Na Emmanuel Kihaule
Kuna watu ni malaika waliotumwa na Mungu kuja hapa duniani kusaidia wengine wenye uhitaji.(Ndefu kidogo lakini naamini na wewe utaguswa sana).
Naona watu kadhaa akiwemo rafiki yangu George Kalimah wamenitaka niandike leo hii hii kuhusu namna huyu Mama Rita Che-Mponda (pichani juu na mumewe) alivyogusa maisha yangu anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa leo. Mama huyu ni Mke wa Marehemu Dkt. Aleck Humphrey Che-Mponda aliyekuwa mwalimu wa vyuo vikuu kadhaa hapa nchini na Marekani kabla ya kuingia katika siasa.
Mwaka 1993 Baba yangu mzazi alifariki dunia hapa Dar es Salaam na tukaenda kumzika kijijini kwetu kule Peramiho, Songea. Mama yangu alikuwa Moshi. Walikuwa wameshatengana kwa miaka mingi. Mama alikuwa hana uwezo mkubwa lakini alikuwa tajiri wa roho.
Baada ya kifo cha baba, maisha yalibadilika sana. Nikajikuta naanza maisha ya kujitegemea nikiwa sekondari. Nilianza kidato cha kwanza mwaka 1994 pale Lugalo B Sekondari (Lugalo Dar es Salaam) ambayo baadae ilikuja kuunganishwa na Lugalo A na kuunda Makongo Sekondari mwaka 1995 baada ya usajili. Haikuwa kazi rahisi sana. Kuna kipindi nilisimama shule kwa kukata tamaa lakini walimu walituma niitwe ili niendelee na shule. Wapo waliosema wapo tayari kukatwa mishahara yao ili wanilipie ada!
Mtaani nilijishughulisha na shughuli za kupiga picha kwenye maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo na pia kwenye kumbi za muziki na disco. Shuleni tulikuwa na shifts mbili ya mchana na jioni. Wiki hii mnaingia asubuhi na inayofuata mnaingia mchana. Hivyo wiki ya kuingia asubuhi ilinipa fursa ya kupiga picha jioni na usiku au kwenda kusafisha picha kwenye studio Kariakoo. Wiki ya kuingia mchana pia ilinipa fursa ya kupiga picha mbili tatu asubuhi au kwenda kusafisha Kariakoo kabla ya kurudi shule mchana kuendelea na masomo.
Sikuwa na kamera nzuri na kadhaa zilikuwa za watu na nilikuwa nazilipia. Kuna kipindi zile kamera zenye ubora wa chini zilipoharibika kabisa na pia nilipokosa uwezo wa kukodisha kamera nzuri hali ilikuwa ngumu haswa. Maana kamera ilikuwa initafutie chakula, nauli na mahitaji mengine. Bahati nzuri nilipata rafiki ambaye alikubali tukae naye kwenye kajumba cha uani cha baba yake mdogo. Hivyo sikuwa nalipa kodi.
Hapa mtaani jioni wakati nazunguka zunguka kupiga picha, nilikuwa namuona mama mmoja Mmarekani akipanda kuelekea nyumbani kwake akiwa katoka kazini. Ilikuwa sio mara kwa mara kwani alikuwa akitumia gari mara nyingi yeye na mumewe. Kule shuleni nilikuwa napenda sana kujifunza kuzungumza lugha ya kiingereza na kwangu hii ilikuwa fursa ya mimi kunoa kiingereza changu. Hivyo kila nikimuona nilikuwa namfuata na kwenda kumsalimia na kisha kumsaidia mzigo wowote ambao alikuwa amebeba na kuanza kumsindikiza huku nikiboronga kiingereza changu cha St. Kayumba.
Ikawa ameshanizoea na nikawa namsindikiza hadi nyumbani kwake. Siku zilivyokuwa zinaenda alinipenda sana kama mtoto wake wa kumzaa. Akaanza kunisaidia kwa hali na mali hususan baada ya kujua hali yangu. Alianza kunipatia vitabu kwa wingi na pia sio mara moja alinipa maziwa (alikuwa anafuga wakati huo) na zawadi nyingine kem kem. Pia akatafuta marafiki zake na kukusanya misaada mbali mbali kwa ajili yangu!
Yeye alikuwa anafanya kazi pale Shule ya Kimataifa ya Tanganyika ile ya pale pembeni ya Tambaza Sekondari kama nesi. Hivyo akafanikisha mialiko mbali mbali kwangu na wanafunzi wengine wakereketwa wa midahalo ya kiingereza pale IST ya Masaki ambayo ni ya wanafunzi wakubwa. Nikawa nashiriki shughuli mbali mbali pale. Nakumbuka siku ya kwanza kijana wa kizungu aliyekuwa MC wakati wa kututambulisha alisema "A warm welcome to our friends from MAKONGORO secondary school". Alikuwa haijui Makongo Sekondari na huenda alikuwa kasikia sikia kuhusu supu ya makongoro
Kubwa kabisa akaniunganisha na kitengo cha Huduma za Jamii wakati huo kilikuwa chini ya huyo mama mzungu hapo kwenye picha ya chini kushoto (Catherine Ambler/Kelsey ambaye alikuwa mwalimu kutoka Uingereza). Nakumbuka mwaka 1995 kupitia kitengo hicho nilipewa hela ya kwenda kulipa ada ilikuwa Tshs. 112,000/-. Ilikuwa hela nyingi sana kwa mtoto kama mimi. Nikawaomba kwamba badala ya kulipa ada, nitumie hela hiyo kununulia kamera nzuri ambayo nitaitumia kutafuta ada na mahitaji mengine bila kuja kuwasumbua tena. Walifurahi sana kwa wazo hilo. Nikaenda kwa raia mmoja kutoka Asia katika studio ya kusafishia picha iliyokuwa inaitwa Shelui pale jirani na soko la Kariakoo nikanunua kamera ya mkononi aina ya Ricoh kwa Tshs. 109,000/-. Ilikuwa kama mpya na iliniletea mapinduzi makubwa sana na ufanisi wa hali ya juu kwenye kazi yangu!
