Na Farida Ramadhani na Josephine Majura

KAMPUNI ya Barrick imeilipa Tanzania dola milioni 100, sawa na takriban sh. bilioni 250, ikiwa ni sehemu ya malipo ya dola milioni 300 ambazo Kampuni hiyo ya Madini ilikubali kulipa kama fidia ya kodi.

Mfano wa Hundi ya kiasi hicho cha fedha imekabidhiwa na Meneja Mkazi wa Kampuni ya Barrick, Bw. Hilaire Diarra kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, kwa niaba ya Serikali, Jijini Dodoma leo Mei 26, 2020.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano na Barrick ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na Kamati yake, Dkt. Mpango alisema tukio hilo ni mwanzo wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 19, 2019 na kusainiwa rasmi Januari 24, 2020.

Dkt. Mpango aliyataja makubaliano mengine yaliyofikiwa kati ya Serikali na kampuni hiyo kuwa ni kuundwa kwa Shirika la Madini la Twiga lenye umiliki wa pamoja likalofanya kazi nchini katika kusimamia uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara pamoja na migodi mingine nchini ambapo Serikali ya Tanzania itashiriki katika utoaji wa maamuzi kuhusu uendeshaji wa migodi, mipango, manunuzi pamoja na masoko ya madini.

“Tulikubaliana kuhakikisha kuwa faida za kiuchumi zinazotokana na migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi pamoja na North Mara zigawanywe kwa msingi wa usawa wa asilimia 50 kwa 50 kati ya washirikania ambapo hisa za Serikali zinazotokana na faida za kiuchumi zitatolewa katika mfumo wa mrabaha, kodi pamoja na kupata asilimia 16 ya faida kutokana na makampuni hayo kufanya kazi nchini” alisema Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alisema mbali na makubaliano hayo, kampuni ya Barrick imekubali kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mtambo wa kuchakata madini nchini (smelter).

“Kampuni ya Barrick pia imekubali kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuahidi kutoa hadi dola milioni 10 kwa kipindi cha miaka kumi kwa ajili ya utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini”, aliongeza Dkt. Mpango.

Alisema Kampuni ya Barrick ilikubali kutoa dola 6 kwa kila ounce ya madini itakayouzwa (ikijumuisha mchango kwenye Mfuko wa Mandeleo ulioanzishwa na Kampuni ya Barrick Tanzania) ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi pamoja na kutoa kiasi cha dola milioni 40 kwa ajili ya kuboresha kipande cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na miundombinu yake.

“Naipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanza kutekeleza makubaliano haya na natoa wito kwa kampuni nyingine za madini na wawekezaji wengine katika sekta hiyo kuiga mfano mzuri uliooneshwa na Kampuni hii katika kuhakikisha kunakuwa na hali ya usawa katika uendeshaji wa shughuli za madini nchini kwa faida ya pande zote mbili” alisisitiza Dkt. Mpango.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto James alisema kuwa fedha hizo tayari zimeshapokelewa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Dennis Mark Bristow ambaye alikuwa akifuatilia makabidhiano hayo kwa njia ya mtandao na kutoa hotuba yake akiwa nchini Afrika Kusini alimpongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Timu yake kwa kufanikisha majadiliano yaliyosaidia kuanzishwa kwa ushirikiano wa dhati kati ya Kampuni yake na Serikali.

Alisema kuwa wataendeleza ushirikiano wao na Tanzania na kwamba wanaamini kuwa ushirikano huo utakuwa wa mfano si tu kwa Afrika bali utakuwa ni ushirikiano wa mfano kwa Dunia nzima.

Aliahidi kuendelea kuboresha miundombinu ya maeneo ya migodi wanayomiliki nchini na kueleza kuwa wanajiolojia wanafanyakazi kwa bidii ili kuirudisha hadhi ya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha uzalishaji dhahabu duniani.

