Picha ikionesha sanamu ya Ng'ombe anayezalishwa na Taasisi ya Mifugo TALIRI-Mpwapwa.
 Mtafiti kiongozi Kabuni Thomas Kabuni- akionesha waandishi wa habari namna wanavyovuna mbegu kutoka kwa Ng'ombe Jike.

 Mkuu wa Taasisi ya Mifugo TALIRI-Mpwapwa Dkt Eliakunda Kimbi akionesha picha ya tafiti zinazofanyika kituoni kwake.
Mtafiti kiongozi Kabuni Thomas Kabuni- akieleza waandishi wa habari hatua wanazozipitia katika kuzalisha viini tete.
Na COSTECH

TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) yaiwezesha taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Mpwapwa kuzalisha ng’ombe kwa kutumia Teknolojia ya urutubishaji na upandikizaji wa viinitete

Taarifa za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonyesha kuwa Tanzania ni Nchi ya tatu barani Afrika kwa wingi wa mifugo hasa ng’ombe ikifuatia Nchi za Ethiopia na Sudan (kabla haijagawanyika). Hata hivyo asilimia tisini na nane (98%) ya ng’ombe wanaofugwa Tanzania ni wa kienyeji ambao hawana nyama nyingi na hawazalishi maziwa kwa wingi.

Tathimini ya sekta ya mifugo inaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na upungufu wa nyama nyekundu kiasi cha tani 1,731,000 sawa na upungufu wa asilimia thelathini na tatu (33%) ya mahitaji.

 Upungufu huu utachangiwa zaidi na changamoto za ubora hafifu wa mifugo, hasa ng’ombe wanaofungwa Tanzania ikiwa pamoja na makadirio ya kuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya watu hasa watakao hamia mijini ifikapo mwaka 2030.  Hizi ni changamoto zinazokabili sekta ya mifugo nchini na ni wajibu wa kila mdau wa maendeleo kufikiri namna bora ya kutatua changamoto hizo.

Kwa sasa Serikali ya Tanzania inahamasisha uchumi wa viwanda unaolenga kwenye ujenzi wa viwanda  vitakavyo tumia malighafi za ndani. Viwanda hivyo vinahitaji uwepo endelevu wa malighafi kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbali mbali. 

Kutokana na changamoto zilizo orodheshwa hapo juu kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha Sekta ya mifugo ili kufanikisha upatikanaji endelevu wa malighafi za mifugo na kusaidia Nchi kufikia azma yake ya kuwa na uchumi wa kati unao ongozwa na sekta ya viwanda. 

Kwa kulitambua hilo, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) Mpwapwa inatekeleza mradi wa kuzaliza ng’ombe wenye tija kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa malighafi zitokanazo na mazao ya mifugo mfano, maziwa, nyama na ngozi.

Katika kuhakikisha kuwa kuna ng’ombe wa kisasa na wa kutosha, TALIRI kupitia mradi unaofadhiliwa na COSTECH imetafuta njia bora ya uzalishaji wa ng’ombe wenye tija. Njia hii inatumia teknolojia ya uvunaji wa mbegu za fahari au ng’ombe dume. 

Katika kila mshindo mmoja wa fahari dume hupatikana  zaidi ya mbegu 500. Mbegu hizi huvunwa na kupandikizwa kwa ng’ombe jike waliopo kwenye joto. Ng’ombe wanaozalishwa kwa njia hii wanatoa maziwa kwa wingi na wana nyama ya nyingi. 

Teknolojia hii hujulikana kitaalamu kama uhaulishaji au “artificial insemination”. Njia hii ni mbadala wa uzalishaji wa ng’ombe kwa njia ya asili inayotegemea ng’ombe jike mwenye joto kupandwa na ng’ombe dume ambaye hutumia mbegu zaidi ya 500 katika kuzalisha ndama mmoja. Kitaalamu mbegu moja tu kutoka kwenye ng’ombe dume huhitajika kuzalisha ndama mmoja. Hivyo kuzalisha ng’ombe kwa njia ya asili husababisha upotevu mkubwa wa mbegu kutoka kwa ng’ombe dume zinazotumika katika kuzalisha ndama mmoja.

Habari njema ni kwamba, kwa teknolojia ya uvunaji wa mbegu kutoka kwa ng’ombe dume na upandikizaji wa mayai yaliyorutubishwa kwa ng’ombe jike  kwa sasa unafanyika hapa Tanzania. Hii itasaidia kuongeza uzalishaji wa ng’ombe Nchini. Badala ya kupata mimba itakayotoa ndama mmoja huku mayai mengine yakiharibika katika kila mzunguko wa joto, ndama wengi zaidi wanaweza kupatikana kwa njia ya uvunaji na upandikizaji wa mayai.

Mkuu wa TALIRI Mpwapwa, Dk Eliakunda Kimbi anasema tangu mwaka 2011 wanafanya utafiti huo kwa ufadhili wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuwezesha upatikanaji wa mayai hayo yaliyorutubishwa ambayo huitwa viinitete.

