Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
PIGO kubwa limeipata familia ya muziki wa dansi nchini Tanzania baada ya nguli kwenye muziki huo Mafumu Bila Bombenga kufariki dunia jana Mei 11 mwaka huu wa 2020.
Kifo cha mwanamuziki huyo nguli ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake wa kupuliza Saxaphone kimeacha majonzi na simanzi kubwa kwa wadau wa muziki huo nchini.
Enzi za uhai wake Mombenga amefanya kazi za muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi na hakika amejijengea heshima kubwa na pengo lake kwenye upulizaji wa Saxaphone litachukua muda mrefu kuzibwa.
Wakati tukiendelea kuombeleza kifo cha nguli huyo wa muziki, ni vema tukakumbusha historia yake kwa ufupi.
![]() |
Mafumu akiimba na bendi yake wakati wa uhai wake. |
Iko hivi Mombebga safari yake ya muziki inaanzia mwaka 1972 alipojiunga na bendi ya Morogoro Jazz, wakati huo akitokea jeshini Makutupola,.
Mwaka 1973 alijiunga na Western Jazz alioshiriki nao kupiga Saxophone, kwenye vibao kadhaa vya bendi hiyo, vikiwamo ‘Hakika’, ‘Kazi ni Kazi’ na ‘Sadaka’, kabla ya mwaka 1978 kutimkia Dar International.
Pamoja na kupuliza kiustadi Saxophone pamoja na kuimba kwenye nyimbo kemkemu, zikiwamo ‘Mayasa’ na ‘Zuena’, lakini pia Bombenga alishiriki kucharaza gitaa la Solo katika kibao ‘Vick’ ilipofika mwaka 1979 alibeba mabegi na kutua Vijana Jazz Band alikotunga kibao ‘Taabu’ na pia kushiriki kukiimba, huku kadhalika akipuliza Saxophone kwenye vibao kama ‘Chiku’ na ‘Matata Ndani ya Nyumba’.
Mombenga ilipofika mwaka 1980 alihamia Maquis ambapo alitesa kwa kupuliza Saxophone kwenye vibao viiingi, baadhi yake ni ‘Zoa’, ‘Sina Ndugu’, ‘Noel’ pamoja na ‘Maige’.
![]() |
Mafumu aliipenda sana kazi yake |
Historia yake kwenye muziki pia inaonesha African Beat ilianzishwa mwaka 1998, baada ya Mafumu Bilali Bombenga kujiengua kutoka katika bendi ya African Stars ambayo nayo ilianzishwa mnamo mwaka 1994 kwenye Hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam, huku yeye akiwa ndiye muanzilishi.
Bombenga anakumbukwa kwani wakati akiwa na African Stars ambayo hata jina lake alilibuni yeye, walitamba na vibao kama ‘Sakatu Sakatu’, ‘Mayanga’, ‘Maya’, ‘Afrika’ na ‘Dance Dance’.
Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi hilo la African Stars linalojulikana zaidi hivi sasa kama ‘Twanga Pepeta’, ni Bob Gady, Andy Swebe, Alfa Nyuki, Palmena Mahalu, Pamela pamoja na Kayumbu ‘Amigolas’.
Latina enzi za uhai wake katika moja ya maelezo yake aliwahi kueleza kuwa alikaa Maquis hadi mwaka 1984 ailipochomoka tena na kuhamia Bima Lee alikokutana na wakali kama Jerry Nashon ‘Dudumizi’, Shaaban Dede ‘Super Motisha’, ‘Joseph Mulenga ‘Spoiller.
Safari yake katika muziki inaonesha mwaka 1985 Bombenga alikuwa mwanzilishi wa bendi ya MK Group ‘Ngoma za Maghorofani’, kabla ya mwaka 1986 kuwa tena mmoja wa waanzilishi wa Tancut Almas ya Iringa.