Masuala ya ada yakawa sio tatizo tena. Ingawa mara nyingine nilikuwa sipati hela yote kwa wakati mmoja. Nakumbuka Mwl. Mkuu wetu wa Wakati huo, Mzee Kanali Iddi Omari Kipingu, aliagiza nisibughudhiwe na kwamba nilipe ada kidogo kidogo kila ninapopata. Pia akanipa tenda zote za picha kwa ajili ya vitambulisho kwa wanafunzi wote waliokuwa zaidi ya elfu tatu! Pia picha za hati za kusafiria za wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana ya kipindi hicho Serengeti Boys waliokuwa wakitunza pale shuleni ilikuwa kazi yangu.
Kupitia kamera ile nikaweza kulipa ada vyema na kujinunulia vitabu. Nilikuwa na vitabu vingi na hata walimu walikuwa wanakuja kuniazima! Kumbuka vingine nilikuwa napata kutoka kwa huyu mama na kule kazini kwake IST.
Maisha yangu yakabadilika sana na masomo yakaniendea sawa. Novemba mwaka 1997 nikamaliza mitihani ya kidato cha nne. Nikiwa bado natafakari nini cha kufanya wakati nasubiria matokeo, huyu mama akaona tangazo la ajira za uandishi wa habari kwa gazeti la kiingereza lililokuwa linakuja kuanzishwa hapa Tanzania. Kwa kiwango changu cha kiingereza na pia umahiri wa kutumia kamera aliamini ningeweza kupata kazi ile. Alimtuma mmoja wa wafanyakazi wake kuja kuniletea hiyo habari kwani simu za mkononi ndio zilikuwa zimeanza na nisingeweza hata kumudu kununua. Kesho yake ndio ulikuwa udahili. Wale mnaofiatilia ukurasa huu mtakumbuka vyema kisa cha huu udahili na jinsi kilivyofungua ukurasa mpya katika maisha yangu. Baadae nikaendelea na kidato cha tano na kuingia chuo kikuu.
Kwangu akageuka kuwa kama mama mzazi. Nakumbuka wakati wa uhai wake mama yangu mzazi alisisitiza kuwa nimuheshimu na kumpenda kama mama yangu mzazi. Walikuwa marafiki haswa! Ameniunganisha na familia yake wakiwemo watoto wake na tumekuwa wote kama ndugu wa damu.
Wanangu wanamtambua kama bibi yao. Isitoshe, yeye na marehemu mume wake na kwa ridhaa ya watoto wameniwezesha kupata eneo la kujenga nyumba na ndipo ambapo ninaishi pamoja na familia yangu! Huu ndio unaitwa Upendo wa Agape! Aliowasaidia kwa namna yangu ni wengi sana. Na ninaamini popote walipo wanamshukuru. Nafahamu watoto kadhaa kutoka katika kituo cha watoto walio katika mazingira magumu cha Tuamoyo kule Kigamboni chini ya kanisa la Mt. Albany anapoabudu mama huyu ambao leo ni watu wazima wengine wamehitumu vyuo vikuu kupitia misaada ya huyu mama.
Msingi bora alionipatia kwa msaada wa Mungu umeniwezesha kusoma kwenye vyuo vikuu mashuhuri vya ndani na nje ya nchi, kufanya kazi na mashirika makubwa ya kimataifa ndani na nje ya nchi tena kwa ufanisi mkubwa. Namshukuru sana Mungu kwa zawadi aliyotupa ya huyu mama na namuombea Mungu ampe maisha marefu yaliyojaa furaha na amani kupitia sadaka zake na kujitoa kwake kwa wenye uhitaji. Amin.
Emmanuel aliposhikwa mkono na Mama Che-Mponda (juu kushoto) na picha zingine wakati wa 'kusota waya" |
Emmanuel sasa ni mfanyakazi katika Shirika la Chakula Duniani (FAO) akiongoza shughuli za miaka 40 za shirika hilo nchini |
Emmanuel akiwa na mwakilishi mkazi wa UNDP nchini aliyemaliza muda wake Bw. Alvaro Rodriguez |
Emmanuel akiwa kazini FAO |
Juu ni Ankal aliyemtia Emmanuel hamasa katika fani ya upigaji picha na chini ni binti Mkubwa wa Mama Rita Che-Mponda, Chemi Che-Mponda, wakiwa na Mzee Reginald Mhango (RiP) aliyekuwa mhariri wa Daily News na baadaye The Guardian ambako Emmanuel alifanya kazi. Chemi, aliyekuwa na Ankal hapo Daily News, ndiye aliyemtia hamasa kuwa mwanahabari
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...