Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri akipokea msaada wa Vikinga Uso (Face shields) kutoka kwa Taasisi ya GFF ambayo imefika ofisini kwake kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga na Corona.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri akiwa katika kikao cha pamoja na wadau wa maendeleo Taasisi ya GFF ambayo imefika ofisini kwake kukabidhi msaada wao wa vifaa vya kujikinga na Corona.
Mkurugenzi wa Taasisi ya GFF, Aisha Msantu akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya kujikinga na Corona kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri.
Charles James, Michuzi TV
TAASISI ya Glaring Future (GFF) imeahidi kushirikiana na serikali katika kuelimisha wanafunzi madhara ya mimba katika umri mdogo, matumizi ya dawa za kulevya na elimu ya kujitambua pamoja na kupeleka vipima joto kwa ajili ya kupimia maambukizi ya ugonjwa wa Corona pindi wanafunzi watakaporejea mashuleni.
Ahadi hiyo imetolewa wilayani Mpwapwa, Dodoma na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo , Jabir Shekimweri wakati walipomtembelea ofisini kwake na kumkabidhi vifaa mbalimbali vya kujikinga na Corona ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Vifaa ambavyo GFF imekabidhi ni Ndoo 30 za Lita 20 kwa ajili ya kunawia mikono na maji tiririka, Vitakasa Mikono 12 vya Mililita 500, Sabuni za kunawia mikono 25 pamoja Vikinga Uso (Face shields) 30 ambazo vyote kwa pamoja vina thamani ya Sh Milioni Moja.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri ameipongeza taasisi hiyo kwa kuungana na serikali katika kipindi hiki lakini pia kwa kuchagua Wilaya hiyo huku pia akiwaomba wadau wengine kujitokeza.
"Niwapongeze na niwashukuru sana, huu ni Moyo wa ajabu sana ambao kwa hakika Mwenyezi Mungu atawalipia. Niwasihi tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuwahudumia watanzania wenzetu, na mimi niwaambie tu niko tayari kuwapa sapoti yoyote katika jambo lolote la kimaendeleo ambalo mtaguswa nalo wilayani kwetu.
Niwaombe pia katika kipindi hiki ambacho taasisi zingine kama Shule ya Sekondari zinafunguliwa tunaomba ikiwapendeza pia mtuletee na vipama joto kwa ajili ya kupimia joto wanafunzi wetu, lakini mrudi tena kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi hasa watoto wa kike," Amesema DC Shekimweri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya GFF, Aisha Msantu amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa namna ambavyo amechukua hatua madhubuti za kupambana na ugonjwa huo nchini kwa kuangalia mazingira ya Nchi yetu bila kufuata presha ya Mataifa menginge.
Amesema wataendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia watanzania huku akiahidi kurudi tena wilayani hapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi lakini pia kuwapa elimu ya ujasiriamali vijana wa Mpwapwa.
" Tukushukuru DC kwa kutupokea, sisi tunaguswa na kasi ya serikali yetu chini ya Rais Dk Magufuli kwa namna inavyotuhudumia wananchi wake, tunaahidi huu hautokua mwisho wetu sisi kuja hapa Mpwapwa tutaendelea kuja kwa ajili ya kusaidiana na watanzania wenzetu kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Ujasiriamali," Amesema Aisha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...