Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza baada ya kuzindua Shule ya Sekondari ya Kata ya Nondwa wilayani Bahi, Dodoma.
Muonekano wa Shule ya Sekondari ya Nondwa iliyopo wilayani Bahi mkoani Dodoma ambayo imezinduliwa na Waziri Selemani Jafo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akikagua madarasa ya shule ya Sekondari Nondwa baada ya kuizindua.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kusimamisha mchakato wa uuzwaji wa eneo la Kijiji cha Magole katika halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ili kubaini uhalali wa uuzwaji wake. Ameagiza lifanyike kwa kushirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Waziri Jafo ametoa agizo hilo wilayani Bahi wakati akizindua Shule ya sekondari ya Kata ya Nondwa iliyojengwa na halmashauri hiyo kwa kutumia mapato yake ya ndani ambapo amesema eneo hilo lina ukubwa wa hekari 200 na linauzwa kwa raia wa kigeni
Amesema haiwezekani mchakato ufanyike bila ya kushirikisha wananchi wa Kijiji husika na kutaka uchunguzi huo uangalie uhalali wa muuzaji na mnunuaji pia kujua dhamira waliyokuwa nayo.
"Timu hiyo iangalie kulikuwa na uhalali gani wa kuuza mali hiyo,na mnunuaji pia aangaliwe kama hakuna harufu ya rushwa,haiwezekani eneo hilo liuzwe bila ya wananchi kujua tena kwa raia wa kigeni,huyu aliyependekeza kuuzwa alishawishiwa na nini, na tangu lini mgeni akamiliki ardhi nchini,?" Amehoji Jafo.
Amesema Baraza la madiwani katika kikao Chao Cha mwisho lilipitisha uamuzi wa kuuzwa eneo la Kijiji lenye hekari 200 bila ya kuwashirikisha wananchi pamoja na kwamba mkuu wa Mkoa aliwaandikia barua ya Kuzuia wasifanye hivyo.
"Huu ni udhaifu wa hali ya juu wa madiwani ambao katika kikao Chao Cha mwisho Cha kuvunjwa Baraza lao ndio waliidhinisha hili," Amesema.
Jafo amesema Hilo eneo ambalo limeuzwa kwa mchina kulikuwa linatumika na wachina kutekeleza miradi ya miundombinu majengo ambayo wangeweza kuyabadili kuwa kituo Cha afya au zahanati.
"Yaani sijui waliuza Ili wapate hela za kuwalipa madiwani viinua mgongo vyao na madeni mengine,hii ni tabia mbaya,nimechukizwa Sana,"Amesisitiza Jafo.
Ameipongeza halmashauri ya Bahi kwa kuwalipa madiwani viinua mgongo vyao vyao na kutumia asilimia 40 ya mapato yao ya ndani katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Dk Fatma Mganga amesema mashine za ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (Pos) zimewasaidia kupongeza ukusanyaji wa mapato ambapo hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu walifikisha asilimia 86 ya ukusanyaji.
"Wewe mwenyewe Mhe Waziri umetuelekeza tuhakikishe mapato tunayokusanya kiasi kirudi kwa wananchi na tumefanya hivyo,na mashine ya Pos ndio zimekuwa msaada mkubwa kwetu,hapa madiwani wetu wamestaafu wakiwa hawana mawazo,pesa zao zote tumeweza kuwalipa," Amesema Mkurugenzi huyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...