Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR -TAMISEMI) inatekeleza Mpango wa wa
Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (BLUE PRINT) unaolenga kuboresha Mazingira
ya Biashara na Uwekezaji kwa Njia ya Majadiliano ili kuwainua Wananchi
Kiuchumi.
Mpango huo
unatekelezwa ili ili kukabiliana na changamoto za kibiashara na uwekezaji
hususani zinazokwamisha kukua kwa biashara na maendeleo ya kiuchumi katika
ngazi ya chini na wananchi wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali za
kiuchumi Vijijini na Mijini.
Mpango unahamasisha
uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji kwa vitendo ili kutatua
changamoto za kibiashara ambazo Serikali inakabiliana nazo katika kukuza
uchumi, kuleta maendeleo, kukuza ajira na kuondoa umasikini katika Taifa.
Katika kuhakikisha
kuwa mpango huu unatekelezwa kikamilifu, wadau mbalimbali wameshirikishwa ambao
ni Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, Ofisi ya Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Jumuiya ya
Tawala za MitaaTanzania (ALAT), Chemba ya Wafanyabiashara, Wakulima na Wenye
Viwanda Tanzania (TCCIA) na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF).
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo anasema
Serikali inasimamia na kutekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara
(BLUE PRINT) unaokusudia kuondoa vikwazo na kero mbalimbali za biashara na
uwekezaji ili kurahisisha mazingira ya kufanyia biashara.
Anasema kufikia
Februari 2020 tozo mbalimbali zimeondolewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa
zikiwemo ushuru wa huduma kwa biashara za nyumba za kulala wageni, marekebisho
ya ushuru wa mazao kati ya asilimia 3 hadi 5 wa awali hadi asilimia 3 kwa mazao
ya biashara na chakula yasiyopungua tani moja.
‘Tozo na ushuru huo umeondolewa
kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, aidha Serikali inaendelea
kufanya tathmini ili kuondoa kodi zenye kero zinazokwamisha ufanyaji wa
biashara na uwekezaji zikiwemo tozo zinazotozwa na Taasisi zaidi ya moja’’
anasema Waziri Jafo.
Waziri Jafo anasema hadi
Februari 2020, jumla ya hekta 854,821.59 zimetengwa katika Mamlaka za Serikali
za Mitaa kwa ajili ya uwekezaji zikiwemo hekta 403,784.92 kwa ajili ya viwanda
vikubwa, vidogo na vya kati pamoja na hekta 45,231.33 zilizotengwa kwa ajili ya
uwekezaji wa masoko, minada, hoteli, ujenzi wa stendi za mabasi, maduka na
biashara.
Akifafanua zaidi Jafo
anasema kupitia kaulimbiu ya Mkoa Wetu, Viwanda Vyetu, iliyoanza kutekelezwa
katika mwaka wa fedha 2017/18, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imesimamia na kutoa
hamasa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mkakati wa
ujenzi wa viwanda ili kukuza uchumi na ustawi wa jamii.
Anasema hadi kufikia
Februari 2020, jumla ya , viwanda 4,876 vimeanzishwa na kuvuka lengo la
kuanzisha viwanda 2,600 lililowekwa sawa na viwanda 100 katika kila Mkoa kwa
Mikoa yote 26 Tanzania Bara, ambapo kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 108,
viwanda vya kati ni 236, viwanda vidogo 2,522 na viwanda vidogo sana 2,010.
Jafo anasema Mikoa 8
ya Tabora, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Geita, Songwe, Morogoro na Dodoma
imefanikiwa kuandaa wasifu wa kiuchumi ili kubainisha fursa za kiuchumi na
uwekezaji unaotumika kuandaa makongamano ya uwekezaji yanayotumika kuwatangazia
wadau fursa za uwekezaji zinazopatikana katika Mikoa hiyo ili waweze kuzitumia.
Kuhusu vitambulisho
vya wafanyabiashara wadogo, Jafo anasema hadi Februari 2020, jumla ya wafanyabiashara
wadogo 1,551,126 wamepatiwa vitambulisho ambavyo vimewezesha kukusanywa kwa
Tsh. Bilioni 31.02 katika Mikoa yote 26, huku lengo kubwa likiwa ni kuwatambua wafanyabiashara
wadogo na kuwawekea mazingira rafiki ya ufanyaji biashara.
‘Ofisi ya
Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za
kusimamia wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wadogo ili kutambua mchango wa
biashara hizo katika ukuaji wa uchumi’’ anasema Waziri Jafo.
Pia Jafo anasema Ofisi
ya Rais - TAMISEMI imeendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Utoaji wa
Vibali vya Ujenzi ulioanza kutekelezwa mwaka 2018 kwenye Halmashauri 184
Tanzania Bara, ambapo mwongozo umesaidia kupunguza muda wa kushughulikia kibali
cha ujenzi kutoka wastani wa siku 180 hadi wastani wa siku 7.
Kuanzishwa kwa Mpango
wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara (BLUEPRINT) kutasaidia kuleta mageuzi ya
kiuchumi kwa vitendo na kubadilisha hali ya uchumi wa jamii, kupunguza gharama
na vikwazo vya kibiashara na kuwa na msingi thabiti wa mapato ya Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Aidha uwepo wa Mpango
huo pia utafafsiri kwa vitendo Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Maendeleo Endelevu ya Kimkakati (SDGs)
pamoja na na mikakati mbalimbali ya Serikali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...