BAADA YA MIAKA 30 WOTE TUPIGE KELELE KWA LIVERPOOL YAKEE

Charles James, Michuzi TV

NI kama Ndoto! Wale wote waliokua wanatusimanga, wanatuponda na kutukejeli leo wametupost kwenye status za WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii wakitupongeza.

Kwenye Radio na Televisheni, Magazeti na Mitandaoni stori ni moja tu mjinii, Liverpool ndio Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya England.

Subirio la miaka 30 limetimia, kiu yetu ya kubeba taji la England imekatika. Hakuna mwenye uthubutu wa kutukejeli tena " Mara ya mwisho kuchukua ubingwa ni lini?" Maana tutamjibu "Ni leo".

Yote haya yamewezekana kwa sababu ya uvumilivu wa mioyo ya wana-Liverpool duniani kote. Moyo uliojengwa tangu zama za Bill Shankly, Bob Paisley hata sasa chini ya Klopp.

Tumepitia nyakati ngumu zenye maumivu, mateso na kebehi, nyakati ambazo hata Chelsea iliyoanza kutamba karne ya 21 ilijiona kubwa kuliko sisi.

Tungeongea nini mbele ya Manchester United? Tuliwapita mataji, wakapambana wakatufikia na kutupita. Arsenal licha ya wao pia kujikongoja bado sisi tulikaa muda mrefu bila kubeba ubingwa wa Ligi.

Chelsea na Man City ndio kama hivyo walishajiona wababe wa England. Nafasi yetu ingekua wapi? Tulijipa matumaini usoni huku mioyo yetu ikichakaa kwa maumivu.

Bado tuliamini katika falsafa yetu ya You'll Never Walk Alone. Tuliamini baada ya mateso makali kuna nyakati za dhahabu zinakuja mbeleni. Lakini nani aliziona?

Baada ya Dalglish kuondoka msimu wa 1989/90 ambao tulitwaa taji la mwisho. Hakuna Kocha ambaye aliturudishia ufalme wetu hadi pale tulipompokea 'mkombozi' Klopp.

Souness alishindwa kuonesha uimara wake wa uwanjani akiwa kocha wetu, Roy na Houllier waliishia kutupa FA na Carling Cup.

Benitez tunamkumbuka kwa Usiku wa Istanbul. Hodgson ni kama hakuwahi kuwa kocha wa Liverpool. Wala usinikumbushe kuhusu Brendan Rodgers.

Ni mateso, karaha na kusimangwa tu. Ungemsikia shabiki wa United akirusha kijembe " Mara ya mwisho Liverpool kutwaa ubingwa Rais wa Tanzania alikua ni Alhaji Hassan Mwinyi, leo Rais ni Dk Magufuli".

Halafu shabiki wa Chelsea angeongezea hii, " Mara ya mwisho Liverpool kubeba Ligi ilikua ukipata kona tano basi zinageuka kuwa goli,". Ilimradi watukejeli tu. Tungejisifu na nini watuelewe?

Ipo misimu tulikosa ubingwa, tukakosa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa, tukaikosa hata nafasi ya kucheza Europa League. Maskini sisi!

Aston Villa walikua wababe kwetu, Crystal Palace waliyadondosha machozi ya Luis Suarez, Chelsea wakamfanya Gerrard adhalilike.

Sitosahau tulivyochapwa na Stoke City goli sita tena katika sendoff ya Steven Gerrard. Yaani mechi ya kumuaga Legend wetu tukachapwa Sita. Fedheha hizi!

Sasa tunacheka, furaha imerudi mahala pake na wala hatuchekwi tena, Dunia nzima inamsifu Mfalme, wote wanaimba mapambio ya kuusifu ubora wa Mfalme mpya.

Tazama twitt ya Mwana FA huko Twitter, amenyanyua mikono kusalimu amri, kumbuka huyu ni Manchester United damu. Msemaji wa Simba na Shabiki wa kutupwa wa Manchester United, Haji Manara amerusha taulo akikiri ubora wa Mfalme.