“Mwanzo tulikuwa tunachukua viinitete kutoka Afrika Kusini, lakini kwa kutumia ufadhili kutoka COSTECH tumeweza kutengeneza teknolojia ambayo kwa kutumia ng’ombe wetu, tuna vuna na kupandikiza viini tete kwenye ngombe jike wenye joto na kuweza kuzalisha ng’ombe wengi kwa pamoja. Teknolojia hii kwa sasa inafanya kazi na tunajipanga kuipeleka kwa wananchi na wadau mbali mbali wa maendeleo kwa ajili ya matumizi,” anasema Dk. Kimbi.

Namna ya uvunaji na upandikizaji wa viinitete
Kutoka katika kila jike lenye joto, wataalamu hupandikiza mbegu zilizovunwa kutoka kwenye ng’ombe dume ili kupata kiumbe kamili (kiinitete) ambacho kinaweza kukuzwa kama mimba na jike lenye afya litakalo chaguliwa kumzaa ndama mtarajiwa.

 Mtafiti mkuu wa TALIRI Mpwapwa na mratibu mkuu wa mradi huo, Dk Kabuni Thomas Kabuni anasema kinachofanyika ni kuandaa jike lenye afya nzuri litakalotoa mayai mazuri na fahari mwenye sifa hizo kwa ajili ya mbegu.

Ng’ombe wazazi (wale wanaotoa mayai), anasema huchomwa sindano ya kuchochea homoni inayopevusha mayai mengi kwa wakati mmoja. Sindano hizi huchomwa kwa siku nne mfululizo. Baada ya hapo ng’ombe wazazi huachwa kwa saa 72 kisha mayai hurutubishwa kwa kupandikizwa mbegu ya kiume kupata viinitete. Viinitete hivyo hupandikizwa kwa ng’ombe jike ambao hawajatumika kwenye zoezi la kutoa mayai.

Ng’ombe jike wanaopandikizwa viinitete huandaliwa kabla ya kupandikizwa kiinitete, hii ni kuhakikisha kila jike linalobeba kiinitete lina afya njema na sifa nyingine muhimu, anasema Dk Kabuni.

Kuanzia sindano ya kuchochea homoni mpaka kupandikizwa mbegu ya kiume kwa ng’ombe wazazi, huchukua siku saba na husubiriwa kwa wiki moja nyingine kabla ya kuvuna viinitete. “Jike moja la ng’ombe hutoa wastani wa viinitete vinne mpaka sita ingawa wapo majike wengine hutoa viinitete kati ya 8 mpaka 12. Kwa kawaida bila kujali aina ya ng’ombe, jike moja anaweza kupandikizwa mbegu za ng’ombe dume mara nne kwa mwaka na kutoa viinitete zaidi ya 50,” anasema Dk. Kabuni.

Baada ya kuvunwa, viinitete hutakiwa kuhifadhiwa kwenye kimiminika baridi (liquid nitrogen) kinachokuwa kimepozwa mpaka nyuzi joto hasi 196 ambayo ni chini zaidi ya barafu iliyoganda zaidi. Katika kimiminika hicho, viinitete vinaweza kusafirishwa kwenda shambani kwa mfugaji vikiwa salama na vyenye ubora unaohitajika. Usafirishaji hufanywa kwa kuvihifadhi kwenye mitungi maalumu. “Kwa sasa tunaweza kusafirisha viinitete kwa masaa 36 na viinitete vikawa salama kabisa. Kifaa cha kusafilishia viinitete kilichopo kinatumia betri,” anasema Dk. Kabuni.

Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Kimbi anasema teknolojia ya viinitete itasaidia malengo ya Serikali kuzalisha ng’ombe bora milioni moja kwa mwaka ingawa kuna changamoto kadhaa zinatakiwa kushughulikiwa. 

“Tunahitaji watafiti wa kutosha watakao endeleza teknolojia hizi na kubuni nyingine zitakazoongeza tija.  Ili kuwa na mifugo bora itakayotoa malighafi viwandani na kukuza pato la mfugaji kunahitaji kuwekeza katika utafiti,” anasema. Taasisi hiyo ya TALIRI inayohitaji watumishi 150 ili ijiendeshe kwa ufanisi unaohitajika kwa sasa inao 48 tu ambao kati yao kuna watafiti 18.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu anaamini mradi wa viinitete ni wa kipaumbele utakaosaidia kuboresha sekta ya mifugo nchini na kusaidia nchi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.

Kufanikisha mradi wa viinitete, COSTECH imetoa fedha za kukarabati maabara ya utafiti na kuweka vifaa vyote muhimu vinavyohitajika pamoja na kununua mtambo wa kuzalisha kimiminika baridi cha kutunzia viinitete.

 TALIRI Mpwapwa ni miongoni mwa taasisi za utafiti wa kisayansi zilizonufaika na ruzuku ya Serikali kuimarisha miundombinu hivyo kuwapa watafiti nafasi ya kutatua changamoto zilizopo nchini kuelekea uzalishaji mali wa kisasa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...