Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewasha umeme
katika maeneo kadhaa ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na kusisitiza viongozi
wa wilaya, vijiji na vitongoji kutoa kipaumbele kwa taasisi za umma zilizo
katika maeneo yao ili ziunganishiwe nishati hiyo muhimu.
Akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo, Aprili 19
mwaka huu, Dkt Kalemani alibainisha kuwa kipaumbele cha Serikali kupeleka umeme
vijijini ni katika kuhakikisha taasisi zote za umma zinakuwa na umeme ili
kuziwezesha kutoa huduma bora zaidi.
Alisema kuwa, Rais John Magufuli ametoa pesa nyingi
kwa lengo la kupeleka umeme vijijini, hivyo ni lazima fedha hizo zitumike kwa
busara katika kukidhi mahitaji ya wananchi walio wengi, hususan katika
kuboresha huduma za afya, elimu, maji, kilimo pamoja na uanzishwaji viwanda
vidogo vidogo.
“Ndugu zangu viongozi, nawasisitiza mhakikishe taasisi
zote za umma katika maeneo yenu zinalipiwa gharama ya kuunganisha umeme ambayo
kwa vijijini ni shilingi elfu 27 tu ili ziunganishiwe nishati hiyo na hivyo
kuboresha huduma.”
Akizungumza kwa nyakati tofauti na viongozi wa vijiji
vya Milade na Mkalama baada ya
kuwasha umeme katika Zahanati za vijiji hivyo, aliwapongeza kwa kuona umuhimu
wa kulipia gharama za umeme zilizowezesha kuunganishiwa nishati hiyo na
kuwataka viongozi wengine wa vijiji na vitongoji nchini kote kuiga mfano huo.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alitoa muda wa
siku saba kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, wilayani Iramba,
kuvuta nyaya na kuwaunganishia umeme wananchi katika kijiji cha Msingi.
Waziri alitoa agizo hilo baada ya kushuhudia nguzo
zilizosimikwa kwa muda mrefu pasipo kufungwa nyaya wakati akipita eneo hilo
akitokea Mkalama.
Alimtaka Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu ambaye alifuatana naye katika
ziara hiyo kumchukulia hatua Mkandarasi husika endapo hatatimiza agizo hilo.
Aidha, akiwa eneo la Kiomboi, Waziri alitoa siku tano
kwa Mkandarasi husika kuhakikisha anaondoa nguzo za umeme zilizorundikwa chini
na kuzitumia kuwaunganishia umeme wananchi wa eneo hilo.
Akiwa ameoneshwa kukerwa na hali hiyo ya nguzo
kurundikwa wakati wananchi wa eneo husika hawana umeme, Waziri alimwagiza
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Singida, Abdulahaman
Nyeye kumchukulia hatua Meneja wa Shirika hilo wilayani Iramba, endapo
atashindwa kusimamia utekelezaji wa agizo lake.
Pia, alimwagiza Mkuu wa Wilaya husika kumchukulia
hatua za kisheria Mkandarasi husika endapo hatatekeleza agizo lake ikiwa ni
pamoja na kumweka ndani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi
Jackson Masaka, aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa
kutekeleza kikamilifu ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo upelekaji umeme vijijini.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Allan Kiula, alimpongeza
Waziri wa Nishati na Naibu wake Subira Mgalu kwa kazi nzuri ya kusimamia
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Vilevile, alimwomba Waziri Kalemani kufikisha salamu
za shukrani kwa Rais Magufuli kutokana na upendeleo ambao amekuwa akiwapatia
katika kuwapelekea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo umeme.
Hadi sasa jumla ya vijiji 57 vya Wilaya ya Mkalama
kati ya 70 vilivyopo, vimekwishafikishiwa nishati ya umeme. Waziri Kalemani
ameeleza kuwa hadi kufikia Juni 2021, vijiji vyote vitakuwa vimekwishapelekewa
umeme.
Waziri Kalemani ameendelea kusisitiza kuwa katika
kipindi hiki ambacho Taifa linakabiliana na ugonjwa wa Corona, ziara zake
kukagua miradi katika maeneo mbalimbali hazitahusisha wananchi ili kuepuka
mikusanyiko. Badala yake, ziara zitahusisha viongozi wachache wa vijiji na
vitongoji katika maeneo husika.
Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani akiwasha umeme kwenye Zahanati ya kijiji cha Mkalama, wilayani
Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020 huku akishuhudiwa na viongozi
wachache ikiwa ni hatua ya kuepuka mikusanyiko ya wananchi ili kujikinga na
ugonjwa wa Corona.
Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani (wa pili kulia) na Ujumbe wake, wakiangalia nguzo za umeme zilizorundikwa
chini akiwa katika ziara ya kazi eneo la Kiomboi, Singida, Aprili 19 mwaka huu.
Waziri aliagiza kuondolewa kwa nguzo hizo mara moja, zisimikwe na
kuwaunganishia umeme wananchi wa eneo hilo
Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani (mbele-kulia) akiwa amefuatana na viongozi na watendaji
mbalimbali wa Serikali wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini
wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika
Zahanati ya Kijiji cha Milade, Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida, Aprili 19
mwaka huu. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson
Masaka na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Mkalama, Allan Kiula.
Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani (kushoto), akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumsimamia Mkandarasi
anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani Iramba, kufunga nyaya za umeme
katika nguzo alizosimika katika Kijiji cha Msingi na kuwaunganishia umeme
wananchi ndani ya siku saba. Alitoa agizo hilo Aprili 19 mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya
Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka (kulia) akitoa salamu za ukaribisho kwa Waziri
wa Nishati Dkt Medard Kalemani (anayesaini kitabu), baada ya Waziri kuwasili
wilayani humo kwa ajili ya ziara ya kazi, Aprili 19 mwaka huu. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Mkalama, Allan Kiula.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza
kushoto), akisalimiana na viongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama,
alipowasili wilayani humo Aprili 19, 2020 kwa ziara ya kazi kukagua utekelezaji
wa miradi ya umeme.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati),
akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala
wa Nishati Vijijini (REA), alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Mkalama,
Mkoa wa Singida, Aprili 19, 2020. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Mkalama, Allan
Kiula na wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhandisi Jackson Masaka.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mbele) na
Ujumbe wake, wakiwa katika ziara ya kazi wilayani Mkalama, Mkoa wa Singida,
Aprili 19 mwaka huu. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi
Jackson Masaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...