Na Emmanuel J. Shilatu
WAKATI mgumu wa janga la ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya Corona vimetuonyesha aina ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuliyenae Watanzania aitwaye Dkt. John Pombe Magufuli (JPM).
Tumemshuhudia JPM akisitisha sherehe zote za kuwasha Mwenge, sherehe ya Muungano na sherehe ya Wafanyakazi na kuelekeza fedha hizo ziende kupambana na janga la Corona. Hapa JPM aliweka pembeni anasa na mazoea yote na kuelekeza fedha ziende kupambana kulinda uhai wa Watanzania kama alivyoapa kiapo cha kulinda uhai na usalama wa Raia wake, JPM ametimiza hili.
Tumemuona JPM akiwa na msimamo mkali wa kutokufungia Raia wake ndani hali iliyopelekea mataifa mengine kumbeza. Leo hii wale wale waliombeza ndio hao hao wanaiga msimamo wa JPM na kuanza kuwafungulia Raia wao. JPM ameifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano Duniani kiuongozi.
Mwamba JPM akaendelea kuwaonyesha Mabeberu juu ya msimamo na ujasiri wake kwa kukataa mikopo kipindi hiki na badala yake watusamehe madeni tofauti na nchi nyingine ambazo wamekopa mikopo hiyo. Huu ni msimamo, ujasiri na uzalendo wa Rais Magufuli kwa nchi yake.
Ni JPM huyu huyu shujaa aliwasihi Watanzania kutokubali misaada ya kukabiliana na Corona toka nchi nyingine kipindi hiki kwani mingine inawezekana isiwe salama; JPM hakubweteka na vipimo vya Corona akavifanyia utafiti na kubaini vina kasoro, jambo lililozua gumzo Duniani. Huu ni ushahidi wa uchapa kazi usiku na mchana alionao JPM na Serikali yake kwa maslahi mapana ya Watanzania.
Ni Rais Magufuli amefanikiwa kuwaunganisha Watanzania kumtegemea Mwenyezi Mungu pekee kutuokoa na janga la ugonjwa wa Covid 19 ambapo alitenga siku 3 za maombezi. Huyo ndio JPM Mcha Mungu na Mzalendo kwa Taifa lake.
Sakata la Corona limetuonyesha Dkt. Magufuli sio tu Rais wa nchi bali ni Baba anayeipenda familia yake (Tanzania) kupitia Uzalendo, ujasiri, ucha Mungu, uadilifu, ufuatiliaji na uchapa kazi.
*Shilatu E.J*
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...