
Kupongeza juhudi
za Serikali dhidi ya Mapambano ya Mlipuko wa Maradhi yanayosababishwa na virusi
vya Corona
Itakumbukwa kuwa katikati
ya mwezi Machi mwaka huu Serikali ilitangaza mapambano rasmi dhidi ya maradhi
yanayosababishwa na virusi vya Corona ambavyo hivi karibuni imekuwa ni janga
kubwa duniani.
Serikali
ilichukua uamuzi huo baada ya Tanzania kuanza kupata taarifa za uwepo wa
wagonjwa wa maradhi hayo nchini na hivyo kuwataka Wananchi kuchukua tahadhari
mbalimbali za kujikinga na maradhi hayo ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa
maji safi yanayotiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa Barakoa na kujiepusha na misongamano.
Kufuatia uamuzi
huo, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inatambua na inaipongeza
Serikali kwa uamuzi huo kwani ni hatua nzuri ya kulinda haki ya afya ya
wananchi wake pia ni hatua muhimu katika kupunguza maambukizi ya maradhi hayo
kwa jamii.
Kipekee kabisa Tume inaipongeza Wizara ya Afya na watendaji wake ikiwemo
Madaktari, Manesi na Wahudumu wengine kwa kazi kubwa wanayoifanya ya
kuhamasisha, kuelimisha na kutoa huduma stahiki kwa wananchi ambao tayari
wamepata maambukizi ya maradhi hayo.
Tume inatumia fursa hii pia kuwapongeza jumuiya za AZAKI na
Wafanyabiashara waliojitokeza kuunga
mkono kwa hali na mali jitihada za Serikali katika kupambana na maradhi hayo.
Aidha, Tume inaiomba jamii kutofanya mzaha na jambo hili, janga hili ni kubwa hivyo ni
muhimu kuunga mkono jitihada za serikali kwa kufuata maelekezo sahihi yanayotolewa
ikiwemo wale wote washukiwa wa maambukizi na wenye maambukizi kukaa Karantini
kwa muda uliopangwa ili kuzuia maambukizi ya ndani yasiongezeke.
Mwisho, Tume
inatoa ushauri kwa Serikali na jamii kama ifuatavyo:
1.
Jamii iendelee kuzingatia maelekezo ya kujikinga yanayotolewa
mara kwa mara na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
2.
Tume inaomba wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika
mapambano dhidi ya maradhi hayo.
3. Serikali
iendelee kuchukua tahadhari hususani katika mipaka yetu ili kuzuia kuingia k
4. Tume inaiomba Serikali kuliangalia kipekee kundi la Watu
wenye Ulemavu kwani wao wanahitaji msaada zaidi kukabiliana na mlipuko wa
maradhi ya Virusi vya Corona, ikiwemo kuwapatia taarifa sahihi kupitia njia
sahihi, kwa mfano Viziwi wapatiwe
taarifa kwa lugha ya alama na Watu Wasioona waandaliwe taarifa zao kupitia
machapisho mbalimbali ya nukta nundu, kuwapa huduma bora za afya na kuwalinda dhidi
ya unyanyapaa.
5. Tume inavishauri vyombo vya habari hususani Luninga
vifuate mfano wa Shirika la Habari la Taifa (TBC) kwa kuweka kipengele cha
msomaji wa habari wa lugha ya alama wakati wa kurusha matangazo yao
ili Viziwi nao waweze kuelewa taarifa zinazorushwa na vyombo hivyo.
Imetolewa
na:
(SIGNED)
Jaji
(Mst) Mathew Pauwa Mhina Mwaimu
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Aprili 16, 2020
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...