Benki ya Exim imezindua kampeni yake mpya inayolenga kuhamasisha wateja wa benki hiyo kutumia zaidi huduma za kiditali ili kurahisha upatikanaji wa huduma zinazotolewa na benki hiyo sambamba na kuokoa muda ambao wangeutumia kufuata huduma hizo kwenye matawi ya benki hiyo.
Kampeni hiyo imekuja kipindi ambacho jamii inapitia mabadiliko kuelekea huduma za kidigitali hususani katika huduma za kifedha na manunuzi, hali iliyochochewa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa virus vya Corona (COVID 19).
Ikifahamika kwa jina ‘Maliza Kirahisi Kidigitali’, kampeni hiyo itadumu katika kipindi chote cha mwaka kilichobaki ambapo itahamasisha wateja wa benki kufanya mihamala ya kibenki muda wowote na mahali popote kwa kutumia simu zao pamoja na njia za kimtandao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni Mkuu wa huduma ya rejareja wa benki ya Exim, Andrew Lyimo alisema: "Kampeni ya ‘Maliza Kirahisi Kidigitali’ inakusudia kubadilisha tabia ya watumiaji wa huduma zetu yaani wateja wetu na zaidi pia inalenga kuongeza kasi ya mabadiliko ya nchi kutoka kwenye kufanya mihamala ya pesa kwenda kwenye mihamala ya kidijitali hususani wakati wa janga hili la Corona, ''
"Hivyo basi kampeni hii imekuja wakati muafaka kwa maana ya kipindi ambacho taifa linaelekea kwenye mabadiliko ya kihuduma za kifedha ili kuepuka misongamano ya watu kwasababu za kiafya na wakati huohuo tukirahisisha utoaji wa huduma zetu wateja pamoja na kuongeza usalama wa fedha zao,’’ alisema.
Zaidi ya hayo, Bwana Lyimo alisisitiza: "Ili kufanya huduma za kibenki ziwe nzuri zaidi na rahisi kwa wateja, Exim benki tunazo chaguzi kadhaa ikiwemo kutumia huduma ya mobile bank inayohusisha matumizi ya simu za mkononi au kwa njia ya USSD, kutumia kadi zetu za benki, mtandao wetu wa POS na pia kutumia huduma za mtandaoni kupitia wavuti au programu (App) ambazo zinawawezesha wateja wetu kupata huduma muhimu za kifedha muda wote''.
"Kupitia huduma hizi wateja wanaweza kufikia akaunti zao, kuangalia salio au kufanya mihamala ya kibenki kwa njia ya mtandao wakiwa majumbani mwao, vyuoni, ofisini, sehemu za biashara au mahali popote na hivyo kuokoa muda wao ili wautumie kutimiza majukumu yao mengine,’’ alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bw Stanley Kafu alisema kampeni hiyo ya ‘Maliza Kirahisi Kidigitali’ imekuja mwaka mmoja tangu benki hiyo izindue kampeni maalum iliyolenga kuhamasisha wateja wake kuhusiana na matumizi ya mtiririko wa huduma maalumu za kiusalama kwenye masuala ya fedha zinazotolewa na benki hiyo.
Kupitia mtoririko huo wateja wa benki hiyo wanapata huduma mbalimbali ikiwemo huduma ya usafirishaji wa fedha kwa usalama (Cash-In-Transit service), huduma ya kiusalama ya malipo (Host to host services), huduma za kisasa za hundi (Corporate Cheque Capture service) pamoja na huduma ya kuweka (deposit) pesa kwenye akaunti ya benki hiyo wakati wowote kwa kutumia mashine ya kuwekea fedha (Cash Deposit Machines services).
"Ujumbe tunaotaka kutuma kwa wateja wetu kupitia kampeni hii mpya ya 'Maliza Kirahisi Kidigitali' pamoja na jitihada nyingine zote ambazo Benki ya Exim tumekuwa tukizifanya kwa ajili yao ni kwamba tuko hapa kuwasaidia ... Exim kazini leo kwa ajili ya kesho’’ '' alihitimisha.
Mkuu wa huduma ya rejareja wa benki ya Exim, Andrew Lyimo ( Katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni mpya ya benki hiyo ijulikanayo kwa jina la "Maliza Kirahisi Kidigitali' inayolenga kuhamasisha wateja wa benki hiyo kutumia zaidi huduma za kiditali ili kurahisha upatikanaji wa huduma zinazotolewa na benki hiyo. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo Bw Stanley Kafu (Kushoto) na Mkuu wa Idara ya Kidigitali na huduma Mbadala wa benki hiyo Bw Silas Matoi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...