 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kulia) akipokea sehemu ya malipo ya dola milioni 100 (Sh. bilioni 250) kutoka  Kampuni ya Madini ya Barrick ikiwa ni makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 2019. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Palamagamba Kabudi. Wa tatu ni Naibu waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo, akifuatiwa na Bw. Hilaire Diarra Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Barrick na Bw. Luiz Correia Meneja Mkuu Mgodi wa North Mara, Jijini Dodoma.

 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza jijini Dodoma na vyombo vya habari wakati wa hafla ya kupokea sehemu ya malipo ya fidia ya Sh. bilioni 250 kutoka  Kampuni ya Madini ya Barick,  jijini Dodoma, leo Mei 26, 2020.


 Bw. Hilaire Diarra Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Barrick (Kulia) na Bw. Luiz Correia Meneja Mkuu Mgodi wa North Mara, wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayumo pichani) alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali na vyombo vya Habari baada ya kupokea sehemu ya malipo ya dola milioni 100 (Sh. bilioni 250) kutoka Kampuni ya Madini ya Barick, Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James kulia na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayumo pichani) alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali na vyombo vya habari baada ya kupokea sehemu ya malipo ya Sh. bilioni 250 kutoka  kampuni ya madini ya Barick, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Palamagamba Kabudi na viongozi mbalimbali wakimsikiliza Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Dkt. Denis Mark Bristow aliyekuwa akifuatilia hafla ya makabidhiano ya mfano wa hundi ya dola milioni 100 kati ya Kampuni hiyo na Serikali, kwa njia ya mtandao akiwa nchini Afrika Kusini, tukio hilo limefanyika katika ukumbi wa Kambaraje wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.(Picha na Saidina Msangi-Wizara ya Fedha na Mipango).



Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Dkt. Dennis Mark Bristow (kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu, Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati wa Kampuni ya Barrick Dkt. Willem Jacobs, wakishiriki na kufuatilia tukio hilo kutoka nchini Afrika ya Kusini kwa njia ya mtandao wakati Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wa pili kushoto, akipokea hundi kifani ya dola milioni 100 kwa niaba ya Serikali kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Barrick Bw. Hilaire Diarra (wa pili kushoto), Jijini Dodoma Tarehe 26 Mei, 2020, ikiwa ni sehemu ya malipo ya dola milioni 300 ambazo Kampuni hiyo ilikubali kuilipa Serikali kumaliza mzozo uliokuwepo kati ya Serikali na Kampuni hiyo hatua iliyosababisha kuanzishwa pia kwa Kampuni ya Ubia ya Madini ya Twiga kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano na Barrick Prof. Palamagamba Kabudi na wa tatu kulia na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) na kushoto ni Meneja wa Mgodi wa North Mara Bw. Luiz Correia



======== ======= ======= ==========

HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO DKT. PHILIP I MPANGO (MB), KWENYE HAFLA YA KUPOKEA SEHEMU YA MALIPO YA FIDIA, DODOMA, 26 MEI 2020


Mheshimiwa Prof. Palamagamba J.A.M. Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali;

Mhe. Prof Adelardus Kirangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali;

Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji(Mb) – Naibu Waziri Wizara ya Fedha na Mipango;

Mhe. Stanslaus Nyongo(Mb) – Naibu Waziri, Madini,

Mhe. Prof. Florens D.A.M. Luoga, Gavana wa Benki Kuu na Makamu Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano;

Bw. Doto James- Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango

Prof. Simon Msanjila- Katibu Mkuu Wizara ya Madini

Mwakilishi wa Msajili wa Hazina;

Dkt Dennis Mark Bristow, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick;

Dkt Willem Jacobs, Afisa Mtendaji Mkuu, Kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati ya Kampuni ya Barrick;

Bw. Hilaire Diarra, Mwakilishi Mkazi – Barrick

Bw. Luiz Correia, Meneja Mkuu – North Mara

Wajumbe wa Timu ya Majadiliano ya Serikali;

Wawakilishi wa Serikali ya Tanzania;

Wawakilishi wa Vyombo vya Habari;

 
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,


Habarini za Mchana,




1. Utangulizi

Tukio hili la leo ni mwanzo wa safari muhimu katika utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya serikali ya Tanzania na ya Barrick yaliyofikiwa tarehe 19 Disemba 2019 na kusainiwa rasmi tarehe 24 Januari 2020 jijini Dar es Salaam.

