PATRICIA KIMELEMETA
Daktari wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, Lucy Mpayo amesema kuwa, ulinzi wa watoto walio chini ya miaka mitano unaanzia kwa mzazi/ mlezi na jamii kwa ujumla.
Dk. Lucy amesema kuwa, watoto hao wanapaswa kuangaliwa kwa ukaribu kwa sababu uwezo wao wa kujilinda bado ni mdogo na kwamba hawawezi kupambana na hatari yoyote inayojitokeza dhidi yao.
Amesema kuwa, kutokana na hali hiyo, wazazi,walezi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuwalinda watoto hao hali ambayo inaweza kuwasaidia kuepusha hatari zonazoweza kuwakabili.
"Ulinzi na usalama wa watoto walio chini ya miaka mitano unapaswa kuangaliwa na wazazi, walezi na jamii inayowazunguka kwa ujumla wake,kwa sababu watoto hao bado wadogo na kwamba hawawezi kupambana na hatari zinazowakabili," amesema Dk. Lucy.
Ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kufuatilia mienendo ya michezo ya watoto hao pamoja na kuondoa vitu vyote vya hatari kama vile kisu, panga, moto na kadharika ambavyo kwa namna moja au nyingine vinaweza kusababisha madhara kwa watoto hao.
Amesema kuwa, watoto wanapaswa kutumia vifaa vya michezo ambavyo sio hatarishi kulingana na umri wao,kama vile mipira, mwanasesere,magari na kadharika,hali ambayo haitahatarisha maisha yake.
"Tunapaswa kuwalinda watoto wetu na hatari zote zinazoweza kujitokeza, jambo ambalo litasaidia mtoto kukua katika mazingira mazuri na ubongo wake kukomaa ipasavyo," amesema.
Amewataka wazazi hao kuhakikisha kuwa, kila wakati wanawaangalia watoto hao kwenye mazingira wanayocheza ili kuhakikisha kama ni salama na kwamba hawawezi kupata madhara yoyote.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...