Na Woinde Shizza, Arusha
WAZIRI wa viwanda,biashara na masoko, Innocent Bashungwa ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) mkoani Arusha kufanya maamuzi ya haki na usawa katika uchunguzi wa mgogoro wa kiwanda cha kuchakata,kusindika na kufungasha nyama cha Happy Sausages kilichopo jijini Arusha.
Bashungwa, ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho huku akiongoza na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Akizungumza kiwandani hapo Bashungwa amesema kwamba Takukuru wapo katika hatua za mwisho kukamilisha uchunguzi wao na anaamini kwamba taasisi hiyo itatenda haki katika uchunguzi wao.
Mbele ya kamanda wa Takukuru mkoani Arusha,Frida Wikesi waziri huyo ametamka kwamba serikali inafuatilia kwa ukaribu mgogoro uliopo kiwandani hapo na hivyo itazingatia maslahi ya uchumi wa viwanda.
"Ninatambua taarifa ya Takukuru ipo kwenye hatua ya mwisho na ninaamini Takukuru itaangalia haki, hatutaki kuona mgogoro huu unaathiri uchumi wa viwanda nchini" amesema Bashungwa
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Andrew Mollel amesema kwamba kutokana na mgogoro huo kiwanda chake kimeshindwa kupata mkopo kutoka benki ya KCB na kupelekea kukwama kuwalipa wafugaji wanaoleta bidhaa mbalimbali kiwandani hapo .
"Takukuru walichukua hati zote za ardhi zilizokuwa kwa msajili wa hati Moshi na hivyo mpaka sasa uchunguzi haujakamilika na hati hazijarudishwa kutokana na hilo kiwanda kimeshindwa kupata mkopo kutoka benki ya KCB" alisema Mollel
Mollel,amesema kwamba kwa hali ya sasa biashara asilimia sabini ya biashara kiwandani hapo zimeyumba kutokana na masoko yao ambayo ni hoteli za kitalii,makampuni ya utalii kufunga biashara zao kutokana na kukosa wageni sababu ya ugonjwa Covid-19.
Hatahivyo, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema kwamba awali aliunda tume kuchunguza mgogoro huo na ilishakamilisha uchunguzi wake lakini wanasubiri ripoti ya Takukuru ili waweze kujumuisha kwa pamoja na kutoa ripoti kamili.
Waziri wa viwanda,biashara na masoko, Innocent Bashungwa akizungumza na uongozi wa kiwanda cha kufungasha, kuchakata nyama cha Happy Sausages kilichopo jijini Arusha wakati alipofanya ziara juzi katika kiwanda hicho ambapo aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) mkoani Arusha kufanya maamuzi ya haki na usawa katika uchunguzi wa mgogoro wa kiwanda hicho.
Picha na Woinde Shizza, Arusha
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...