Masuala muhimu yaliyokubalika na kila upande ni:

(i) Kuunda Shirika la Madini la madini la Twiga lenye umiliki wa pamoja litakayofanya kazi nchini katika kusimamia uendeshaji wa migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara pamoja na migodi mingine nchin ambapo serikali ya Tanzania itashiriki katika utoaji wa maamuzi kuhusu uendeshaji wa migodi, mipango, manunuzi pamoja na masoko ya madini. Shirika la madini la Twiga lilizinduliwa rasmi 20, octoba 2019.

(ii) Nia ya Kampuni ya Barrick ni kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika maeneo ya uchambuzi yakinifu juu ya jinsi nchi inavyonufaika na maendeleo ya uchakataji wa madini (Smelter facility)

(iii) Faida za kiuchumi zitokanazo na migodi ya Bulyanhulu, Buzwagi pamoja na North Mara zigawanywe kwa msingi wa usawa kati ya washirika yaan 50/50 ambapo hisa za Serikali zinazotokana na faida za kiuchumi zitatolewa katika mfumo wa mrahaba, kodi pamoja na kupata asilimia 16 ya faida kutokana na makampuni hayo kufanya kazi nchini.

(iv) Barrick kulipa dola milioni 300 za kimarekani kwa Serikali ya Tanzania kama malipo ya Patano kuhusu fidia ya kodi kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.

(v) Serikali ya Tanzania kuruhusu usafirishaji wa Makinikia nje ya nchi.


2. Chimbuko:

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana

Utakumbuka kuwa Tanzania ilipitisha sheria muhimu tatu mwezi Julai 2017 ambazo zilitoa muelekeo wa sekta ya madini, sheria hizo ni:

(1) Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya Mwaka 2017 (Sheria ya Madini Sura ya 123);

(2) Sheria ya Umiliki wa Maliasili na Rasilimali ya Mwaka 2017; na

(3) Sheria ya Mapitio ya Masharti Hati katika Mikataba ya Maliasili na Rasilimali ya Mwaka 2017.

Kufuatia mabadiliko katika sekta ya madini, majadiliano kati ya GNT na kampuni ya Barrik yalianza jijini Dar Es Salaam tarehe 31 Julai 2017. Kufuatia hoja za msingi za Serikali, majadiliano yalifanyika kupitia jitihada za utekelezaji wa azimio la Profesa John Thornton’s wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa washikadau kwamba:

“Kanuni za msingi za BGC’s zinatokana na uelewa na jitihada za pamoja katika karne ya 21 kama jambo la msingi katika kujenga ushirikiano wa kina na kuaminiana na Serikali wenyeji, jamii , Mashirika yasiyo ya kiserikali, wazawa pamoja na wadau wengine. Kutokana na kuhusishwa kwa watu hao muhimu, tunaruhusiwa kuchukua madini yao nje ya wigo wa utawala wao na hivyo kuwezesha utajiri kwa wote’

Baada ya miaka miwili ya majadiliano, tarehe 24 Januari 2020, mikataba na nyaraka zifuatazo ziliwekwa saini.

