Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab Kawawa amewasihi wafanyabiashara kutumia bandari ya Bagamoyo kuingiza bidhaa zao na kusafirisha bidhaa zinazotoka nje ya Bagamoyo.

Mhe. Zainab ameyasema hayo alipofanya mkutano maalum na wafanyabiashara wa Bagamoyo wanaotumia bandari ndogo ya Bagamoyo baada ya wafanya biashara hao kuacha kutumia bandari hiyo wakidai huduma zisizoridhisha toka kwa uongozi wa mamlaka ya bandari ya Bagamoyo.

Akizungumza kwa niaba ya Wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Bagamoyo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao Bw. Shabani Khamsini Almaarufu “Chavurugu” amesema, Uongozi wa Mamlaka ya bandari ya Bagamoyo umekuwa ni kero kwa wafanyabiashara kwani baadhi ya Maofisa Bandari wamekuwa na lugha chafu za matusi kwa wafanyabiashara hao, kutoa risiti zenye kiwango tofauti na pesa wanazolipia huduma, na wakati mwingine kutishia kuwapiga wanapofika Ofisi za bandari kupata ufafanuzi na huduma, Amesema Mwenyekiti huyo.

Baada ya kupokea kero na malalamiko ya wafanyabiashara hao Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo amesema ni kinyume cha kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya Utumishi wa umma kwa Mtumishi kutoa lugha chafu kwa wateja anaowahudumia, kuwapiga na kuhujumu mapato ya Serikali kwa kutoa risiti inayotofautiana na kiasi cha fedha alichopokea, hivyo akawataka wafanyabiashara hao kuhakikisha tuhuma walizowasilisha kwake zina ukweli kwani mara baada ya mkutano huo kamati ya Ulinzi na usalama itaanza uchunguzi wa tuhuma hizo mara moja ili sheria ichukue mkondo wake kwa Maofisa wote wanaohusika na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa umma, maana vitendo hivyo vimeiingizia Serikali hasara kubwa baada ya wafanya biashara hao kuisusa bandari ya Bagamoyo na kuacha kabisa kuingiza bidhaa kupitia bandari ya Bagamoyo.

“Naombeni rudini itumieni bandari ya Bagamoyo, ni mali yenu, ni kwa ajili yenu, chonde chonde rudini mtumie bandari yenu kibiashara, nipo pamoja nanyi kusimamia haki zenu na maslahi yenu na nawaahidi kufuatilia na kumaliza kero na malalamiko yenu yote na wote wanaohusika katika kuwakwamisha ntahakikisha wanachukuliwa hatua stahiki,” Amesema Mhe. Zainab Kawawa.

Aidha Mhe. Zainab Kawawa ametumia mkutano huo kumwagiza Meneja Bandari ya Bagamoyo Bw. Witharo Jared Witharo kuacha mara moja vitendo anavyoshutumiwa navyo vya ukiukwaji wa maadili, kanuni, sheria na taratibu za Utumishi wa umma na ahakikishe anatoa huduma bora kwa wafanya biashara hao ili kurejesha hadhi ya bandari hiyo kama ilivyokuwa mwanzo.

Bandari ya Bagamoyo imepata mtikisiko mkubwa wa kimapato baada ya mapato yanayotokana na bandari kushuka kutoka Shilingi Bilioni 03 Mwezi Novemba Mwaka 2019 hadi kufikia Shilingi Milioni 293.8 Mwezi Mei mwaka huu baada ya wafanyabiashara wanaotumia bandari hiyo kususia kuingiza mizigo kupitia bandari ya Bagamoyo wakilalamikia usumbufu mkubwa na huduma mbovu zilizokuwa zikitolewa kwenye bandari hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Zainab Kawawa alipokuwa akizungumza na Wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Bagamoyo kuingiza bidhaa zao na kusafirisha bidhaa zinazotoka nje ya Bagamoyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...