SERIKALI imepeleka wataalam kwenda kuanza mchakato wa kuweka mipaka ya kuwa na Pori la Akiba (Game Reserve) la Bonde la Ziwa Natron na sehemu nyingine itakayokuwa na makazi ya watu (WMA).

Akizungumza kwa simu na mtandao huu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda, alisema serikali bado haijatangaza eneo hilo kuwa Pori la Akiba bali kinachoendelea kwa sasa ni kamati ya wataalamu kukutana na viongozi wa vijiji na watu wengine ili kukubaliana kwa pamoja.

Katibu Mkuu alitoa ufafanuzi huo baada ya kujitokeza kwa hofu kutoka kwa wananchi wanaoishi katika Bonde hilo kwamba tayari serikali imetangaza kwamba eneo hilo limepitishwa kisheria kuwa Pori la Akiba.

"Hapana sijatangaza kwamba eneo hilo limepitishwa kuwa pori la Akiba, tuliitambulisha Kamati ya Wataalamu ikiongozwa na ndugu Kauzeni kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro (Rashid Taka). Tayari wamepiga picha za juu kutazama mipaka na makazi ya watu na wamechora ramani," alisema Profesa Mkenda.

Alisema wamechora ramani kwa kushirikiana na watu wa wilaya ambayo inaonesha uwepo wa eneo la litakalokuwa pori la akiba la Ziwa Natron na sehemu ya makazi ya watu (WMA) kisha kinachoendelea kutafuta maoni ya ramani hiyo kutoka kwa wenyeviti wa vijiji ma wananchi.

"Mwenye mamlaka ya kutangaza pori la akiba ni Rais, mimi siwezi kutangaza nilichofanya ni kuunda kamati ya wataalamu..Ni work in Progress (mchakato unaendelea)," alisema Profesa Mkenda.

Ufafanuzi huo wa serikali unafuatia hofu ya wanachi anaoishi katika Bonde hilo kueleza kwamba serikali kupitia Katibu Mkuu huyo Juni 11 mwaka huu ametangaza kwamba eneo la Bonde la Ziwa Natron limekuwa pori la Akiba na wamemuomba Rais John Magufuli, kubatilisha maamuzi hao.

Wakizungumza katika mkutano ulioshirikisha viongozi na wananchi wa bonde hilo lenye wilaya za Ngorongoro na Longido, walisema uwamuzi wa kulifanya eneo hilo kuwa Pori la Akiba, haukuwashirikisha wananchi waliowengi.

Diwani wa kata ya Engusero, Ibrahim Olesakai alisema bado hawajapata barua rasmi ya kuwataka waondoke eneo hilo, bali wamemsikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,  Profesa Mei 11 mwaka huu, akisema eneo hilo limetengwa kuwa pori la akiba.

Diwani huyo alisema eneo hilo haliwezi kuwa Pori la Akiba, kwasababu ni maeneo ya ardhi ya kijiji na makazi ya watu kwa kipindi cha miaka mingi baada ya kuhamia maeneo kutoka sehemu nyingine walikohamishwa.

Kufuatia hatua hiyo diwani huyo ambaye alikuwa akizungumza na wananchi kutoka vijiji vya Kata hiyo, alimuomba Rais kutengua uwamuzi huo utakaokuwa na maslahi kwa wananchi ambao wanafanya shughuli za ufugaji na kutunza vyanzo vya maji pamoja na wanyama pori.

"Mheshimiwa Rais tarehe 15/1/2019 ulitoa maelekezo kuwa maeneo ya wafugaji yaliyokuwa ndani ya hifadhi, wananchi wake wasibughuziwe, kwa kauli hiyo tunaona katibu mkuu amepuuza maagizo yako, " alisema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Ngarasero Yohana Meeli,  alisema vijiji karibu 74 vilivyopo katika wilaya ya Ngorongoro vimeingizwa katika mpango wa serikali wa matumizi bora ya ardhi  hivyo kutangaza eneo hilo ni Pori la Akiba kutaleta mgogoro baina ya serikali na wananchi.

"Tunakuomba mheshimiwa Rais usikubali mapendekaeizo ya mpango huo yaliyoletwa na Wizara kwasababu hayajaridhiwa na wananchi, eneo hili linatumika kwa utaratibu uliowekwa wa matumizi bora ya ardhi, "alisema mwenyekiti huyo.

Wananchi waliopata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo, walimwangukia Rais kutupilia mbali mpango huo, wakieleza kwamba kukubali utaratibu huo uendelee hawatakuwa na mahali pengine pa kwenda kwasababu Wamasai utatibu wao wa kuhamahama wameufutilia mbali.

"Siku hizi Wamasai hatuhami, maana kila sehemu utakayokwenda kuna wenyewe na kunatokea migogoro, tunakuomba Rais tunajua utakuja kuomba kura na tutakuchagua tena, tusaidie tusiondolewe, " alisema Joshua Mliyetwe mwenyekiti wa kijiji cha Magadini wilayani Longido.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Profesa Adolf Mkenda.
 Mwenyekiti wa kijiji cha Ngarasero Yohana Meeli akizungumza katika mkutano waliouitisha kijijini hapo.
 Mkazi wa kijiji cha Ngarasero Muriel Awada akielezea wasiwasi wa eneo hilo kuwa pori la akiba

 Lagwanani Losiku Olesaiyani akielezea namna walivyoishi miaka mingi katika eneo la bonde hilo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...