Rasimu ya Mkataba wa Makubaliano ya Msingi (Framework Agreement);

(i) Mkataba ya Uchimbaji Madini kwa mgodi wa Bulyanhulu uliorekebishwa (Mining Development Agreement);

(ii) Mkataba ya Uchimbaji Madini kwa mgodi wa North Mara uliorekebishwa;

(iii) Mkataba ya Uchimbaji Madini kwa mgodi wa Buzwagi uliorekebishwa;

(iv) Mkataba wa Wanahisa katika Kampuni ya Ubia baina ya Serikali na Barrick (Shareholders Agreement);

(v) Mkataba wa Wanahisa katika Kampuni ya North Mara, ikiwemo Serikali;

(vi) Mkataba wa Wanahisa katika Kampuni ya Bulyanhulu, ikiwemo Serikali;

(vii) Mkataba wa Wanahisa katika Kampuni ya Buzwagi, ikiwemo Serikali;

(viii) Mkataba wa Menejimenti na Huduma za Uendeshaji wa makampuni tanzu;

(ix) Katiba ya Kampuni ya Ubia baina ya Serikali na Barrick (Memorandum and Articles of Association);

(x) Katiba ya Kampuni Tanzu ya Bulyanhulu iliyorekebishwa;

(xi) Katiba ya Kampuni tanzu ya North Mara iliyorekebishwa; na

(xii) Katiba ya Kampuni tanzu ya Buzwagi iliyorekebishwa.



3: Kuhusu Kanuni ya 50/50


Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick zimekubaliana kwamba pande mbili zitashirikiana katika msingi wa mambo yote yanayohusisha faida za kiuchumi zinazotokana na madini ya Tanzania katika msingi wa 50/50 kwa kuzingatia mipango ya uwepo wa madini inayoendana na kanuni ya usawa wa kiuchumi kama ilivyoelezwa na sheria. Itakumbukwa kwamba malipo ya dola za kimarekani milioni 300 ni nje ya kanuni ya 50/50.

4.0. Kuhusu Malipo ya mwanzo ya Dola za Kimarekani milioni 100


Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana

Hundi ya Dola za Kimarekani milioni 100 inayotolewa leo ambayo ni sawa na kiasi cha Shilingi bilioni 250 ni sehemu ya malipo ya awali ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 300 sawa na kiasi cha shilingi bilioni 750. Pande husika zimekubaliana mpango wa malipo wa bakaa ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 200.

Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Kampuni ya Barrick kwa kuonesha dhamira ya dhati ya ushirikiano mzuri kwenye muelekeo mpya wa sekta ya madini Tanzania ambao umekubalika na pande zote kwa manufaa ya pande zote husika.


5. Ahadi za Kiuchumi na Kijamii zilizotolewa

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Mbali ya makubaliano hayo, Kampuni ya Barrick imekubali kufanya yafuatayo:

(i) Kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mtambo wa kuchaka madini nchini (Smelter);

(ii) Kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutoa hadi dola za marekani milioni 10 kwa kipindi cha miaka kumi kwa ajili ya utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini;

(iii) Kutoa hadi dola za marekani 6 kwa kila ounce ya madini itakayouzwa (ikijumuisha mchango kwenye Mfuko wa Maendeleo ulioanzishwa na Kampuni ya Barrick Tanzania) ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi;

(iv) Kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 40 kwa ajili ya kuboresha kipande cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na  miundombinu yake;

6. HITIMISHO:

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Tunatumaini kwamba, pande zote mbili zinazohusika katika makubaliano zitaheshimu makubaliano na kuhakikisha yanatekekelezwa. Nawahakikishia kwamba, kwa upande wa Serikali ya Tanzania imedhamiria kwa dhati kutekeleza makubaliano hayo. Na kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni Serikali imeruhusu makontena na makinikia ya madini 277.

Tukio la leo ni hatua muhimu katika Sekta ya madini nchini ikizingatiwa kuwa Kampuni ya Barrick ni mdaiu muhimu katika Sekta hii. Nawaomba Kampuni nyingine za madini na wawekezaji wengine katika Sekta hii kufuasta mfano mzuri uliooneshwa na Kampuni ya Barrick katika kuhakisha kunakuwa na hali ya usawa (win- win Situtuation) katika uendeshaji wa shughuli za madini.

Napenda kuhitimisha kwa kutangaza kwamba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania imedhamiria kwa dhati kuwa ushirikiano wenye usawa katika Sekta ya madini utasaidia kuleta fedha ambazo zitasaidia katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Ahsanteni kwa Kunisikiliza

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...