Charles James, Michuzi TV

NGOMA inarudi! Kipute kinalia, mbugi linarudi mwanangu, vita vinarejea, mtanange unaputwa ili uanze kupigwa. Furaha yenye mateso tuliyokua tumeimiss kitambo sasa inakuja kwenye macho yetu.

Ipo hivi; Baada ya miezi miwili ya Ligi mbalimbali za Soka duniani kusimamishwa kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid19 'Corona' sasa filimbi zinapulizwa kuashiria ligi zinarejea.

Ligi zinarudi baada ya Serikali za Nchi mbalimbali kuruhusu michezo kuanza kutokana na kuridhishwa kwake na kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo kwenye maeneo yao.

Nchini kwetu serikali kupitia kwa Rais Dk John Magufuli imeruhusu ligi kuanza kuchezwa ila ikisisitiza hatua za tahadhari kuchukuliwa. Na itarejea Juni 17 mwaka huu.

Ujerumani ngoma imeshaanza kupigwa bila mashabiki. England Ligi pendwa na yenye mashabiki wengi inarudi Juni 13 huku wataalamu wakishauri tahadhari kuchukuliwa.

Vipimo vimechukuliwa mara kadhaa kwa wachezaji wa timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu England kubaini idadi ya maambukizi na vipimo vya mwisho vimethibitisha kutokua na maambukizi mapya.

Tuachane na Corona. Maana sisi hapa nchini tulishakubaliana nayo iamue mambo mawili, moja iamue kuondoka nje ya mipaka yetu au kama itakaa basi ikae kwa kutulia na iwe na heshima.

Hayo siyo maombi bali ni maelekezo ambayo tumeipa Corona. Iamue kuondoka au ikikaa hapa ikae kwa heshima kubwa.

Nisamehe kwa kuchepuka na kuongelea Corona, turudi njia kuu. Kipenzi chetu kinarudi. EPL is back, EPL inakuja tena. Maisha yetu tuliyoyazoea yamerudi.

Mbugi Jumamosi na Jumapili, Ngoma Jumatatu Usiku. Vijiwe vya betting nako sasa patawaka ile mbaya. Biashara ya vinywaji itafurika kwa wingi wa wateja watakaojazana kucheki mechi za Ligi Kuu.

Sipati picha namna magazeti yatakavyouza kwa stori za michezo. Zile tambo za mashabiki kwenye magroup ya WhatsApp zitawaka sana. Usipime Man!.

Sasa sikiliza mashabiki wa Liverpool wanarudi kwenye mbio wakiwa kileleni mwa msimamo na pointi zao 82 baada ya michezo 29. Man City anaemfutia yupo mita nyingi kutoka walipo vijana wa Jurgen Klopp.

Klopp na vijana wake wanahitaji alama sita tu kutangazwa kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu England baada ya kitambo cha miaka 30.

Furaha yao ya kuchukua taji la Ligi ilishaanza kutibuliwa na Corona. Washukuru Mungu watu wameifukuza Corona kwa kupiga Nyungu. Na sasa furaha yao inakaribia kutimia.

Ndugu zangu wa Chelsea msijisahaulishe na usajili wa Timo Werner mnarudi kwenye Ligi mkiwa nafasi ya nne na alama zenu 51. Hamna uhakika wa kubeba taji la EPL kwa msimu wa tatu mfululizo.

Ebwana ee, hakuna jambo natamani kuliona ligi inaporejea kama combination ya mdenguaji Paul Labile Pogba na mchawi wa Kireno, Bruno Fernandes.

Ngoja nikukumbushe kabla ya Ligi kusimama Pogba aliwadengulia sana Manchester United, mara ooh nataka kurudi Juventus, mara ooh anataka kwenda Real Madrid kwa Zizzou.

Ed Wood akazama sokoni wakati wa dirisha dogo, akamleta Bruno. Moto aliouwasha Mchawi huyo wa Kireno ni kama umemshtua Labile hivi.

Mara paap stori za kusepa zikapotea. Jamaa amerudi mazoezini kwa fujo na nasikia wanaelewana balaa. Sasa pata picha hapa Matic au McTominay mbele kidogo anacheza Pogba na Bruno. Wapinzani mtaomba Corona 'irudi'.

Kama kuna watu wana hasira na Ligi kurudi basi ni Arsenal, walishaanza kunenepa maskini ya Mungu. Wewe unadhani wakianza kushuhudia vipigo vya timu yao si watakondeana tena?

Mashabiki wa Arsenal ni miongoni mwa waliokua wakiomba Ligi zifutwe ili mambo yaanze upya. Kurejea tena kumalizia ngwe iliyobaki kwao ni mateso.

Furaha nyingine niliyonayo ni kumuangalia Mtanzania mwenzetu, Mbwana Samatta Poppa akiwasumbua mabeki wa Kizungu katika michezo takribani tisa ya Ligi iliyobaki.

Poppa anashikilia rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England. Na ni juzi tu mashabiki wa Klabu yake ya zamani ya KRC Genk wamemtaja katika kikosi chao cha muda wote.

Mbio za ufungaji bora je? Hujazimiss? Pierre Aubameyang, Mommo Salah na mtasha Jamie Vardy nani ataibuka na kiatu cha dhahabu?

Kwa wasiojua Salah anakitafuta kwa mara ya tatu na Pierre kwa mara ya pili mfulululizo. Kurejea kwa Ligi kutatupa majibu ya nani ni nani.

Hivi Tottenham ya Jose Mourinho ndiyo ile ile ya Mouricio Pochettino iliyocheza fainali ya UEFA na Liverpool? Wako nafasi ya nane na alama zao 41. Kucheza Ligi ya Mabingwa ndio wasahau tu. Chao hawana.

Niwashauri tu jiandaeni kisaikolojia, hiki ndio kipindi ambacho watu huongea wenyewe barabarani. Hasira zisizokwisha na visirani kila kukicha.

Watoto wawe makini na Baba zao watajikuta wanapigwa kisa Arsenal imefungwa. Akina Dada kuweni makini na wapenzi wenu mnaeza kushangaa mmeachika tu kwa sababu Liverpool imefungwa na Everton.

Hizi ndio zile nyakati za watu kukaa Bar hadi saa nane za usiku na michepuko wakisingizia wanaangalia mpira.. Wenye waume zenu tafuteni ratiba mkae nazo msije kusema hatukuwapa angalizo.

0683015145

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...