Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Njombe-Moronga - Makete (km 107. 4) kwa kiwango cha lami, mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christpher Ole Sendeka na Katibu wa Siasa na Uenezi CCM mkoa wa Njombe, Bw. Erasto Ngole, wakikagua ujenzi wa barabara ya Moronga-Makete yenye urefu wa KM 53.5 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Njombe-Moronga yenye urefu wa KM 53.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Mradi wa ujenzi huo utakamilika mwezi Oktoba, 2020 na utagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 107.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Moronga-Makete yenye urefu wa KM 53.5 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Njombe. Mradi wa ujenzi huo utakamilika mwezi Aprili, 2021 na utagharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 110.

SERIKALI imetoa agizo kwa wakandarasi wote nchini kutosimamisha ujenzi wa barabara na madaraja yanayoendelea kujengwa kwa kuwa makandarasi hao wameshalipwa madai yao na Serikali.

Hayo yamesemwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati wa ziara yake mkoani Njombe ya kukagua utekelezaji wa mradi wa barabara ya Njombe - Makete (km 107.4), inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo sehemu ya mradi wa Njombe - Moronga (km 53.9) umefikia asilimia 62 na Moronga - Makete (km 53.5) umefikia asilimia 45 na kusisitiza kuwa hakuna mkandarasi nchii hii anayeidai Serikali.

"Ujenzi wa mradi huu unatekelezwa na fedha za wananchi na nyie wakandarasi tumewalipa fedha zenu, tunachohitaji ni barabara kwani wananchi wanaisubiri kwa hamu", amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Kwandikwa ameeleza kuwa mara baada ya barabara hiyo kukamilika Serikali imeshatenga fedha katika mwaka huu wa 2020/21 kujenga kilometa 93 kutoka Makete hadi Isyonje kwa kiwango cha lami.

"Lengo la Serikali ni kuhakikisha mikoa yote nchini inaunganishwa kwa barabara za lami hivyo niwahakikishie wananchi wa mkoa huu kuwa sasa utaweza kufika mkoa wa Mbeya kupitia barabara hii imara na salama wakati wote ukizingatia mkoa huu una miinuko mingi", amesema Naibu Waziri huyo.

Amewataka watanzania kuweka kifua mbele kwa kuwa kodi zao sasa zinawezesha kupata miradi mingi katika miundombinu ya barabara, majini, anga na hata sekta zingine kama Afya, Elimu na Kilimo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, amesema sasa wananchi wa mkoa wake watanufaika na barabara hii kwa kuwezesha kusafirisha mazao yao ya kilimo na hasa matunda aina ya parachichi.

"Haya ni matunda ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kinachoongozwa na Kiongozi bora Mwenyekiti wetu Dkt. John Pombe Magufuli hivyo tujivunie wananchi kupata barabara hii ambayo ni historia kwa nchi yetu", amesema Mkuu wa Mkoa huyo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe Mhandisi Yusuph Mazana, amesema kuwa sehemu ya ujenzi barabara ya Njombe - Moronga utakamilika mwezi Oktoba mwaka huu na sehemu ya Moronga hadi Makete utakamilika mwezi Aprili, 2021.

Pia amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwasimamia makandarasi hao katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na viwango vya ubora.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete yenye jumla ya urefu wa KM 107.4 unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 217.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...