Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema imeamua kuwekeza kwenye katika uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi za Elimu ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu kwa watanzania walio wengi.
Kauli hiyo imetolewa wilayani Mpwapwa, Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo cha Ualimu Mpwapwa.
Katika ziara hiyo Prof Ndalichako amekagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika chuo hiko ambao umegharimu zaidi ya Sh Bilioni 2.8.
Baada ya ukaguzi huo Waziri Prof Ndalichako alizungumza na watumishi na wanafunzi wa chuo hiko na kuwaeleza kuwa Serikali imeamua kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwani inatambua elimu ndio suluhisho la kufikia maendeleo makubwa.
Waziri Ndalichako ametaja miundombinu inayojengwa chuoni hapo kuwa ni jengo moja la ghorofa kwa ajili ya Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bweni la ghorofa moja la walimu tarajali wa kike, bwalo la chakula na nyumba mbili za watumishi ambazo nyumba moja ina uwezo wa kuchukua familia tatu.
" Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imeamua kwa dhati kabisa kuboresha sekta ya elimu kwa sababu inatambu elimu ni nguzo muhimu katika kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, ndio maana tunazidi kuboresha miundombinu yake kuanzia elimu ya Msingi, Sekondari na hata vyuoni.
Niwaombe wanafunzi wangu msimame kidete katika kuwa mabalozi wazuri wa serikali yenu na hasa kwenye sekta ya elimu ambayo nyie wenyewe mmeshuhudia uwekezaji mkubwa tulioufanya, semeni mazuri yanayofanywa na serikali yenu, huo ndio uzalendo," Amesema Prof Ndalichako.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala, Said Mwaliego akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Jabili Shekimweri, ameishukuru Wizara kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa chuo hicho. Ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia mradi huo kwa karibu ili ukamilike kwa wakati.
Nae Mkuu wa Chuo hiko, Gerald Richard amemshukuru Rais Dk John Magufuli kwa namna alivyoifanyia maboresho makubwa sekta ya elimu huku akimpongeza Waziri Ndalichako kwa kusimamia Wizara ya Elimu kwa mafanikio makubwa toka ateuliwe na Rais Magufuli.
" Tunaishukuru Wizara kwa kutupatia fedha za ukarabati wa chuo kwani miundombinu yake ilikuwa imechakaa kutokana na kuwa ni cha muda mrefu, tunaamini ujenzi wa miundombinu unaoendelea utaongeza nafasi za udahili wa wanachuo wengine," Amesema Mkuu huyo wa Chuo.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na watumishi na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa kilichopo wilayani Mpwapwa, Dodoma alipofika kukagua maendeleo yake.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa alipofika kukagua chuo hiko na kuzungumza na wanafunzi hao.
Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa wakimsikiliza Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako alipofika kuzungumza nao.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akikagua miundombinu inayojengwa kwenye Chuo cha Ualimu Mpwapwa kilichopo wilayani Mpwapwa, Dodoma.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi w Chuo cha Ualimu Mpwapwa katika jengo la Tehama.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi w Chuo cha Ualimu Mpwapwa katika jengo la Tehama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...