Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa maelekezo kwa watendaji juu ya namna rahisi ya
kuwashirikisha wadau ili kuweza kufanikiwa kampeni ya ugawaji wa
vyandaru kwa kaya.

Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya kampeni ya uhamasishaji wa ugawaji wa vyandandarua katika kaya yaliyofanya na wawakilishi wa Wizara ya Afya mkoani Rukwa. 

Shekhe wa Mkoa wa Rukwa Shekh
Rashid Akilimali (katikati) akisikiliza kwa makini mafunzo ya kampeni ya
uhamasishaji wa ugawaji wa vyandandarua katika kaya yaliyofanya na
wawakilishi wa Wizara ya Afya mkoani Rukwa.
**********************************
Katika hatua
kukabiliana na mbu waenezao ugonjwa wa Malaria nchini, Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii jinsia, Wazee na Watoto kwa
ushirikiano na Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) imeendelea kutekeleza kampeni mbalimbali za kudhibiti Malaria
ikiwa ni miongoni mwa hatua za kutokomeza ugonjwa huo hadi kufikia
mwaka 2030.
Mwakilishi kutoka
Wizara ya Afya Peter Gitanya amesema kuwa Kampeni hiyo ambayo imelenga
kugawa vyandarua 719,254 kwa mkoa wa Rukwa ni muendelezo wa kampeni
kubwa tatu za uhamasishaji wa ugawaji wa vyandarua kwa kaya zilizowahi
kufanyika miaka ya 2009, 2010 na 2015/2016 na kuongeza kuwa Bohari ya
Dawa (MSD) itahusika na usafirishaji wa vyandarua kutoka maghala yao
katika kila mkoa hadi kituo cha ugawaji katika Kijiji ama mtaa husika.
“Halmashauri
ambako kampeni itafanyika ni zile halmashauri ambazo zina kiwango cha
chini cha umiliki wa vyandarua, chini ya 40%, na pia maambukizi ya
malaria yapo katika kiwango cha juu na cha kati, Halmashauri zenye
kiwango cha chini cha uwepo wa malaria zilizozungukwa na halmashauri
zenye kiwango cha juu na cha kati cha uwepo wa malaria na halmashauri
ambazo mpango wa ugawaji wa vyandarua kupitia wanafunzi shuleni
haufanyiki,” Alisisitiza.
Katika kusisitiza
hilo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wahusika wote
wa kampeni hiyo kushirikiana kwa karibu katika kufikisha elimu
iliyosahihi kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya vyandarua na kuongeza
kuwa ili kufanikisha mpango wa serikali kufikia uchumi wa kati ifikapo
mwaka 2025 ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha tunapambana na maradhi
hayo ili kuwa na jamii yenye afya na yenye uwezo wa kuzalisha.
“Mimi nitoe wito
tu kwamba ili mpango huu uweze kufanikiwa, tunahitaji tushikamane,
tushirikiane kwa nguvu zote, kufikisha elimu iliyosahihi kwa wananchi,
vinginevyo tusipotoa elimu kwa nguvu zote na watu wakaelewa tunaweza
tukatwanga maji kwenye kinu, kwahiyo jambo kubwa liwe ni elimu, elimu
iwafikie wananchi kwa nguvu zote, kama tulivyoanza hapa kushirikishana
hivi, tuendelee kushusha kuwashirikisha wadau mbalimbali,” Alisema.
Aidha, aliishauri
wizara ya afya na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kuona namna ya
kufanya utafiti juu ya miti shamba inayotumika kufukuza mbu katika
baadhi ya maeneo vijijini ili wananchi waweze pia kutumia miti hiyo kwa
kuipanda maeneo ya nyumba zao na hatimae kuwafukuza mbu hao.
Kampeni hiyo
itagawa vyandarua 7,097,565 katika Halmashauri 50 kutoka katika mikoa 10
nchini ikiwa na lengo la kugawa vyandarua hivyo vyenye dawa kwa
walengwa kwa asilimia 100 na Kwa mkoa wa Rukwa kampeni hiyo itagawa
vyandaru katika halmashauri zote nne za mkoa kwa kuwatambua walengwa na
kuwahamasisha juu ya matumizi na utunzaji wa vyandarua hivyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...