JESHI la Polisi mkoani Arusha, litaanza ujenzi wa kituo kidogo cha polisi katika kata ya Kisongo wilayani Arumeru mkoani hapa baada ya jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro kuwapa eneo la ujenzi huo ili kuondoa kero kwa wananchi.

Akikabidhi eneo hilo kwa kuanza kupanda miti, Mkuu wa wilaya hiyo Muro, alisema kituo hicho kitasaidia kuimarisha ulinzi kwa jamii katika eneo hilo baada ya muda mrefu kuwepo matukio ya uhalifu.

Alisema eneo hilo ambalo linakuwa kwa kasi kumekuwepo na matukio ya watu kuporwa mali zao ikiwemo vitendo vya wanawake kubakwa.

"Tumeamua kutoa eneo hili haraka ili Polisi wajenge kituo cha polisi ambacho kitasaidia kuimarisha ulinzi pamoja na kutoa huduma kwa wananchi ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu," alisema Muro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye amekuwa karibu na wananchi katika kutatua na kuyapa majawabu matatizo mbalimbali wanayokabiliana nayo, pamoja na kukabidhi eneo hilo, pia alipanda miti ya kivuli ili kulinda mazingira ya eneo litakalojengwa kituo hicho.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha (SACP)  Jonathan Shana alisema mipango ya kujenga kituo hicho kwa haraka ipo tayari baada ya kumpata mfadhili.

SACP Shana alimhakikishia mkuu huyo wa wilaya kwamba tayari wamepata mfadhili wa kusaidia ujenzi huo wa kituo ili ukamilike kwa haraka.

"Nakuhakikishia mkuu wa Wilaya, tayari tumepata mfadhili kutoka shirika la Umoja wa Mataifa Divisheni ya Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia makosa ya kesi za mauaji ya Kimbari, "alisema SACP Shana.

Shana alisema ujenzi wa kituo hicho ambacho pia kitahudumia wananchi wa Matevesi, utaanza wakati wowote wiki hii.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa shirika hilo la umoja wa Mataifa, Tevita Colati alisema wametoa mchango wa kujenga kituo hicho kama sehemu ya kutekeleza mpango wa mahusiano na jamii inayozunguka Mahakama hiyo.

"Masuala ya ulinzi na amani ni kipaumbele cha Dunia na Afrika, hivyo tumetoa mchango kutekeleza mpango wa kusaidia jamii inayotuzunguka katika Mahakama ya kushughulikia mauaji ya Kimbari, "alisema Colati.

Kukamilika kwa kituo hicho kitahudumia wananchi wapatao 350,345 wa kata za Kisongo na Matevesi wilayani Arumeru.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro akipanda Mti baada ya kukabidhiwa Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Jonathan Shana eneo litakalojenga kituo cha polisi

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Divisheni ya Mahakama ya kushughulikia mauaji ya Kimbari,Tevita Colati akipanda Mti eneo hilo.
 Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro (Kulia)  Akizungumza na wadau watakaofanikisha ujenzi huo kushoto ni mwakilishi wa shirika hilo Colati na katikati ni Mkurugenzi wa kampuni ya Ulinzi ya Bond Security Frank Kessy
 Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro akifafanua jambo
 Picha ya pamoja

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...