Na Emmanuel J. Shilatu
Ni
miaka 56 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na Wazanzibar
liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri Muungano wa
Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. Hii ilitokana na ujasiri,
ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano huu,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume
(Zanzibar).
Hatua hiyo
ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na mahusiano ambayo
yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote mbili (Tanganyika
na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi, kitamaduni na
kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana
na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa kwamba Visiwa
vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata kushikamana
kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika. Hivyo tangu awali
tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya pamoja.
Pia
kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni baina ya
Wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama kuolewa
ilizidi kushamiri baina yao.
Halikadhalika
harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze kujitawala wenyewe
kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia kutuunganisha. Inaaminika
(na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya Wazanzibar walishiriki
kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Mwingereza
ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya pamoja walifanikiwa kupata
Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini
pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika mchakato wa
Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia kubwa ya mchango
wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda yake yalionekana
ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja wa Gombani Pemba
yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na hila na ghiliba za
Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne mbili na hatimaye
waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia
tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere ya
kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake zilianza
kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa kuiunganisha
Tanganyika na Zanzibar.
Mnamo
April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa zinaunda
Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya Tanganyika) na
Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar ) walitia sahihi
Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao, unaojulikana kama “Hati ya
Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of Tanganyika and Zanzibar
(URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria na unaotambulika
Kikatiba.
Siku ya
Jumatatu ya tarehe 26 Aprili, 1964 viongozi wa nchi zote mbili
walikutana katika ukumbi wa Karimjee kwa nia ama lengo moja tu la
kubadilishana “Hati za Muungano”.
Wananchi
wa Tanzania walipiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa kwanza
kabisa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwaka 1965.
Kama
nilivyodokeza kwamba Muungano wa Tanzania ulifikiwa kwa kutiwa sahihi
mkataba unaoitwa Hati ya Muungano (Articles of the Union) na wakuu wa
nchi hizi mbili, Mwalimu Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar)
Aprili 22,1964 na kuridhiwa na mabunge ya nchi hizo Aprili 25, 1964 na
hatimaye kuwa sheria ya Muungano ya (Acts of Union) ya mwaka 1964.
Kimsingi
sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha na ndiyo iliyopewa haki ya chombo
cha kikatiba kinachodhibiti katiba zote mbili za Serikali ya Muungano.
Mwanzoni
kabisa Hati ya Muungano (Articles of Union) iliyomo ndani ya sheria ya
Muungano iliorodhesha na hata kudadavua mambo 11 ya Muungano. Mambo hayo
ni kama vile:- Mambo ya nchi za nje, Ulinzi na usalama (lakini si
usalama wa Taifa); Polisi, Uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nchi
za nje, utumishi katika serikali ya Muungano, kodi ya mapato, usimamizi
wa fedha, Bandari, Usafiri wa anga, Posta na simu.
Kwa
nia safi na malengo mazuri yanayojitokeza Hati ya Muungano imekuwa
ikiboreshwa zaidi kwa kadri siku zinavyozidi kusonga mbele kwa malengo
kusudi ya kuleta umoja, mshikamano, amani na utulivu wetu ule ule
tulioanza nao awali na halikadhalika maridhiko yanayoendelea kuufanya
Muungano huu uendelee kudumu hadi hii kesho.
Ndio
maana mtu timamu hatoshangaa sana kuona Hati ya Muungano ikiendelea
kuboreshwa kila siku (na itaendelea hivyo) ambapo ilianzia na mambo 11
ambapo hii leo yamefikia takribani 23.
Mengineyo
ama baadhi ya yale yalioongezeka ni kama vile;- Noti; Elimu ya juu,;
Maliasili na mafuta (mafuta) yasiyochujwa, bidhaa za mafuta na gesi
asilia , ya mwaka 1968; Baraza la Mitihani ya Taifa; utafiti; utabiri wa
hali ya hewa; Takwimu,; Mahakama ya Rufaa ya juu ya mwaka 1979; pamoja
na uandikishwaji wa vyama vya kisiasa .
Tusisahau
mwaka 1965 iliundwa katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(The Interim Constitution of The United Republic of Tanzania) mpaka
kufikia mwaka 1977 ndipo ilipoundwa katiba ya kudumu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inaendesha nchi hadi sasa.
Muungano
huu tulionao unawafanya wale wageni, mataifa ya nje na watu wote wenye
hila, donge, roho ya korosho kuogopa kutugusa na kutuvuruga kutokana na
kuwepo kwa nguvu kubwa ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina yetu.
Muungano
huu wetu unatupatia fursa kubwa ya uhuru wa kusafiri kwa pande zote iwe
ni bara ama ni visiwani. Leo hii ni rahisi sana kwa mtu wa bara kwenda
Visiwani na hata wale wa Visiwani kuja Bara kwa uhuru zaidi kwani Uhuru
huo wa uwepo wa nafasi hiyo umeshalipiwa na huu Muungano wetu tulionao.
Kutokana
na uwepo wa uhuru wa kusafiri usio na mipaka baina yetu, pia Muungano
wetu tulionao unazidi kutuongezea fursa na nafasi zaidi ya uwanja mpana
wa ufanyaji biashara. Hali hii imesababisha uwepo wa mzunguko mkubwa wa
pesa ndani yetu kwani si jambo la ajabu kuona pesa zikitoka Visiwani
(Zanzibar) kuja Bara (Tanganyika) kupitia mabadilishano ya bidhaa kama
vile nafaka, kahawa, matunda, vipuri vya magari na kadhalika.
Pia
si jambo geni tena kwa sasa kuona pesa zikivuka Bahari na kwenda
visiwani Zanzibar kwa ajili ya ufanyaji ama ununuzi wa biashara kama
vile Magari, nazi, Karafuu, Tende na kadhalika.
Muungano
huu unatuzidishia fursa ya mianya ya uwanja mpana tena usio na kikomo
wa ufanyaji biashara, Muungano huu hautubagui ama kutojulisha au kuwa na
upendeleo wa upatikanaji wa Elimu bora, huduma za kijamii bora,
Muungano hautugawi wala kuwa na upendeleo bali umejaa uwiano sahihi wa
upatikanaji wa mabo yote ya msingi yaliyomo ndani ya “Hati ya Muungano”
(Articles of union). Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima
wa nyanja za kimaisha yetu.
Ni
ukweli uliodhahiri kuwa haitakaa itokee Muungano kama huu (wa
Tanganyika na Zanzibar) hapa Barani Afrika umoja ushirikiano,
ushikamano, amani na utulivu ni sehemu mojawapo ya manufaa ya Muungano
huu.
Hakika, historia
tunailinda na kuiheshimu. Njia mojawapo ya kuwaenzi vyema waasisi wetu
ni kwa kuudumisha Muungano wetu ambao ni urithi wa aina yake
waliotuachia. Watanzania yatupasa tuenzi Muungano wetu kwa kuulinda na
kuudumisha kwa vitendo kwani ni nguzo na fahari ya kipekee na ya aina
yake Barani Afrika.
0767488622
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...