Mbunifu Julius Mwangwa akizungumza na waandishi wa habari.

Mwandishi Wetu, COSTECH
MBUNIFU Julius Mwangwa, mkazi wa wilaya ya Ilemela jijini Mwanza amebuni mtambo wa kufua umeme kwa kutumia mgandamizo wa hewa ikiwa ni miongoni mwa bunifu zitakazochangia katika sekta ya nishati ya umeme nchini.


Teknolojia inayotumika kwenye mtambo huo ni hewa inayoingizwa kwenye matenki kisha inazungushwa na kutoa nishati inayozalisha umeme unaoweza kutumika maeneo tofauti.

“Mwaka 2011 nilitengeneza prototype (mtambo wa mfano) ambayo niliipeleka kwa Mkuu wa Mkoa ambaye aliipenda na akawaita wataalamu wake waikague,” anasema mbunifu huyo.

Watalaamu kutoka Wakala wa ufundi Umeme (TAMESA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mhandisi wa Mkoa waliukagua mtambo na kuona ubunifu huo una manufaa hivyo wakamuunganisha na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo hakuwa anaifahamu kabla.

Wakati huo, wataalam hao walioitwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro walikadiria mtambo huo ungehitaji Shilingi milioni 70 kuukamilika. Hata baada ya uhamisho wa Kandoro na nafasi yake kuchukuliwa na Evarist Ndikiro (Mkuu wa mkoa wa kipindi hicho) bado aliendelea kuungwa mkono kwa kufanya mawasiliano yaliyokuwa yanaratibiwa na ofisi Mkuu wa Mkoa, Ndikiro alimpeleka moja kwa moja COSTECH.

Baada ya muda akapata barua kutoka COSTECH kupitia kwa ofisi ya Mkuu wa mkoa ikimualika kufika ofisini kwao jijini Dar es Salaam. Baada ya Tume kukagua wazo lake, anasema walimuunganisha na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine ambao walilikagua wazo lake na kutoa ripoti. “Wataalamu hawa waliandaa ripoti iliyopelekwa COSTECH kwamba wazo langu ni zuri na lina uwezo wa kuleta manufaa makubwa kwa jamii,” anasema Mwangwa.

Kwa majibu hayo, akaona anapaswa kuongeza nguvu kutekeleza ubunifu wake hivyo akawa anatumia akiba yake ndogo kufanya vitu vichache vinavyowezekana, alijitahidi kwa uwezo wake lakini kwa kuwa ubunifu huo unahitaji fedha nyingi kuliko uwezo wake mambo hayakuwa rahisi.

Kutokana na hali hiyo, anasema COSTECH walikubali kumpatia ruzuku ili kuhakikisha mambo yanafanywa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika. Mbunifu anasema wataalamu wa Chuo Kikuu walimsaidia kutengeneza bajeti inayoainisha mahitaji ya msingi kwa ajili ya mradi huo.

Tathmini iliyofanywa, anasema ilionyesha fedha inayohitajika ni kubwa kuliko ruzuku inayotolewa na COSTECH lakini ikaahidi kumsaidia ili wazo lake lisife.

“COSTECH walinipa Sh10 milioni ambazo zinatosha kununua vifaa vichache vya mtambo huu. Nina imani wakinipa awamu ya pili itasaidia kuukamilisha na kuanza kuzalisha kati ya kilowati 50 mpaka 60 ila utakapokamilika utatoa kilowati 100 zinazotosha kuwasha wastani wa nyumba 50,”anasema.

Akieleza mwanzo wa wazo lake la ubunifu, alikuwa ana nia ya kuzalisha umeme na kuziunganisha nyumba zilizo nje ya mfumo wa gridi ya Taifa na ikiwezekana aingie mkataba na Tanesco kumsaidia kuusambaza na kukusanya mapato kutoka kwa wateja. Mtambo alioupeleka kwa Mkuu wa Mkoa ulikuwa unazalisha wati 60 zilizowashawishi wataalamu kwamba una manufaa kwa jamii iwapo kutakuwa na uwekezaji unaohitajika.

Ushauri kwa wabunifu
Akiwa ameboresha mtambo wake kwa kiasi, anashauri kwa kuwa COSTECH ndio wenye dhamana ya kuendeleza ubunifu, waendelee kuwafikia wenye vipaji na kuwawezesha hata kama wapo vijijini.

Kwa kuanza na kiasi kidogo cha fedha, anasema utafika wakati COSTECH itaweza kutoa kiasi kikubwa zaidi ili kufanikisha miradi mikubwa zaidi ya kibunifu na Tanzania kuanza kuzalisha bidhaa zake badala ya kutegemea kuagiza kutoka nje.

Katika jitihada za kufanikisha hayo yote, anasema, elimu itolewe ili wabunifu waliopo vijijini ambao hawajui namna ya kuwafikia COSTECH kupata uelewa wa pamoja na kuwasilisha bunifu zao ili wasaidiwe.

“Kupitia COSTECH, mbunifu anaweza kuunganishwa na wataalamu wa eneo analolifanyia kazi hivyo kuongezewa maarifa ambayo akiwa peke yake hawezi kuyapata,” anasema.

Serikali,
Kuanzia mwaka jana (2019), Serikali ilianzisha mkakati wa kuwatambua wabunifu kisha ikazindua mashindano ya kitaifa kwa ajili yao yajulikanayo kama MAKISATU.

Mwangwa anasema Serikali inastahili pongezi kwa hatua hiyo muhimu ya kuwatambua na kuwawezesha wabunifu kwani suala linalotia moyo ni kuona zipo mamlaka zinazosaidia kufanikisha malengo ya kila mbunifu.

“Kwa wabunifu waliopo vijijini na hawana mtu wa kuwashika mkono, nashauri waende ofisi za Serikali kupeleka ubunifu wao kwani upo utaratibu wa kuwaunganisha na mamlaka za kuwaendeleza ili waihudumie jamii inayowazunguka,” anasema Mwangwa.

Vilevile, anashauri wabunifu wahudhurie makongamano ya wabunifu yanayofanyika sehemu tofauti nchini yakiratibiwa na mamlaka tofauti.

Hata hivyo, anasema ufadhili kwa bunifu sio lazima utolewe na Serikali pekee bali kuna njia nyingi tofauti pamoja na watu wenye uwezo wa kuwezesha wabunifu wenye mawazo mazuri yanayotekelezeka.

“Ubunifu ni muhimu katika kuinua uchumi lakini wabunifu wengi hawana mtaji kufanya uzalishaji mkubwa hivyo benki na taasisi nyingine za fedha ziangalie namna ya kuwakopesha ili wazipeleke bidhaa zao sokoni,” anashauri Mwangwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...