Charles James, Michuzi TV
KUTOKANA na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia kutoka analojia kuelekea digitali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kutumia mfumo wa ujazaji matamko ya rasilimali na madeni kwa njia ya mtandao.

Mfumo huo umeanzishwa ili kutekeleza sera ya serikali mtandao (e-goverment) ambayo serikali imeelekeza Wizara, Idara, Taasisi na Mashirika yote ya Umma kutumia mfumo wa tehama katika kurahisisha mawasiliano na utendaji kazi.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Harold Nsekela mbele ya wandishi wa habari jijini Dodoma leo.

Haji Nsekela amesema mfumo huu wa ujazaji fomu mtandaoni utawawezesha viongozi kujaza matamko yao kwa urahisi na ufanisi zaidi popote pale walipo iwe ndani au nje ya Nchi.

" Mfumo huu utampunguzia kiongozi usumbufu wa kutumia muda mrefu kusafiri kutoka eneo lake la kazi kwenda katika Ofisi za Sekratarieti Makao Makuu jijini Dodoma au katika ofisi zetu za Kanda ambazo pia ni chache kwani zipo katika kanda nane nchini.

Lakini pia ujazaji huu wa fomu utaepusha upotevu wa fomu za matamko katika zoezi la urejeshaji unaotokana na usafirishaji kwa njia ya posta au katika vyombo vingine vya usafiri," Amesema Jaji Nsekela.

Amesema mfumo huo pia utaepuka uwezekano wa kupokea matamko kutoka kwa watumishi ambao sio viongozi kwa mujibu wa sheria ya Maadili ya viongozi wa umma na.13 ya mwaka 1995. 

Katika mfumo huu mpya wa mtandaoni, kiongozi atakayejaza tamko atakua ametengenezewa akaunti ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma hivyo matamko yatakayopokelewa yatakua ya viongozi wanaowajibika na sheria ya maadili.

Amewataka viongozi wanaoteuliwa au kupandishwa cheo na kuwajibika na sheria hiyo na wanaokoma uongozi wanapaswa kutuma taarifa zao kwa Sekretarieti kupitia anuani ya barua pepe helpdesk@ethicssecretariet.go.tz ili waweze kutengenezewa akaunti za kuingilia mfumo huo.

Hayo yote yanafanyika kwa kuzingatia sheria ya maadili ya viongozi wa umma kifungu cha 9(1) (b) kinachomtaka kiongozi wa umma kila mwisho wa mwaka kabla ya Desemba 31 awe amewasilisha tamko lake kwa Kamishna wa Maadili linaloonesha rasilimali zake, au mume na watoto wake wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa wala kuolewa.

Haji Nsekela amesema ni kosa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko lake la rasilimali na madeni bila sababu za msingi.

Akizungumzia hali ya maadili kwa sasa nchini kwa viongozi wa umma, Katibu Usimamizi wa Maadili, John Kaole amesema inaridhisha kulinganisha na miaka ya nyuma wakati mfumo wa vyama vingi unaingia.

" Kiukweli kwa sasa hali ni nzuri hasa kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano, maadili yamekua kwa kasi na kipimo sahihi ni namna ambavyo ubora wa utoaji huduma katika ofisi za serikali ulivyoongezeka," Amesema Kaole.
 Katibu Usimamizi wa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, John Kaole akieleza namna ambayo maadili yameongezeka katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano.
 Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Harold Nsekela akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma.
 Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Harold Nsekela akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma leo.
Katibu Usimamizi wa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, John Kaole akieleza namna ambayo maadili yameongezeka katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya tano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...