingo upande huku nikiwa kwenye wingu zito la mawazo kwani sikuamini mtu mkubwa kama Rais aniite mtu kama mimi Ikulu".

Kutoka Chuo cha Kivukoni hadi Ikulu si mbali lakini siku hiyo Bi TABITHA alipaona ni kama kutoka Musoma hadi Mbeya!.

10. Mwalimu Amteua Bi TABITHA kuwa Mbunge

Bi TABITHA  na Bi PERUZI walipoingia kwenye geti la Ikulu mapigo ya moyo ya Bi TABITHA yalizidi kuongezeka. Mwalimu alipomuona Bi TABITHA katika hali ile alimtuliza kisha akamwambia kuwa amemteua kuwa Mbunge kwani Katiba inampa Rais mamlaka ya kuteua wabunge 10 wa viti maalum. Bi TABITHA hakuamini hivyo alimuomba Mwalimu arudie tena alichokisema ili ajithibitishie.  Hofu ilipomuisha, Bi TABITHA alikubali dhamana hiyo ingawa hakuelewa ni kwanini Rais alimpa heshma hiyo kubwa na ya kipekee.

Bi TABITHA alirejea chuoni akiwa na furaha tofauti na hofu aliyokuwa nayo alipokuwa akienda Ikulu. Akiwa chuoni, aliitunza siri hiyo bila kumwambia yeyote, kana kwamba hakuna kilichotokea!.

Siku hiyohiyo saa 2 usiku, redio Tanzania katika taarifa ya habari ikaeleza kuwa Mwalimu alikuwa amewateua watanzania 8 kuwa Wabunge wa kuteuliwa ambao ni TABITHA SIWALE, HADIJA SWEDI, ANNA KABATI, TITUS MPANDUJI, JULIE MANNING, DAVID MSUYA, WILBERD CHAGULA na TATU MAMAMPAKANI.

Ndipo Walimu Wakuu wenzake walipomwendea na kumpongeza sana kwa uteuzi huo mujarab.

11. Bi TABITHA Ateuliwa WAZIRI

Siku ya Jumapili, tarehe 9.11.1975,  Mwalimu alimwita tena Mh. Mama TABITHA na kumueleza kuwa amemeteua kuwa Waziri wa Nyumba, Ardhi ma Maendeleo Mijini na hivyo kuwa Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri nchini. Bi TABITHA alimueleza Mwalimu - "mbona mimi sio mtaalam wa mambo ya Ardhi?".

Mwalimu alicheka sana kisha akamjibu- "Mpaka nimekuteua ujue nimefanya utafiti wa kina. Nina imani kubwa na wewe. Utakwenda kujifunzia hukohuko kazini"

12. Mh. TABITHA Amshukuru Mungu

Baada tu ya kutoka  kuteuliwa Ikulu na kuweka historia ya kuwa Waziri wa kwanza Mwanamke TZ, Mh. Mama TABITHA alitoka Ikulu akawakusanya baadhi ya ndugu wachache na kwenda Masaki kwa mdogo wake ie Mama ROSE MWAMBENJA (Mama yake MZEE WA ATIKALI) ili kufurahia pamoja na kumshukuru Mungu.

13. MAMA ROSE MWAMBENJA Aangusha UGALI wa Nguvu!

Mama ROSE MWAMBENJA, licha ya kuwa na mtoto wa mwaka moja, Bi CARO MLIPANO @ "Manecha"), alipika ugali wa nguvu na wageni hao wachache  walifurahi sana na kumshukuru Mungu!.

14. Mh. Mama TABITHA Ang'ara Wizara ya Ardhi

Mh. Mama TABITHA alileta mabadiliko mengi kwenye wizara ya Ardhi. Mwaka 1980, alihamishiwa wizara ya Elimu. Hata hivyo, mwaka 1982 alirudishwa tena wizara ya Ardhi hadi 1984 alipostaafu na kubaki mbunge hadi mwaka 2000.

15. Mh. Mama TABITHA- Msomi, Mchapakazi na Mwadilifu

Mh. Mama TABITHA alikuwa mwadilifu sana ndio maana aliaminiwa na Baba wa  Taifa, Mwalimu JK NYERERE. Bi TABITHA alikuwa mchapakazi hodari aliyekuwa, mara kwa mara, akiagana na kitanda chake saa 10.30 alfajiri. Alitilia mkazo sana elimu hasa kwa mtoto wa kike na kuwasihi kusoma kwa bidii. Nasaha hizi pamoja na za wazazi wake, ndizo zilizopelekea mtoto wa mdogo wake, Dr. LUCY MLIPANO CHOVE (Dada wa MZEE WA ATIKALI) kufaulu na kupata Shahada ya  First Class (Hons) na hivyo kubakishwa Chuo cha Sokoine ambako ni Mhadhiri.

16. Mh. Mama TABITHA Atunukiwa Tuzo ya "MWANAMKE WA KARNE"

Mwaka 2000, Taasisi maarufu ya Kimarekani ilimtunukia Mh. Mama TABITHA "Tuzo ya Mwanamke wa Karne" kutokana na mchango wake mujarab kwa Taifa lake.

17. Mh. Mama TABITHA Ahudumu Bodi Nyingi

Kutokana na kuwa na weledi na uzoefu wa mambo mengi, Mh. Mama TABITHA amehudumu kama Mwenyekiti au Mjumbe kwenye Bodi nyingi mf PPF, NBC, DAFCO, NMC, Baraza la Chuo cha Ardhi, Women Advancement Trust nk.

18. Mh. Mama TABITHA's MOTTO

"Katika maisha yangu, neno SIJUI au SIWEZI kwangu mwiko. Kazi yoyote ukipewa kuifanya, ifanye kwa uwezo wako wote ili matunda yake yaonekane, na watu wakiiona kazi hiyo, wakukubali".
      26.5.2012

19. MWISHO:

Huyo ndiye Mh. Mama TABITHA IJUMBA WILFRED MWAMBENJA SIWALE, mwanamama mchapakazi hodari na mwadilifu aliyeaminiwa na Baba wa Taifa na kuteuliwa kuwa Waziri wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania.

Mama huyu wa kipekee anaishi Msasani mkabala na ilipo nyumba ya Baba wa Taifa.

Licha ya kugonga miaka 81, lakini ubongo wake bado unachemka sana na amekuwa akimwaga madini kwa watu mbalimbali.

20. TAFAKURI JADIDI:

Je, baada ya Mh. Mama TABITHA kuwa Mwanamke wa Kwanza kuwa Waziri na Mh. Mama SAMIA SULUHU HASSAN kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais, je ni mwanamke gani, miaka kadhaa ijayo, atakuja kuwa Mwanamke wa kwanza kuwa Rais hapa nchini? Au ni mpaka hawa wanafunzi wa kike waliopo mashuleni mf Bi. ATTU-JULITHA, wamalize shule?.

By MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️

April 5, 2020

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...