Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza jambo wakati alipotembelea kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) cha Amana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuona namna ambavyo madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo watakavyoweza kutoa huduma kwa wagonjwa hao.
Msimamizi wa kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) Dkt. Stanley Binagi akielezea jinsi wanavyowahudumia wagonjwa hao wakati wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walipotembelea kituo hicho leo ili kuona namna ambavyo watatoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa hao.
Wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa katika picha ya pamoja mara walipomaliza kikao chao na uongozi wa kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) cha Amana jijini Dar es Salaam. Wataalamu hao walitembelea kituo hicho kwa ajili ya kuona namna ambavyo watatoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wanaotibiwa
katika kituo hicho.  Picha na JKCI

*******************************

Na Mwandishi maalum – Dar es Salaam

24/04/2020 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itawahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo yanayohitaji matibabu ya kibingwa walioko katika kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) cha Amana jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Janabi alipotembelea kituo hicho kwa ajili ya kuona ni namna gani wataalamu wa Taasisi yake wataweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo.

Prof. Janabi alisema licha ya Taasisi hiyo kwenda katika kituo hicho kutoa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo pia itatoa mafunzo kwa vikundi vya watu wachache kwa wafanyakazi wa Hospitali hiyo ambayo yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona.

“Mimi pamoja na wataalamu wangu tumekuja hapa ili kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wagonjwa. Kwani wagonjwa wa Corona ambao wanamatatizo ya moyo wanahitaji kupata huduma za matibabu walizokuwa wanazipata kabla hawajapata maambukizi”,.

“Pia tutatoa mafunzo katika makundi ya watu wachache kwa wataalamu wa afya ya jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa hasa wenye matatizo ya moyo”, alisema Prof. Janabi.

Kwa upande wake Dkt. Stanley Binagi ambaye ni msimamizi wa kituo hicho alisema baadhi ya wagonjwa waliopo katika kituo cha Amana wanasumbuliwa na magonjwa mengine ikiwepo moyo, figo na kisukari yanayohitaji matibabu ya kibingwa .

“Ninawashukuru Wataalamu kutoka JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambao mmefika katika kituo hiki na kuona jinsi gani mnaweza kushirikiana na sisi katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa COVID -19”.

“Kupatikana kwa huduma za matibabu kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa hawa”, alisema Dkt. Binagi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...