Na Ismail Ngayonga,MAELEZO-DAR ES SALAAM
SEKTA ya Kilimo nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo
ya uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu
tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda.
Katika kipindi cha
miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei
za Mwaka 2015
limeongezeka kwa asilimia 17
kutoka Tsh. Trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi Tsh. Trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile, sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58
Mwaka 2018 na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa huku sekta ndogo ya
mazao ikichangia asilimia 16.2 na hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo.
Ili kufikia kiwango
malengo makubwa ya uzalishaji wa mazao, Sera zinazoongoza utafiti zina mchango
mkubwa katika kupanga maendeleo ya sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na ya
kuboreshea viwango vya maisha ya wananchi kwa kuchochea ukuaji na kuongeza tija
katika sekta muhimu za uzalishaji za uchumi wa taifa.
Historia inaonyesha
kuwa nchi zilizozingatia sera zenye mwelekeo wa utafiti thabiti zimefanikiwa
kujenga uchumi wenye ushindani kwa kutumia rasilimali walizonazo, na
kuziendeleza kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wao.
Katika jitihada hizo,
Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeendelea kuboresha
uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na uvuvi katika eneo la Tafiti na
Ushauri elekezi ili kutoa huduma ya elimu ya ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema Serikali kupitia SUA imeendelea na
miradi mipya 13 ya utafiti yenye lengo la kuboresha uzalishaji wa mazao ya
kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ili
kuwezesha wananchi kuzalisha mali na malighafi za mazao ya kilimo kwa ajili ya
viwanda.
Prof. Ndalichako
anasema Chuo hicho pia kimeweza huduma ya elimu ya ushauri wa kitaalamu kwa
wakulima 9,500 kwa kutumia vituo atamizi, mashamba darasa, semina, kozi fupi,
runinga na redio kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija na kupunguza
umaskini kwa wananchi.
‘Mafunzo hayo
yametolewa kwa wakulima katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Iringa, Dodoma,
Tabora, Tanga, Pwani na Morogoro kwa lengo la kutoa elimu kuhusu kilimo na
ufugaji’’ anasema Prof. Ndalichako.
Aidha Prof.
Ndalichako anasema SUA pia ) imepima jumla ya sampuli 1,553 zikiwemo sampuli za
udongo 1,180, za mimea 297, za mbolea za viwandani 20, za samadi tisa (9) na
sampuli za maji 47 kutoka kwa watafiti mashirika ya kilimo, Viwanda na Taasisi
mbalimbali pamoja na wakulima binafsi.
Waziri Ndalichako
anasema kuwa Serikali imeingia mikataba mipya 13 ya mahusiano na Taasisi
nyingine za ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo wafanyakazi na wanafunzi
katika kufanya tafiti za kisayansi na kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji
wenye tija katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
Anazitaja taasisi
hizo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sophia kilichopo Japan; National
Institute of Health - Korea; Foundation Pierre Fabre - France; Kunming
Institute of Zoology, Chinese Academy of
Science; Silverlands Tanzania Limited - Iringa, Tanzania; College of Animal
Science and Technology Nanjing Agricultural University - China; Agronomos Sin
Fronteras Foundation (ASFF ) - Iringa Tanzania; University of Leeds – UK; na
Wuhan University (WHU) – China.
Akifafanua zaidi
Prof. Ndalichako anasema katika kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia Serikali imejenga jengo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,400 kwa
wakati mmoja litakalokuwa na maabara nane zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100
kila moja.
Prof. Ndalichako
anasema Serikali pia imekamilisha ujenzi wa jengo la utafiti wa wanyama na
wadudu kwa ufadhili wa mradi wa Eastern and Southern Africa Centers of
Excellence for Innovative Rodent Pest Management and Biosensor Technology
Development (ACE II, IRPM and BTD) na kuendelea na ukarabati wa madarasa
likiwemo jengo la Hay Building kwa lengo la kuongeza nafasi za kufundishia na
kujifunzia.
Mazao ya Kilimo ni
malighafi muhimu sana katika viwanda, hivyo ni utafiti ni nguzo muhimu sana inayoweza
kuleta kuleta ubunifu wa bidhaa, uboreshaji wa bidhaa, kuongeza ufanisi wa
huduma, tija na ubora wa utendaji katika soko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...