Nani ambaye hataki kukubali ubora wetu? Anyooshe mkono tu hata ajifanye tu anajikuna.

Misimu minne ya mafanikio makubwa chini ya Jurgen Klopp. Alituahidi, amefanya na leo kila mmoja anasifu mafanikio yetu.

Maisha yangekuaje bila Klopp katika viunga vya Merseyside? Press Conference yake ile Oktoba 12, 2015 wakati akitambulishwa kuwa Kocha mpya wa Liverpool bado inazunguka kichwani mwangu.

Aliahidi kuwa atleast baada ya miaka minne basi atakua ameleta ubingwa Anfield, akaongeza asipotupa ubingwa basi ataenda zake kufundisha soka Uswis.

Misimu mitatu ya kwanza ilitosha kutushtua na kutueleza ni kocha wa aina gani. Tulitinga fainali tatu tofauti, Ligi ya Mabingwa vs Real Madrid kule Ukraine, Europa dhidi ya Seville na Kombe la Ligi vs Man City. Zote tulipoteza, kejeli zikazidi.

Tazama sasa ndani ya kipindi cha miezi 12 Liverpool imetwaa mataji makubwa manne. Ndani ya msimu mmoja huu wa 2019/20 tumetwaa mataji matatu makubwa. Ligi Kuu, Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu. Heshima ilioje.

Nimepata bahati ya kumsoma Bill Shankly ambaye anatambulika kama Baba wa Liverpool na binadamu mwenye heshima nyingi sana Anfield.

Spirit, Falsafa na Identity tuliyonayo leo imetokea kichwani kwake. Ninamtunuku nyota nyingi sana.

Bob Paisley OBE ndie Kocha mwenye mataji mengi kuliko wote kwenye historia ya Liverpool. Makombe zaidi ya 20.

Yeye, Zinedine Zidane na Carlo Ancellot ndio makocha ambao wametwaa mara tatu taji la UEFA. OBE amefanya hivyo mara tatu akiwa Anfield. Heshima yake ni kubwa sana.

Jurgen Kaiser Klopp; Tuseme nini kuhusu huyu bwana. Alitukuta tukiwa walalahoi haswa. Tulikataliwa na makocha hadi wachezaji. Usisahau Karim Benzema alivyowahi kutupiga chini akisema sisi siyo timu ya hadhi yake.

Jurgen Klopp alitubadilisha kutoka kuwa wenye mashaka kuwa wenye imani. Alitukanwa, akasimangwa, akabezwa (mimi nikiwemo) lakini leo ametusimamisha juu ya mnara wa 'Babeli' na wala hatujapata ububu.😊

Tumetwaa taji la sita la Ligi ya Mabingwa. Tumetwaa Super Cup. Zaidi ya yote tumebeba Kombe la Klabu bingwa Dunia ambalo hatujawahi kubeba toka Liverpool ianzishwe.

Leo hii tumetwaa Taji la Ligi ya England. Hii ni baada ya miaka 30, miaka 30 ya kunyanyaswa, kutukanwa na kuchekwa.

Jurgen ametupandisha juu ya Mlima Kilimanjaro na kila mmoja anaimba mapambio ya kuisifu Liverpool. Mapambio ya kumsifu Mfalme mpya mjini.

Waliosema Ligi ifutwe kwa sababu ya Corona sasa wameinamisha vichwa, Tulisema msimu huu tutahakikisha Chizi anakimbia Jalala.

Labda niwaulize ndugu zangu wa Manchester United na Arsenal wanawezaje kukaa kitambo kirefu hiko bila kuchukua Ligi Kuu? Sisi wenzao mara ya mwisho kubeba ni leo tu.

Na baada ya yote hayo mimii binafsi. Mimi hapa, kwa kutwaa Taji hili la Ligi ninamueka Klopp daraja la juu, juu zaidi ya Shankly na OBE.

0683 015145


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...