MZEE wangu Abdulrhman Kinana acha leo niseme ukweli nilitaka kushangaa.Ndio nilitaka kushangaa kuhusu wewe.Unajua kwanini ?Nitaeleza huko mbele ya safari kwenye maelezo yangu.
Hata hivyo kabla ya kuendelea naomba nikurejeshe kwenye kile ambacho mzee Kinana amekizungumza jana akiwa mkoani Arusha baada ya kwenda kumtembelea na kumsalimia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Arusha.
Akiwa katika ofisi ya CCM Mkoa wa Arusha Kinana amesikika akisema hivi "Ni kweli jambo hili liliwahi kutoka,najua nilikereka wakati fulani, nilihuzunika na kukasirika, katika kushughulika na lile suala nadhani nilikwenda mbali kidogo nikasema maneno ambayo labda hayakuwa mazuri kwa kiongozi wangu, Mwenyekiti wa Chama(CCM) na kwa Rais.
"Na baada ya kutafakari nadhani ni wakati muafaka, ni wakati mzuri wa kuungana nao na kumtaka radhi Mwenyekiti na kumuomba msamaha kwa kusema Mwenyekiti nimekukwaza, nimekukera, nimekuhuzunisha, na nadhani sio kwa mwenyekiti tu peke yake , mi nadhani wako wanaCCM wengine na watanzania ambao walisema Ah! mbona ndugu Kinana amekwenda mbali kiasi hicho.
"Labda kupitia kwake vile vile na wengine wote waliohuzunika na kusikitishwa niwaombe radhi lakini haswa haswa nadhani nimuombe radhi Mwenyekiti wangu na Rais kwa yale ambayo niliyasema na unajua misahafu yetu lakini vile vile katika maisha ni uungwana wakati mwingine kukaa na kutafakari na kuomba radhi.Sina shaka hata kidogo naye leo akisikia hayo bila shaka ataniwia radhi".
Hicho ndicho Kinana amekizungumza baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.Tunafahamu Kinana alikuwa kimya sana.Amekuwa kimya kwasababu kwa sasa amepumzika siasa kwa maana ya nafasi yake ya mwisho ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM.Hivyo muda mwingi amekuwa akiendelea na majukumu yake mengine.
Sote tunakumbuka kilichotokea kuhusu mzee Kinana.Sitaki kurudia kwasababu walio wengi wanakumbuka.Kifupi alitoa maneno kupitia sauti iliyosemekana ni yake kwenye mitandao ya kijamii na hivyo ikaleta shida .Hayo yamepita na sasa tunaganga yajayo.
Ukweli kitendo cha Kinana kutoka hadharani na kuomba radhi kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk.John Magufuli ni jambo lenye kuonesha nidhamu, utiifu, busara na hekima ya hali ya juu.Kinana ameonesha ukomavu wa kisiasa.Ameonesha namna ambavyo amebaini alikosea na kisha ameamua kuomba radhi.
Ndio Kinana amemuomba radhi Rais Magufuli, amewaomba radhi wanaCCM, ameomba radhi kwa Watanzania wote ambao kwa namna moja au nyingine aliwakwaza.Hata hivyo kwenye maelezo yake amesisitiza hasa hasa kwa Rais na Mwenyekiti wake Dk.Magufuli.
Ujue ndugu yangu Mtanzania iko hivi baada ya ile sauti ya Kinana kuvuja huko mtandaoni, mengi yalizungumzwa.Wengi walijadili na kila mmoja kwa kadri ya ufahamu wake.Ni kweli watu walijadiliana sana kuhusu sauti ile.Mjadala ulikuwa mkubwa sana .Wapo waliohoji ni kweli ile sauti ilikuwa ya Kinana au imetengenezwa na wabaya wake kisiasa.
Nilichofarijika ni kumsikia Kinana akiomba radhi kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk.Magufuli.Amefanya jambo jema sana.Hata hivyo kwa kuwa amekiri na kuomba radhi nami angalau naweza kueleza jambo japo kidogo kuhusu Kinana.
Nafahamu unapotaka kumzungumzia mzee Kinana lazima ujipange.Unapotaka kuelezea historia ya Kinana uwe na muda wa kutosha na uwe unajua hatua kwa hatua kuhusu maisha yake hasa ya kisiasa na kiuongozi.Nikiri historia ya Kinana ina mambo mengi ya kujifunza.Ndio.
Unachopaswa kufahamu na kuweka akilini Kinana ni kati ya wanasiasa waliojijengea heshima kubwa katika nchi yetu.Najua kuna watu wanaomjua vizuri kuliko mimi.Huo ndio ukweli.
Kwa kukumbusha tena kwa ufupi sana.Kinana ni mwanasiasa aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini. Amewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.
Kinana amewahi kulitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa miaka mingi kabla ya kustaafu akiwa na cheo cha Kanali.Mzee Kinana amewahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki mwaka 2001 mpaka mwaka 2006.Amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha kwa muda wa miaka 10.Pia amewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuanzia Novemba 2012 hadi Mei 2018.
Nimegusa kwa kifupi sana kuhusu Kinana na huyo ndio Kinana ambaye nataka kumzungumzia japo kidogo baada ya kujitokeza hadharani na kisha kuomba radhi kwa Rais Magufuli.Nikiri nimepata nafasi ya kuwa karibu na Kinana na hasa wakati wa ziara zake za kuzunguka nchi nzima kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wana CCM pamoja na Watanzania.
Kinana aliyekuwa akiambatana na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye walifanya kazi kubwa na ya kutukuka ya kukijenga Chama chao.
