Charles James, Michuzi TV
KUFUATIA agizo la Rais Dk. John Magufuli kuagiza kurejea kwa masomo ifikapo Juni 29 kwa wanafunzi wa Elimu ya Msingi hadi kidato cha Tano leo Michuzi TV tumetembelea Shule ya Sekondari Dodoma kujionea namna shughuli za masomo zilivyorejea.
Akizungumza na Michuzi TV, Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwalimu Amani Mfaume amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo huku akiahidi kuendelea kufuata muongozo wa Wizara ya Afya katika kujikinga na Corona.
Mwalimu Mfaume amesema jana usiku walipokea wanafunzi 150 wa kidato cha tano kwa sababu wao wapo bweni na leo wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne wameripoti shuleni na wameanza masomo yao kama kawaida.
Amesema wanafunzi wote baada ya kuripoti shuleni hapo walipimwa joto la mwili na hakuna mwanafunzi yoyote aliekutwa na joto kubwa lakini asubuhi kabla ya kuanza kwa masomo wamekaa na wanafunzi wao na kuwakumbusha umuhimu wa kuvaa Barakoa na namna ya kujikinga.
" Leo asubuhi tumefanya mazungumzo na wanafunzi wetu na kabla alivyosisitiza Rais Magufuli kuondoa hofu na sisi tumewaondoa wanafunzi wetu hofu na kuwasisitiza kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari kama ambavyo serikali imekua ikisisitiza.
Tuna furaha kuona wanafunzi wetu wamerejea wakiwa salama na wana ari ya kuendelea na masomo na hata hawa wa kidato cha sita ambao wameanza mitihani yao leo ya Taifa wapo na ari na tunaamini watafanya vizuri katika matokeo yao," Amesema Mwl Mfaume.
Amesema wanaendelea kufuata muongozo wa Wizara katika kujikinga ambapo wanayo madumu mawili ya Lita 1000 moja likiwa katika lango la kuingilia na lingine likiwa bwenini lakini pia kila Darasa lina ndoo ya maji tiririka na sabuni kwa ajili ya kunawia.
Mwalimu Mfaume amesema wameunda kamati ndogo ya kupambana na ugonjwa wa Corona yenye Walimu kwa ajili ya kuongea na wanafunzi na kila Mwalimu anaeingia kwenye kipindi anakua na muda wa kuwaelimisha wanafunzi na kuwaondoa hofu.
Kwa upande wake Zawadi Abbas ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne amemshukuru Rais Magufuli kwa kuruhusu masomo kuendelea kwani imewapa fursa ya wao kumaliza masomo yao.
Amesema wao kama wanafunzi wanaendelea kufuata maelekezo ya kujikinga na Covid19 kupitia walimu wao ambao wamewapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo leo baada ya kurejea shuleni.
" Kwa kweli Rais Magufuli tunamshukuru sana maana tulikua nyumbani na wengine tulishakosa Matumaini ya kurejea shuleni, tunampongeza kwa hatua yake ya kurejesha masomo na shughuli zingine na sisi tunamuahidi kusoma kwa bidii na kufuata maelekezo yote ya kujikinga na Corona," Amesema Zawadi.
Muonekano wa Ndoo za Maji Tiririka na Sabuni zikiwa Nje ya kila Darasa katika Shule ya Sekondari Dodoma baada ya masomo kurejea rasmi leo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kuruhusu masomo kuendelea kama kawaida.
Wanafunzi wakiendelea na shule za usafi shuleni baada ya kurejea kuendelea na masomo leo ikiwa ni utekelezeji wa agizo la Rais Magufuli la kuruhusu shughuli za masomo.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dodoma wakiendelea na masomo yao leo baada ya kuripoti shuleni kufuatia agizo la Rais Dk John Magufuli kuruhusu masomo yaendelee kama kawaida baada ya kupungua kwa maambuzi ya Corona.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Dodoma akitoa maelekezo kwa Mwanafunzi wake wa kidato cha Tano baada ya masomo kurejea tena.
Wanafunzi wa Sekondari Dodoma wakiwa Darasa leo ambapo wamevalia Barakoa huku wakizingatia tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Corona ikiwa ni pamoja na kukaa umbali wa mita moja.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Dodoma, Mwl Amani Mfaume akizungumzia kurejea kwa wanafunzi wake wa kidato cha kwanza hadi cha tano pamoja na namna wanavyojikinga na Corona.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...