Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imetangaza washindi wa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa Mwaka 2020 ambayo kilele chake kilifanyika Machi 16-18 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na mshindi wa kwanza kujinyakulia kitita cha Sh Milioni Tano.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo wakati wa kutangaza washindi hao kutoka kada mbalimbali pamoja na zawadi watakazopata, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watanzania wenye ubunifu na wagunduzi wa teknolojia mbalimbali.

Waziri Ndalichako amesema lengo la serikali kupitia MAKISATU ni kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania hususani wale wa ngazi za chini ambapo pia yanatoa nafasi kwa wagunduzi wa teknolojia kujitangaza na kujulikana na wadau wa ubunifu.

Kada zilizoshiriki kwenye mashindano hayo ni Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ufundi Stadi, Vyuo vya Ufundi wa Kati, Vyuo Vikuu, Taasisi za Utafiti na Maendeleo na Mfumo usio rasmi na kila kada ikitoa washindi watatu.

" Nitumie fursa hii kuwapongeza washindi wote walioshinda kwenye mashindano haya ambayo naamini kabisa yataongeza chachu ya ubunifu na teknolojia, nitoe wito kwa watanzania kuzidi kutumia teknolojia kwani pia ni kichocheo cha maendeleo ya haraka katika sekta ya huduma.

Kupitia mashindano haya pia washindi ambao wameshinda wanaweza kupata kipato kutokana na kiwango cha fedha ambacho kimetolewa kwa mshindi wa kwanza Sh Milioni Tano, mshindi wa pili Sh Milioni Tatu na mshindi wa tatu Sh Milioni mbili," Amesema Prof Ndalichako.

Amewahakikishia washindi wote kuwa serikali itaziendeleza bunifu zao ili ziwe bidhaa na zichangie katika harakati za kukuza uchumi lakini pia serikali imetenga kiasi cha Sh Milioni 750 kupitia COSTECH kwa ajili ya kuendeleza wabunifu 70 walioshiriki katika fainali za MAKISATU.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumzia mashindano ya MAKISATU na zawadi za washindi leo jijini Dodoma.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma leo wakati akitangaza washindi wa mashindano ya MAKISATU.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...