Wakati mwaka 1987 alirejea tena MK Group ambapo nyimbo yake ya kwanza kupuliza Saxophone awamu hii ya pili ilikuwa ni ‘Utakuja Kuanguka Kwenye Matope’. Mwaka 1989, kaka yake Adam Kinguti alirudi nchini akitokea Sudan alipokuwa akifanyakazi kwenye ofisi za ubalozi, wakaanzisha Bicco Stars na yeye kushiriki kupuliza Saxophone kwenye vibao kadhaa kama vile; ‘Magret Mage’, ‘Wapangaji’ na Kisamvu’.
![]() |
Mafumu alikuwa ni mcheshi wakati wote |
Ilipofika mwaka 1991 alitoka Bicco akiwa na mpapasaji kinanda mahiri wa kike ambaye kwa sasa ni marehemu, Asia Daruweshi, baada ya kutokea hali ya kutoelewana kati yake na Kinguti, wakaanzisha Zanzibar Sound.
Aliwahi kueleza huko nyuma kwamba wakiwa na Zanzibar Sound, walipata mkataba katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha na mwaka mmoja baadaye mwanamuziki mwenzao kwenye bendi hiyo, Kanku Kerry alipata mkataba Japa, hivyi waliondoka naye kwa sharti la sasa kujiita Kilimanjaro Connection.
Hivyo walizunguka nchi nyingi za bara la Asia wakiwa na Kilimanjaro Connection, waliporudi mwaka 1994 alijitoa na baadaye kidogo Asia naye alijitoa na kurudisha upya bendi yake ya Zanzibar Sound na kurejea mkataba wake Bahari Beach Hotel.
Bombenga wakati huu akabaki bila bendi, ambapo muda si muda Asia alipata kazi nchini Bahrain na kumuachia Bombenga mkataba wa Bahari Beach.
Baada ya kuona ameachiwa mkataba wakati hana bendi, Bombenga ndipo alipomfuata Baraka Msirwa na kumuomba vyombo vya muziki ambapo alimpa kwavile havikuwa na kazi kutokana na kufa kwa bendi za MK Group, MK Beat na MK Sound zilizokuwa zikivitumia.
Na hicho ndio kilikuwa chanzo cha bendi ya African Stars niliyoibuni mwenyewe hadi jina, iliyoniletea uhasama mkubwa na dada yake Asha Baraka baada ya kujitoa.
![]() |
Sehemu ya waombolezaji katika Msiba wa Mahufu Bilal, wakiwemo wanamuziki wenzake. |
Nani warithi wa Bombenga?Jibu ni kwamba
kwa upande wa warithi, anao wanawe wawili wanaoonekana kufuata vema nyayo zake, ambao ni Feruzi (22) anayepapasa kinanda na Aziza (19) ambaye ni mwimbaji.
Ikumbukwe Bombenga katika muziki wa dansi amekuwepo kwa zaidi ya miaka 40 na aliyejifunza mengi kupitia sanaa hiyo.Enzi za uhai wake katika moja ya mahojiano aliwahi kusema anavutiwa na waimbaji; Isha Mashauzi, Nasseeb Abdul ‘Diamond’, Flora Mbasha na Hassan Bitchuka.
Haha Hi yo ndoto yake kubwa mwanamuziki huyo ilikuwa baada ya kustaafu shughuli za muziki, ni kujikita kwenye shughuli za ujasiriamali.
![]() |
waombolezaji. |
Kabla ya kuhitimisha historia yake, unapaswa kufahamu kwamba Bombenga ni mtoto wa tano katika familia ya mzee Bilali Mafumu. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya H.H Agakhan, Kigoma na baadae alijiunga na shule ya sekondari Kazima, Tabora nilikosoma hadi kidato cha nne.
Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Bombenga aliyesoma shule moja ya sekondari na mbunge wa Tabora, Ismail Aden Rage, mwaka 1972 alijiunga na JKT kwa mujibu wa sheria ya enzi hizo, alikojifunza kuimba na kupuliza Saxophone.
Kwa Dar es Salaam alikuwa akiishi Vingunguti pamoja na familia yake ambayo ni mkewe na watoto saba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...