*Pia ataka kila familia ijadili inavyoweza kukabiliana na virusi vya Corona


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WANANCHI wa Jiji la Dar es Salaam ambao wanatoka kwenda kwenye shughuli mbalimbali wanatakiwa kuvaa barakoa kuanzia Jumatatu ya Aprili 20, mwaka huu kama hatua ya kukabiliana na virusi vya Corona na atakayekaidi atachukuliwa hatua kali.

Akizungumza leo Aprili 18, 2020 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema kuwa kuanzia Jumatatu watu wa Jiji hilo watatakiwa kuvaa barakoa na wale ambao watakaidi watachukuliwa hatua kali huku akisisitiza kuwa ni wakati kila mwananchi kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huo badala ha kufanya mzaha.

" Serikali imekuwa ikichukua hatua zote kuhakikisha tunapambana na Corona.Ni ugonjwa mbaya sana maana ni kama vile unapambana na adui ambaye haonekani.Hivyo tunalojukumu la kuchukua hatua madhubuti ya kukabiliana na Corona,"amesema Makonda na kusisitiza kuwa kuna haja ya kuchukua hatua zaidi.

Hivyo ameeleza wazi anafahamu kuwa wananchi wamekuwa wakitoka majumbani na kwenda kwenye shughuli zao za kila siku lakini sasa watu wote wahakikishe kabla ya kutoka nyumbani wawe wamevaa barakoa ili kupunguza kasi ya maambukizi.

Pia amesisitiza umuhimu wa watu kukaa umbali wa mita moja moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine na kwamba utaratibu huo unatakiwa kufanyika kila mahali na kuongeza umefika wakati viongozi katika masoko yote ya Jiji la Dar es Salaam kuweka mfumo mzuri ambao utawezesha watu kufanya shughuli zao huku wakiwa wamechukua tahadhari zote.

" Katika masoko yetu kuanzia Jumatatu nako tunataka kuona kunakuwa na utaratibu mzuri ukiwemo wa kuachiana nafasi lakini pia wakiwa wamevaa barakoa,"amefafanua Makonda na kuongeza ukienda sokoni nunua unachotaka na kisha ondoka.

Wakati huo huo Makonda ameonesha kukasirishwa na baadhi ya watu ambao licha ya Serikali kufanya jitihada zote za kukabiliana na Corona ukiwemo utoaji  elimu lakini wao bado wanafanya utani kwenye janga hilo.

Hivyo amesema  itakuwa vizuri kama kutakuwa na vikao kwa kila familia na kisha kujadiliana kama wako tayari kufa kwa Corona au laa kwani haiwezekani Serikali inachukua kila aina ya hadhari lakini watu wanashindwa kuyafuata.

"Serikali imeamua kufunga shule lakini kuna baadhi ya wazazi wanakwenda kwenye klabu za muziki na kumbi za starehe na matokeo yake wanapeleka Corona nyumbani bila sababu,"amesema Makonda.

Amesisitiza hakuna sababu ya kutumia nguvu katika kukabiliana na ugonjwa huo, lakini itakuwa bora iwapo kila mmoja wetu atachukua hatua kwa kufuata maelekezo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...