Na Said Mwishehe, Michuzi TV
 
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kupitia kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo Mashimba Ndaki amesema kwa miaka mitano sasa kamati hiyo imekuwa ikiwasilisha maombi serikalini ya kuondoa ushuru wa bidhaa kwa chupa zinazotumika kwa ajili ya kufungashia mvinyo unazalishwa nchini.

Akizungumza leo Juni 15,2020 Bungeni Mjini Dodoma Ndaki amesema kwa sasa chupa zinazoingizwa nchini zinatozwa ushuru wa bidhaa kwa asilimia 25, pamoja na tozo nyingine za serikali na hivyo kusababisha mvinyo ambao unaozalishwa nchini kuwa ghali kuliko ule unaozalishwa nje. 

"Wadau wameitaarifu kamati kwamba mataifa mawili yaliyoko katika jumuiya ya Afrika Mashariki yameanza kulima zao la zabibu. Jambo la msingi la kujiuliza hivi kwa hatua hizi tunalitakia mema zao hili ambalo linalimwa Dodoma katika Mji mkuu wa Tanzania,"ameeleza.

Pia amesema kamati hiyo imeishauri Serikali kufanya mabadiliko katika Ibara ya 31 ya muswada kipengele (e) ambacho kinaruhusu mapato yatakayotumika katika mapambano ya COVID - 19 kuondolewa wakati wa ukokotoaji wa mapato ya kampuni.

Amesema katika ibara hiyo Kamati inapendekeza kuongeza aya mpya ya (f) ambayo itatoa mwanya wachangiaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mashine na vifaa vya kupima usalama wa damu ambazo zimekuwa changamoto.

Ndaki amefafanua kuwa lengo la mapendekezo hayo ni kuvutia sekta binafsi kuchangia katika ununuzi wa mashine hizo ambazo ni muhimu kwa kuhakikisha kunakuwa na damu salama.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na kufanya mabadiliko katika Jedwali la Kwanza la Sheria hiyo kwa kupanua wigo wa kiwango cha mapato ambacho hakitozwi kodi kwa sababu limekuwa pendekezo la Kamati kwa muda mrefu na viwango hivyo vilikuwa vimepitwa na wakati.

Wakati huo huo,Dk.Mpango ametumia Bunge hilo kuelezea kwamba baadhi ya hatua zilizobainishwa katika Hotuba ya Bajeti zitatekelezwa na mawaziri husika kupitia Kanuni na Matangazo ya Serikali kwa mujibu wa matakwa ya sheria husika.

Dk.Mpango ametaja baadhi ya hatua hizo ni kupunguza tozo inayotozwa na Bodi ya Sukari, kupunguza ada zinazotozwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kurekebisha tozo kwenye sekta ya mifugo na uvuvi na kupunguza ada ya mabango ya matangazo kwenye magari ya wazalishaji wa bidhaa yanayotumika kusafirisha bidhaa kutoka viwandani kwenda kwa wasambazaji.

Hatua nyingine ni kupunguza tozo ya elimu kwa umma inayotolewa na OSHA na kurekebisha hati iliyoanzisha TAWA ili kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukusanya maduhuli. Aidha, amesema sehemu ya 14 inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sura 148.

Amefafanua kuwa marekebisho hayo yanahusu kurekebisha kifungu cha 59(3)(e) ili kuruhusu utozaji wa kodi ya ongezeko la thamani kwa asilimia sifuri kwenye huduma zinazotolewa kwenye mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia nchini kwa kipindi cha ziada ambacho Kamishna wa Forodha ataruhusu.

"Lengo ni kuwapa unafuu waagizaji wa mizigo kupitia bandari pale ambapo mizigo hiyo inachelewa kuondoka nchini kwa sababu mbalimbali,"amesema.
Pia amezungumzia kurekebisha kifungu 68(3) ili kufuta kifungu kidogo cha aya (d), lengo ni kuwawezesha wauzaji wa bidhaa ghafi nje ya nchi kuendelea kujirudishia kodi ya ongezeko la thamani iliyolipwa kwenye gharama za huduma au bidhaa katika shughuli hizo, ili bidhaa hizo ziweze kushindana katika masoko ya nje.

"Hatua hiyo itawawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo na kuvutia wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli zao za kilimo kama ukame na mafuriko,"amesema Dk.Mpango.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...