Makamu wa
Rais anayeshughulikia Maendeleo Endelevu katika Kampuni ya GGML,
Simon Shayo akizungumza katika ziara ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko
aliyetembelea miradi ya kampuni hiyo inayotekelezwa chini ya mpango wa kusaidia jamii (CSR) mkoani Geita.
Waziri wa Madini
Dotto Biteko akitoa pongezi za serikali kwa GGML baada ya kutembelea miradi
hiyo. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Josephat
Maganga wakati kushoto ni baadhi ya maofisa wa mji wa Geita.
Waziri wa Madini
Dotto Biteko akielekea kukagua soko kuu la Geita huku akiwa ameongozana na Mkuu
wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Geita,
Josephat Maganga (kulia) pamoja na maofisa wengine wa mji wa Geita.
======== ======= ======= =========
UKUSANYAJI MAPATO SEKTA YA MADINI WAMKOSHA WAZIRI DOTTO BITEKO,
AIMWAGIA SIFA GGML KWA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI KATIKA MKOA WA GEITA
Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko ameipongeza Kampuni ya Uchimbaji
wa Madini ya dhahabu - Geita (GGML) kwa kuwa mdau wa mfano katika kuchangia
utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Geita huku akielezea
kufurahishwa kwake na Serikali ya Mkoa wa Geita inavyosimamia ukusanyaji mapato
katika sekta ya madini.
Biteko ametoa kauli hiyo katika ziara fupi aliyoifanya mkoani
Geita na kukagua miradi inayotekelezwa na Kampuni ya GGML chini ya mpango wake
wa kusaidia jamii (Corporate Social Responsibility) katika Mji wa Geita.
Aidha, amesema lengo la Serikali ni kuona maisha ya watu katika
maeneo yote yenye rasilimali madini, ikiwemo Geita yanabadilika kiuchumi na
kwamba anafurahishwa na namna ambavyo Serikali ya Mkoa wa Geita inavyosimamia
ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye sekta ya madini.
"Tayari tumeshafikia lengo la kukusanya zaidi ya Sh bilioni
400 kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2020 kutoka kwenye sekta hii, na sehemu
kubwa ya makusanyo haya imetoka Geita, hususan GGML. Inatia moyo sana kuona sekta
hii sasa inachangia zaidi ya asilimia 5 ya uchumi wa nchi yetu. Lengo ni
kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025,"amesema
Waziri Biteko.
Mojawapo ya miradi ambayo ilikaguliwa na Biteko katika ziara
yake hiyo ni ujenzi wa Kanda maalumu ya uwekezaji "Special Economic
Investment Zone" ambao utasimamiwa na Mamlaka ya ukanda maalumu wa
Uwekezaji (EPZA) na Halmashauri ya Mji wa Geita.Pia ametembelea miradi mingine
ya kimkakati inayofadhiliwa na GGML, ikiwemo ujenzi wa Soko Kuu la Geita Mjini
na soko la Katundu.
Kwa upande wake Makamu wa Rais anayeshughulikia Maendeleo Endelevu
katika Kampuni ya GGML Simon Shayo amesema utekelezaji wa miradi ambayo
imetembelewa na Waziri Biteko ni sehemu ya mpango wa mwaka 2018/19 unaoenda
sambamba na mojawapo ya tunu za kampuni hiyo inayoelekeza kwamba jamii
inayozunguka shughuli zake sharti ifaidike kwa uwepo wake.
Ameongeza kuwa GGML ambayo ni sawa na kampuni-raia inawajibika
ipasavyo kwa jamii kwani hutumia Sh bilioni 9.2 kila mwaka kugharimia miradi ya
jamii mkoani Geita na kuifanya kampuni hiyo kuwa ya kipekee kutokana na mchango
mkubwa inayotoa kusaidia jamii.
"Kama Kampuni-raia ndani ya Tanzania, GGML iliyoko chini ya
AngloGold Ashanti itaendelea kuunga mkono na kusaidia jamii zinazotuzunguka.
Utekelezaji wa miradi ya CSR na shughuli zingine kama hizo.
"Ni ushahidi wa wazi kwamba kampuni, serikali na jamii
zikifanya kazi pamoja zinaweza kuboresha maisha ya watu kupitia uwekezaji
endelevu katika miundomuni ya biashara na huduma.Tunataka kuona maisha ya mtu
wa kawaida katika jamii yetu yakiwa bora zaidi kupitia uwekezaji endelevu wa
Kampuni yetu,"amesema.
Aidha katika kipindi cha mwaka 2018, GGML iliwezesha
utekelezwaji wa miradi kadhaa kupitia mpango wake wa kuwekeza katika jamii.
"Miradi hii inajumuisha; uwekaji wa taa za barabarani
katika mji wa Geita, ujenzi wa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ujenzi wa
soko la kisasa Geita mjini, umaliziaji wa majengo zaidi ya 600 ya afya na elimu
na ujenzi kamili wa shule tatu mpya na vituo vya afya vinne. Pia GGML imetenga
Sh. bilioni 18 kwa ajili ya miradi mingine kama hiyo katika kipindi cha kati ya
mwaka 2019/20 na 2020/21.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...