Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukuwa uamuzi
wa kulegeza baadhi ya mambo mambo kumi yaliyowekwa baada ya kufanikiwa
kukabiliana kwa kiasi kikubwa na mripuko wa Virusi vya Coroma vilivyoleta
mtafaruki katika Mataifa mbali mbali Duniani.
Uamuzi huo wa SMZ Unaungana na ule uliochukuliwa na
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuviruhusu Vyuo vyote vya Elimu
ya juu kuendelea na Programu zao kama kawaida kwa upande wa Zanzibar kuanzia
Tarehe 1 Juni 2020.
Akitoa Taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kwa Umma kupitia Vyombo vya Habari Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi huo unakwenda sambamba na Wanafunzi wa Kidato
cha Sita nao kuanza masomo yao Tarehe 01 Juni 2020 ili kuwawezesha
kujitayarisha na Mitihani yao ya Taifa.
Alisema kufuatia maamuzi hayo Serikali imeiagiza
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
kushirikiana na kikamilifu ya Wizara ya Afya katika kuandaa Miongozo ya Kiafya
itakayopaswa kuzingatiwa ili kuepuka maambukizo pamya ya Virusi vya Corona.
Balozi Seif alibainisha kwamba Wanafunzi wa Kidato
cha Kwanza hadi cha Tano pamoja na Wanafunzi wa Skuli za Msingi, Maandalizi na
Madrasa, Skuli na Vyuo vyao zitaendelea kufungwa hadi pale yatakapotolewa
maelekezo mengine na Serikali Kuu.
Kuhusu Mchezo wa Soka Zanzibar, Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar alisema Ligi Kuu ya Zanzibar itaendelea kuanzia Tarehe Tano
Juni 2020 ambapo Wizara inayosimamia Sekta ya Michezo kwa kushirikiana na Chama
cha Mpira wa Miguu Zanzibar {ZFF} pamoja na Wizara ya Afya ziandae Muongozo na
namna bora ya kuendesha Ligi hiyo.
Kwa upande wa Michezo mengine yote inayochezwa na
Vilabu, Vikundi au Makundi ya Wananchi na hata Mtu Mmoja Mmoja ikiwemo Mazoezi,
Mashindano ya Viwanjani na Ufukweni Balozi Seif alisema Makundi yote hayo
yatasubiri hadi itakapotolewa Taarifa nyengine hapo baadae.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba
tokea kuripotiwa kwa rasmi kwa Ugonjwa wa Corona mnamo Tarehe 19 Machi 2020,
Serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu muenendo wa Ugonjwa huo.
Alisema hadi kufikia leo Tarehe 27 Mei 2020 Watu
wapatao Mia 134 wamethibitishwa kuambukizwa Virusi vya Ugonjwa wa Corona , kati
yao Wagonjwa 109 wamepatikana Unguja na Wagonjwa 25 wameripotiwa Kisiwani
Pemba wakati Wagonjwa Sita walifariki
Dunia.
Balozi Seif alifafanua kwamba jumla ya Wagonjwa 115
wamepona ambapo hadi sasa wamebakia
Wagonjwa 19 wakiendelea na huduma za Afya katika Kambi za matibabu za Kidongo Chekundu, Skuli
ya Sekondari ya JKU Mtoni, Kihinani na Kidimni kwa Upande wa Unguja wengine
katika Kituo cha Vitongoji kwa upande wa Kisiwa cha Pemba.
Alisema jitihada hizo zote zimefanikiwa kutokana na
utekelezaji wa maelekezo na maagizo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa akiwemo Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein ambao wanastahiki
kupongeza kwa dhati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Jamii
Nchini kwa jitihada inazochukuwa za kuitikia wito na Ushauri wa Serikali pamoja
na Wataalamu wa Sekta ya Afya katika suala zima la mapambano dhidi ya Virusi
hatari vya Corona { CAVID – 19}.
Alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeridhika na juhudi
hizo zilizoleta faraja kubwa kwa kila Mwananchi kuendelea kuishi kwa matumaini na
kuwataka waondoe hofu kutokana na janga hilo lililoiathiri Dunia hivi sasa.
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba pamoja na Serikali Kuu
kuregeza masharti yaliyotolewa ya kukabiliana na Maradhi yanayotokana na Virusi
vya Corona aliwasisitiza Wananchi kwamba lazima waelewe kuwa maradhi hayo bado
yapo na ni tishio linaloendelea kutishia Afya za Wanaadamu Ulimwengu mzima.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa Tamko Rasmi
mnamo Tarehe 19 Machi 2020 na kulekeza Mambo Kumi ya kutekelezwa katika
kuhudumia Waathirika wa Virusi vya Corona sambamba na udhibiti wa Maradhi
yanayosababishwa na Virusi hivyo.

Uongozi wa Shirika la Utangazaji
Zanzibar {ZBC} ukimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alipofika Kituo cha Matangazo Karume House kutoa Taarifa ya Serikali
kuhusu kuregeza masharti yaliyowekwa kuhusiana na Ugonjwa wa Corona.
Balozi Seif akiwa katika Studio za
Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Karume House kutoa Taarifa za ulegezaji wa
msharti ya Virusi vya Corona vinavyosababisha Homa kali.
Mtayarishaji wa Vipindi vya Afya
katika Kituo cha Matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Bibi
Mwanakhamis Sose akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kumaliza kutoa Taarifa ya Serikali.
Balozi Seif Ali Iddi akiagana
na Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar na Naibu
Wake Bibi Narsa Mohamed mara baada ya kumaliza kutoa aarifa ya Serikali kuhusu
Corona.Picha na – OMPR – ZNZ.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...