Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za
rambirambi kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Job Yustino Ndugai na wananchi wa Jimbo la Sumve Mkoani Mwanza kufuatia kifo
cha Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Richard Mganga Ndassa.
Mhe. Ndassa
amefariki dunia ghafla leo tarehe 29 Aprili, 2020 Jijini Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli
amesema “Nimesikitishwa
na taarifa za kifo cha ghafla cha Mhe. Ndassa, nakumbuka mimi na yeye tulianza
pamoja Ubunge mwaka 1995, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Sumve na mimi nikiwa
mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki ambalo sasa hivi linaitwa Jimbo la Chato,
namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina”
Mhe. Rais Magufuli
amemuomba Spika, Mhe. Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya
Marehemu, Wabunge, wananchi wa Sumve pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote
walioguswa na kifo cha Mhe. Ndassa.
Amewataka wafiwa
wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki
kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
29 Aprili,
2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...