Ukiondoa yaliyotokea hapo katikati Kinana amekuwa mfano wa kuigwa.Katika CCM wanamjua vizuri Kinana na mchango wake kwa Chama na Serikali.Kinana ndio msuka mipango ya wagombea urais wa CCM kuanzia Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne na hata kwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Ndio maana mwenyewe kwenye maelezo yake ameeleza wazi ametafakari na kubaini aliteleza na sasa anaomba radhi.Kuomba kwake radhi ndiko ambako msingi hasa wa mimi kuamua kuandika hiki ambacho nakiandika.Ndio , kwani kuna dhambi gani ya kueleza chochote kuhusu Kinana.
Waliyoyapitia kwenye ziara hiyo binafsi niliyashuhudia kwa macho.Waliyoyasema na kutenda yamebaki kumbukumbu isiyofutika kwenye historia ya maisha yangu.Milima na mabonde ya ziara yote yanabaki kwenye kumbukumbu za maisha yangu.Ukweli kwenye medani ya siasa na uongozi Kinana anabaki kuwa mwalimu mzuri.
Katika ziara yake aliyokuwa ameambatana na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye kuna mengi ambayo ameyafanya kwa vitendo na kuyasema.Wana CCM na Watanzania wanayakumbuka.
Pamoja na yote kwenye ziara hizo ambazo zilitumia takribani miaka miwili kwa maana ya miezi 24 na siku 28 Kinana alipita jimbo kwa jimbo, wilaya kwa Wilaya na Mkoa kwa Mkoa.Kote huko alikopita mbali ya kukagua miradi ya maendeleo alikuwa na jukumu la kuijenga CCM yake ambayo ilikuwa kwenye hali mbaya.Haikuwa inapendwa tena na Watanzania na hivyo kazi ya Kinana ikawa ni kuirejesha CCM kwenye mioyo ya Watanzania.Alifanikiwa.
Achana na hilo, ambalo kwangu lilibaki kama kumbukumbu kwenye ziara za Kinana ni uungwana wake wa kuomba radhi kila alipoona kuna kosa aidha limefanywa na CCM, Serikali au viongozi wa Chama chake.
Nakumbuka alikuwa akiomba radhi mara kwa mara kwa Watanzania.Waliokuwa kwenye zile ziara wanakumbuka.Kinana alikuwa akisimama mbele ya mamia ya wana CCM na watanzania kuomba radhi.
Alikuwa akisisitiza kuwa kuomba radhi ni njia mojawapo ya kujiimarisha na wala sio kujidhalilisha.Alikuwa akieleza kuwa muungwana huomba radhi anapobaini amekosea.
Hivyo kila alipokuwa akielezwa makosa ya CCM na Serikali yake hakusita kuomba radhi na kueleza yaliyotokea hayatatokea tena.Ndio maana pale mwanzoni wakati naanza kuandika hiki ambacho unakisoma nilisema hivi "Mzee wangu Kinana nilitaka kushangaa...hatimeye nimekumbuka hekima na busara."
Kwa kuwa yeye alihubiri kuomba radhi kwa anayebaini kukosea dhidi ya aliyemkosea, hivyo nilikuwa nasubiri kuona lini Kinana atatafakari na kubaini kosa lake na kisha kuomba radhi kama ambavyo amekuwa akituhimiza wengine.Hatimaye ameonesha kile ambacho anakiamini na kukihubiri kwa wengine bado kinayo nafasi katika maisha yake ya kila siku.
Ameomba radhi kwa Rais Magufuli.Ameomba radhi kwa Watazania.Wakati ule upepo unavuma vibaya kwa Kinana baada ya ile sauti yake kuvuja mitandaoni nakumbuka kuna mwanasiasa mmoja ambaye anayo nafasi Serikalini aliamua kujiondoa kwenye kundi ambalo tuliamua kuliunda la WhatsApp kama marafiki wa Kinana.
Katika kundi hilo Kinana hakuwepo ila tupo watu ambao tumepata nafasi ya kuwa naye karibu na hasa wakati wa ziara zake.Jamaa yetu aliamua kujiondoa kwani aliona ni kama vile anakaribisha hatari kwenye safari yake ya kisiasa.Huenda baada ya Kinana kujitokeza kuomba radhi atarudi tena kundini.
Kwa kuwa Kinana anajua huenda wako wengi walikwazika baada ya kufanya kile alichokifanya ndio maana ameamua kuomba radhi kwa Wana CCM na watanzania wengine.Naamini na jamaa yetu ambaye alijitoa kwenye kundi la marafiki wa Kinana baada ya kumsikia jana atakuwa na amani ya moyo.
Tunamkaribisha maana wengine tuliamua kubaki na kundi letu, nia yake ni njema na liliundwa kwa ajili ya kuhamasisha kulitumikia taifa letu kwa uadilifu na uaminifu na ndicho tunachoendelea kukifanya tangu wakati huo.
Somo ambalo Kinana analiacha kwa Watanzania ni kwamba hata uwe mkubwa kiasi gani, hata kama una cheo au umewahi kuwa na cheo kiasi gani bado unalojukumu la kuheshimu viongozi wako.
Uzuri nchi yetu tumebahatika kuwa na Rais mwenye kusamehe,sina shaka hata kidogo atamsamehe Kinana baada ya kuomba radhi na kuomba radhi ni jambo la kiungwana. Yaani sijui nikoje nimejikuta naandika tu bila hata ya kumsailimia Mzee Kinana.
Kabla ya kuweka nukta ya mwisho Mzee Kinana shikamoo, habari za siku tele.Ni mimi Said Mwishehe nakusalimia na kukutakia afya njema na maisha marefu yenye mwisho mwema.
Simu yangu ni ile ile 0713833822
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...