Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha
Songwe, Bw. Pius Kazeze, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi Elias
Kwandikwa, wakati Naibu Waziri huyo alipokuwa akikagua hatua za
uboreshaji wa kiwanja hicho, mkoani Mbeya

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akitoka kukagua eneo linalongezwa kwa ajili ya usalama wa
ndege zinazoruka na kutua katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani
Mbeya

Muonekano wa jengo la abiria la
sasa linalotumika, jengo jipya la abiria linalojengwa ambalo litakuwa na
uwezo wa kuchukua abiria laki tano kwa mwaka na barabara ya zege ya
kutua na kuruka ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani Mbeya.
Uboreshaji wa kiwanja hicho unagharimu bilioni 14.7

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, akikagua uimara wa barabara ya zege iliyopo katika maegesho
ya ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe, mkoani Mbeya.

Kazi za uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe zikiendelea, mkoani Mbeya.
*****************************************
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias
Kwandikwa, amemtaka mkandarasi China – Geo Engineering Corporation
kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa katika uboreshaji wa Kiwanja
cha Ndege cha Songwe.
Aidha, amemuagiza kuongeza vifaa
muhimu vyote katika eneo la kazi na wataalamu wa kutosha ili waweze
kufanikisha utendaji kazi usiku na mchana kwa muda waliopangiwa wa miezi
nane.
Kwandikwa alisema hayo akiwa
mkoani Mbeya, alipofanya ziara ya kukagua hatua iliyofikiwa ya mradi huo
utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 14.7 ambapo fedha hizo
zinatolewa na Serikali kwa asilimia 100.
“Nimekuja kuona maendeleo ya
uwanja huu na ninafahamu kuwa hapa kumekuwa na changamoto ya mvua na
kusababisha maeneo mengi ya mradi kukwama sasa mvua imepungua, naagiza
kazi iendelee kwa kasi zaidi”, amesema Naibu Waziri huyo.
Alifafanua kuwa lengo la Serikali
ni kuufanya uwanja huo kuwa ni wa kimataifa na wenye sifa zote za
kuruhusu ndege kubwa kuruka na kutua na kutumika usiku na mchana.
“Huu uwanja tunahitaji utumike
kimataifa kama viwanja vingine na ndio maana maboresho tunayofanya
yanahusisha na utoaji wa barabara ya zamani ya kuruka na kutua ndege
yote iliyokuwepo uwanjani hapo na kuweka tabaka jipya la lami ya zege
imara ili ndege kubwa zitue bila tatizo lolote, taa za usiku na uzio”,
amesisitiza Naibu Waziri huyo.
Kwandikwa alisema Serikali
inategemea kuibua shughuli nyingi za kimaendeleo katika Mkoa wa Mbeya
kupitia kiwanja hicho kwa kuwa mkoa unavutia kuwa na vitu vingi vya
kufanya hususani biashara.
Awali akitoa taarifa ya mradi
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Mbeya, Mhandisi
Eliazary Rweikiza, alisema kuwa kazi ya usimamizi wa uboreshaji wa
kiwanja hicho unasimamiwa na TECU na kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa
tabaka jipya la lami, uzio, uwekaji taa za kuongezea ndege na ujenzi wa
eneo la usalama mwisho na mwanzo wa uwanja.
Uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege
cha Songwe ni moja ya mkakati wa Serikali wa ukarabati na upanuzi wa
viwanja vya ndege 11 nchini vikiwemo Viwanja vya Songea, Shinyanga,
Mtwara, Kigoma, Sumbawanga, Tabora, Iringa na Musoma ambavyo vipo katika
hatua mbalimbali za utekelezaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...