*Aruhusu bodaboda kuingia katikati ya Mji
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema ataendelea kuchukua
hatua za kila namna katika kuhakikisha anawalinda wakazi wa Dar es
Salaam dhidi ya mlipuko wa virusi vya Corona na hiyo ni pamoja na
kupuliza madawa katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza
na wananchi katika kituo cha mabasi cha Makumbusho leo jijini Dar es
Salaam Makonda amesema kuwa upuliziaji wa madawa katika maeneo
mbalimbali unaendeleaje na kuna mpango wa kutumia helikopta katika zoezi
hilo ili kuwaweka wakazi wa Mkoa huo salama zaidi.
Pia
Makonda amesema kuwa kutokana na hali ya uchumi wamiliki wa nyumba,
vyumba na majengo ya biashara ni vyema wakapunguza kodi kwa asilimia 50
katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona.
"Wananchi
wa hali ya chini wanategemea biashara ambayo kwa sasa haiendi vizuri,
ninawaomba wamiliki wa vyumba, nyumba na majengo ya biashara kushusha
kodi kwa asilimia 50 ili kuwawezesha wananchi kubaki na fedha za kununua
chakula katika kipindi hiki wanachoshauriwa kubaki ndani" ameeleza
Makonda.
Aidha Makonda
amewataka wazazi kuwalinda watoto ambao wapo majumbani baada ya shule
kufungwa na kuwataka wale wote wasio na shughuli za msingi kusalia
majumbani.
Wakati huo huo
Makonda amewaruhusu waendesha wa pikipiki maarufu kama bodaboda kuingia
katikati ya Mji na kubeba abiria ila kwa kuzingatia Sheria zilizopo
ikiwemo kuvaa kofia ngumu (helmet) pamoja na kutopita kwenye barabara za
mwendokasi.
"Mna ruhusa
ya kuingia katikati ya Mji na kubeba abiria na zoezi hili litaendelea
hadi pale amani, afya na Corona itakavyoondoka nchini" amesema.
Kuhusiana
na wageni kuingia ndani ya nchi Makonda amesema kuwa utaratibu wa
wageni hao kuwekwa karantini kwa siku kumi na nne unazingatiwa na
kuwataka wale wote wenye ndugu wanawasili nchini kutokwenda kuwapokea na
kuacha majukumu hayo kwa Serikali ya Mkoa na madaktari na kuwashauri
wananchi wa Mkoa huo kwenda hospitali pindi watakapohisi kuwa na dalili
za Corona.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...