Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa maagizo kwa Machifu na Waganga wa Tiba asili wa mkoa wa
Rukwa (hawapo pichani) katika kikao kifupi alichokutana nao ili
kuwaelimisha juu ya ugonjwa wa Corona

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (aliyekaa katikati) pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa
Benard Makali (Kushoto) na kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt.
Emanuel Mtika katika Picha ya pamoja na baadhi ya Waganga wa Tiba Asili
wa mkoa wa Rukwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (aliyekaa katikati) pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa
Benard Makali (Kushoto) na kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt.
Emanuel Mtika katika Picha ya pamoja na baadhi ya machifu wa mkoa wa
Rukwa.
*********************************
Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza machifu pamoja na waganga wa tiba
asili ndani ya mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwa na ndoo za maji
yanayotitirika na sabuni katika maeneo yao ya kazi ili kuwahamasisha na
kuwaelimisha wateja wao wanaowapa huduma kuelewa umuhimu wa kunawa
mikono ili kujikinga na ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa
haitakuwa na maana kama wamepata elimu halafu hawaitumii hali ambayo
hakutakuwa na wa kumlaumu endapo ugonjwa huo utasambaa na kuangamiza
watu, alisisitiza kuwa kutowaelimisha wateja wao na kushindwa kuchukua
tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ni sawa na kulisaliti taifa, ikiwa
serikali inaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa elimu ya ugonjwa huo
kwa kutumia njia mbalimbali.
“Kwa upande wa
maji mimi kwangu ni agizo, machifu wote muwe na ndoo ya maji tiririka na
sabuni, muoneshe mfano, waganga wa tiba za asili, na nyinyi wote kwa
umoja wenu mkawe na ndoo za maji tiririka na sabuni na elimu mmeipata
vizuri, haitakuwa na maana kama mmepata elimu halafu kule mnakwenda
hamuitumii halafu ugonjwa unakuja unatuangamiza, utamlaumu nani na elimu
tumekupa, itabidi ujute kwamba wewe ni msaliti, umelisaliti taifa,
umemsaliti na mungu pia,” alisema.
Mh. Wangabo
ametoa maagizo hayo kwa nafasi yake kuwa kiongozi wa machifu mkoani
Rukwa, katika kikao kifupi kilicholenga kutoa elimu ya ugonjwa wa Corona
kwa machifu pamoja na viongozi wa waganga wa tiba asili wakiwemo wa
Chama cha Waganga/ Wakunga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Mkoani Rukwa
(CHAWATIRU).
Aidha, Mh.
Wangabo aliwataka machifu hao kukemea mila zinazowezesha kusambaa kwa
ugonjwa wa Corona kwa haraka, ikiwemo watu zaidi ya mmoja kutumia chombo
kimoja kunywa pombe za asili, familia kutumia chombo kimoja kutumbukiza
mikono kwaajili ya kunawa, pamoja kutumia chombo kimoja cha kuchotea na
kunywea maji katika mtungi.
Halikadhalika
aliwataka waganga wa tiba asili kuwa na utatratibu wa kulipwa kwa
kutumia huduma za mitandao ya simu ama benki ili kuepuka kushika fedha
za wagonjwa ambao hawajulikani ugonjwa wao huku akisisitiza kutotowa
dawa zinazopelekea mtu kupiga chafya kwa wingi jambo ambalo sio zuri
hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa
Corona.
Kwa upande wake,
kaimu mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika aliwatahadharisha
kuwa kuwatibu wagonjwa wa Corona ni gharama kubwa sana kiasi ambacho
endapo ugonjwa huo utasambaa watu wengi wanaweza kupotea kwa kushindwa
kufuata maelekezo ya wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.
“ Kumtibu mgonjwa
mmoja kwa siku ni shilingi milioni 48 na mgonjwa anatakiwa atibiwe kwa
siku 15, je sisi huo uwezo tunao, hiki kitu kikitutokea huku sisi
tutakwisha na ndio maana namshukuru mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa kuona
umuhimu wa kuitana ili tuelezane ukweli, hiki kitu kikitokea kwetu
tutakwisha, kwahiyo nawaomba sana tutumie zile njia za kawaida za
kupambana na hili janga,”Alisema.
Pia aliwataka
waganga wa tiba asili pindi hasa wale wanaoishi katika mipaka ya Zambia
na Kongo kuhakikisha wanapojiwa na mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa
corona ni vyema wakamshauri au kumpeleka katika kituo cha afya kwa
uchunguzi zaidi, au kuwasilisna na uongozi wa Kijiji kwa hatua zaidi.
Aidha, katika
kukazia hilo afisa afya wa mkoa alishauri kuwa endapo mtu hana uwezo wa
kununua ndoo ya maji tiririka kutokana na gharama yake anaweza kutumia
kibuyu chirizi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...