Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

ANAFAHAMIKA kwa jina la Edward Saidi 'Tingatinga' mchoraji wa kitanzania ambaye pia anaelezwa kuwa ni mwanzilishi wa mtindo wa uchoraji maarufu kama Tingatinga, ambao umekuwa kivutio kwa watalii na umekuwa ukifanywa katika nchi za Tanzania, Kenya na baadhi ya maeneo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Tingatinga ni sanaa ya ufundi inayojumuisha uchoraji, upakaji rangi, ufinyanzi, uchongaji na utengenezaji wa mapambo ya asili na utamaduni.

Tingatinga alizaliwa mwaka 1932 katika kijiji cha Namocheli, Mindu karibu na kijiji cha Nakapanya mkoani Tunduru, Kusini mwa Tanzania karibu na mpaka wa nchi ya Msumbiji.

Alifahamu hakukuwa na wajuuzi wa kazi hiyo katika eneo alilokuwa akiishi akaamua kujitosa na kuifanya na aliifurahia.

Ndugu wa Tingatinga bado wanaishi, upande wa mama yake wanaishi katika vijiji vya Nakapanya, Mindu na Mtonya na ndugu wa baba zake wanaishi Ngapa kilomita 20 kutoka Kaskazini mwa Nakapanya.

Edward Tingatinga alizaliwa kwenye familia ya kimaskini, mama yake alikuwa Agnes Binti Ntembo kabila la mmakua na baba yake Saidi Tingatinga aliyekuwa Mngindo na Tingatinga alipewa majina ya dini zote kutokana na mfumo wa matrilinia unaofuatwa na kabila la wamakua, Tingatinga alilelewa zaidi na upande wa mama na hiyo ni baada ya mahusiano ya wazazi wake kuvunjika.

Mwaka 1950 Edward alimwacha mama yake na kwenda kufanya kazi katika mashamba ya mkonge Mkoani Tanga, baadaye akaalikwa kwenda Dar es Salaam na mjomba wake Salum Mussa Mkaoya aliyekuwa anafanya kazi ya upishi kwa ofisa ya kiingereza, na alipofika akaajiriwa kama mtunza bustani.

Wakati huohuo alianza kujifunza Muziki na mwaka 1968 uchoraji, alichora kwa kutumia  malighafi za bei rahisi ikiwemo rangi ya kung'arisha baiskeli na mabaki ya vigae na malighafi za ujenzi.

Michoro yake ilikua halisi na inayoakisi maeneo ya Afrika hasa Tanzania na hasa alichora wanyamapori na maeneo ya vivutio yanayopatikana Tanzania.

Mwaka 1970 alimuoa Agatha Mataka mmakonde kutoka Msumbiji na wakati huo michoro yake ya Tingatinga ilikua inafahamika sana kwa wakazi wa Ulaya nchini Tanzania na watalii hapo ndipo akaanza kutumia muda wake wote katika sanaa hiyo.

Baadaye akaanzisha kundi 'Tingatinga Art Co-operative Society' na moja wa wanakikundi hao ni pamoja na January Linda, Adeus Mandu, Ajaba AbdallahMtalia, Casper Tedo, Simon Mptata na Omari Amonde hilo ndilo lilikuwa kundi la kwanza la wanafunzi waliojifunza sanaa ya Tingatinga, na kati yao Omari Amonde ambaye ni mpwa wa Omari ndiye anayeishi.

Maisha ya Edward Saidi Tingatinga yalikatishwa mwaka 1972 kwa bahati mbaya, polisi walimfyatulia risasi kwa kudhani kuwa ni mhalifu na alizikwa katika makaburi ya Msasani Dar es Salaam.

Shule za Tingatinga bado zinaishi na zimekua na kufanyiwa marekebisho kwa kiasi kikubwa na kuwa na wafuasi wengi na vivutio kwa watalii katika nchi za Tanzania, Kenya na sehemu kubwa ya Mashariki mwa Afrika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...