Na Ismail Ngayonga,MAELEZO-DAR ES SALAAM
MAENDELEO ya nchi
yetu kwa kiasi kikubwa yanategemea matumizi endelevu ya maliasili zilizopo
nchini uwepo wake hizi ni muhimu kwa ajili ya mahitaji ya sasa na ya vizazi
vijavyo.
Hata hivyo, Taarifa
ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini ya mwaka 2019 imebainisha kuwepo kwa shughuli za kiuchumi na kijamii
zisizo endelevu ambazo zimeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa
mazingira nchini.
Uharibifu huo ni
pamoja na uharibifu wa ardhi, ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu,
upotevu wa bioanuai, uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa mifumo ikolojia ya
maji, kupungua kwa ubora na upatikanaji wa maji na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, hivi karibuni
kumekuwepo na ongezeko la viumbe vamizi, taka za kielektroniki, taka za
kemikali, uchafuzi utokanao na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na
gesi, ambavyo kwa kiasi kikubwa vimechangia uharibifu wa mazingira na
kuhatarisha afya ya binadamu na ikolojia kwa ujumla.
Katika kulinda,
kuhifadhi na kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira nchini, Ofisi ya
Makamu was Rais (Muungano na Mazingira), imeendelea kusimamia utekelezaji wa
Sera, Sheria, Mikakati mbalimbali ya hifadhi ya mazingira na Mikataba ya
Kimataifa ya Mazingira.
Katika kipindi cha
mwaka 2019/20, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imeendelea
kutekeleza Mkataba wa Stockholm Kuhusu Udhibiti wa Kemikali Zinazodumu Katika
Mazingira kwa Muda Mrefu na tayari Serikali imeandaa Mpango wa Kitaifa wa utekelezaji
wa mwaka 2018-2023.
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadiro ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Zungu anasema Mpango huu
unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kwa gharama ya Tsh. bilioni
1.8 chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
Waziri Zungu anasema kupitia
mpango huo, Serikali iliratibu zoezi la ukusanyaji wa jumla ya sampuli 553 za
mafuta ya transfoma zinazokisiwa kuwa na kemikali ya Polychlorinated Biphenyls
(PCBs) ambazo zinadumu katika mazingira kwa muda mrefu na hivyo kuhatarisha
afya ya binadamu na mazingira.
‘Sampuli hizi
zilikusanywa kutoka katika mikoa ya Dodoma, Singida, Mwanza, Kilimanjaro,
Arusha, Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Morogoro na kwa pande wa Zanzibar,
katika Mikoa ya Mjini Magharibi - Unguja na Kaskazini Pemba, ambapo katika sampuli zilizokusanywa, sampuli
22 zilibainika kuwa na kemikali ya PCBs’’ anasema Waziri Zungu.
Kwa mujibu wa Waziri
Zungu anasema kemikali hizo ni mojawapo ya kemikali zinazodhibitiwa chini ya
Mkataba wa Stockholm ambazo zinapaswa kuondoshwa kwenye matumizi ifikapo mwaka
2025.
Aidha Waziri Zungu
anasema sanjari na zoezi hili, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa
kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuelimisha jamii
kuhusu madhara yatokanayo na kemikali ya PCBs ambapo elimu ilitolewa kwa
wananchi takriban 810 wakiwemo wafanyakazi 45 wa TANESCO waliopewa mafunzo ya
namna bora ya kudhibiti kemikali hiyo.
Zungu anasema Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) pia imekamilisha na kuanza kutekeleza
Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Kemikali na Taka Hatarishi wa mwaka 2020 –
2025 na kukamilisha Mfumo wa Kieletroniki wa Upatikanaji wa Taarifa za Kemikali
na Taka nchini, ambapo hatua inayoendelea kwa sasa ni kutoa mafunzo kwa
wataalam watakaokuwa wanatumia mfumo huo.
Waziri Zungu anasema
Ofisi yake pia inatekeleza Mpango wa Kimataifa wa Ufuatiliaji wa Madhara ya
Kemikali Zinazodumu Katika Mazingira Kwa Muda Mrefu (2017 – 2020), ambapo tayari
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu imekusanya sampuli 55 za maziwa ya wamama
wanaonyonyesha na kutumwa nchini Ujerumani kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
‘Sampuli hizi
zilichukuliwa katika mikoa ya Mbeya, Pwani, Arusha, Mwanza na Dodoma. Vilevile,
sampuli 44 za hewa zilichukuliwa katika Mkoa wa Pwani na kutumwa nchini
Uholanzi na Sweden kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini kiwango cha
kemikali hizi katika hewa’’ anasema Waziri Zungu.
Udhibiti wa kemikali
na kemikali taka ni muhimu katika kila sekta inayotumia kemikali ili kulinda haki ya kikatiba ya kila mtanzania na azimio
la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu ya kuhakikishiwa mazingira bora ya
kuishi kwa afya na familia yake.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...