Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe, Simai Mohammed Said amewaomba Wazazi na Walezi kushiriki kikamilifu katika kuwasaidia watoto kuwasomesha wakiwa nyumbani kwao hasa katika wakati huu wa mlipuko wa maradhi ya Korona.
Akizungumza wakati alipozindua picha maalum inayohamasisha Wazazi kuwasomesha watoto, huko katika jengo la Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja, Mhe Simai amesema pamoja na kuwa wazazi wanatoka kwenda katika shughuli zao za kila siku, lakini bado wana jukumu la kuwasimamia watoto wao.
Amesema Wizara ya Elimu Zanzibar itaendelea kuunga mkono Juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanakuwa katika usalama, pia kuhakikisha wanaendelea kupata Elimu yao wakiwa nyumbani kwao kutokana na kufungwa Skuli na madrasa katika kipindi hiki cha maradhi ya korona, pamoja na kuendelea kutoa taarifa na maelekezo mbalimbali ya kielimu.
Hivyo amewaomba wazazi kuendelea kuwasimamia watoto wao kwa kuwadhibiti kutoka ovyo katika nyumba zao na kufuata masharti ya wataalamu wa Afya ili kuweza kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo.
Nae Naibu Katibu Mkuu Utawala na uendeshaji Wizara ya Elimu, mwalim Abdullah Mzee Abdullah amesema katika kipindi hiki cha kufungwa Skuli kulikosababishwa na kuwepo maradhi ya Korona, Wizara hiyo imeandaa Kamati ya wataalamu kutoka Sekta mbalimbali ili kuandaa mikakati ya kuwawezesha watoto kusoma wakiwa nyumbani ili kupunguza athari za kufungwa Skuli.
Amesema Kamati hiyo imeweza kuandaa vipindi mbalimbali katika Radio na Runinga, hivyo ni jukumu la wazazi kuvifuatilia kwa karibu vipindi hivyo na kuwa karibu na watoto wao kwa kuwasaidia ili malengo yaweze kufikiwa.
Aidha amewaomba wahisani kuendelea kutoa misaada katika Wizara ya Elimu kutokana na kuwepo kwa baadhi ya jamii kushindwa kumiliki Redio kwa ajili ya kuwapa watoto wao kuweza kufuatilia na kusikiliza masomo hayo.
Pia amesema WEMA inashirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania Bara ambapo tayari wameandaa masomo ya Sayansi na Hesabu kwa Wanafunzi wa Kidatu cha Tano na Cha sita ambapo tayari wameshakabidhiwa na waakati wowote yataanza kurushwa katika vutuo hivyo vya Radio na Runinga.
Nae Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa kinaloshughulikia masuala ya Elimu Zanzibar UNICEF, bibi Maha Damaj amesema katika kipindi hiki cha kuwepo Maradhi ya Korona hapa Zanzibar ni vizuri WEMA imetoa vipindi hivyo katika vyombo vya Habari ili watoto wasikae na kutosahau masomo yao.
Hivyo ameishukuru WEMA na kuipongeza kwa hatua nzuri waliyoichukua katika kuwasaidia watoto kupata Elimu kama inavyostahiki.
Kwa upande wake mchoraji wa picha hiyo Sei Soud Ali ameishukuru Wizara ya Elimu kwa kumuamini kuchora picha hiyo ikiwa ni mzazi katika kuwahamasisha wazazi wenziwe kuwasimamia watoto wao.
Aidha ameahidi kuendelea kuitumikia nchi yake kwa kuchora picha mbali mbali zenye kutoa Elimu kwa jamii kwa kutimiza
uzalendo kwa nchi yake.
Picha hiyo imezinduliwa ikiwa na ujumbe wa ELIMU YA WATOTO WETU NI JUKUMU LETU
![]() | |
|
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe, Simai Mohammed Said akizindua picha maalum inayohamasisha Wazazi kuwasomesha watoto katika jengo la Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...