Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwapungia wananchi wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa
Nachingwea akiwa njiani kwenda Ruangwa kwa ziara ya kikazi, Juni 20,
2020. Wa pili kushoto ni mkewe Mary na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
mkewe Mary wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, wakati
walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa nachingwea akiwa njiani kwenda
Ruangwa kwa ziara ya kikazi Juni 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
**********************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amesema Serikali imewaagiza Makamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) nchini wahakikishe wanawakamata na kuwachukulia
hatua watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi
mkuu.
“Watu wamezoea vitendo vya
rushwa kwenye uchaguzi, Serikali tumeagiza kwa kamati za ulinzi na
usalama zishirikiane kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vya rushwa katika
uchaguzi na yeyote ambaye anajihusisha na rushwa asiachwe.”
Alitoa kauli hiyo jana jioni
(Jumamosi, Juni 20, 2020) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa
Lindi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Nachingwea akiwa
njiani kuelekea wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi.
Waziri Mkuu alisema kitendo
cha kutoa na kupokea rushwa ni kosa, hivyo viongozi hao wa TAKUKURU
nchini hawana budi kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika
kujihusisha na vitendo hivyo.
Vilevile, Waziri Mkuu
amewataka Makamanda wa TAKUKURU katika wilaya zote nchini wahakikishe
wanawakamata watu wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa wakiwemo
na wapambe ambao ndio wachochezi wa vitendo hivyo.
Waziri Mkuu alitoa maagizo
hayo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka
huu unakuwa huru na wa haki, hivyo kuwawezesha wananchi kuchagua
viongozi wanaowahitaji na si kwa msukumo wa rushwa.
Katika hotuba yake aliyoisoma
Juni 15, 2020 bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa
Bunge, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau
wengine wa uchaguzi wazingatie katiba, sheria, kanuni na miongozo
iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kuwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi
kwa ujumla waendelee kulinda amani na kuendeleza mshikamano katika
kipindi hiki na wakati wa uchaguzi Mkuu.
Mapema asubuhi jana Mheshimiwa
Majaliwa alikweda Zanzibar ambako alishiriki katika tukio la Kuvunja
Baraza la Wawakilishi liliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwenye ukumbi wa Baraza
hilo. Pia tukio hilo lilihudhuliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...