Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema kuwa Katika Bajeti ya Fedha ya mwaka 2020/2021,Serikali inapendekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye bima ya kilimo cha mazao. 

Dk.Mpango amesema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati anawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali yenye jumla ya Sh.Trilioni 34.88 ambapo katika eneo hilo la kusamehe kodi amefafanua lengo ni kupunguza gharama na kutoa unafuu katika bima za kilimo kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kuziwekea bima shughuli za kilimo pamoja na kuvutia wananchi kutumia huduma za bima kwa ajili ya kujikinga na majanga mbalimbali yanayoathiri shughuli zao za kilimo.

Pia ametumia nafasi hiyo kutangaza kuruhusu michango ya wadau kwenye Mfuko wa Ukimwi isitozwe kodi ya Mapato.Amependekeza kwamba michango iliyotolewa na wananchi kwa Serikali na itakayoendelea kutolewa katika kipindi cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona isitozwe kodi hadi hapo serikali itakapotangaza kuisha kwa ugonjwa huo.

Dk.Mpango amesema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuhamasisha uchangiaji wa hiari katika Mfuko wa Ukimwi na kwa serikali ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na Corona.

Wakati huo huo amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa bidhaa kifungu cha 124(2), ameeleza marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla. Pia kutokana na biashara za bidhaa hizo kuzorota kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na Corona, amependeza kutofanya mabadiliko ya viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwa bidhaa zote.

Akiendelea kuwasilisha bajeti hiyo Waziri Mpango amesema hatua hiyo inazingatia kiwango kidogo cha mfumuko wa bei nchini na azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.

Pamoja na mambo mengine katika eneo hilo amependekeza kupunguza kiwango cha tozo kwa ajili ya maendeleo ya ufundi stadi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4. Lengo la marekebisho hayo ni kuwapunguzia waajiri mzigo na gharama za uendeshaji wa shughuli zao na kutimiza azma ya kupunguza tozo hizo hatua kwa hatua bila kuathiri mapato kwa kiasi kikubwa.

"Pia natangaza kupunguza ushuru wa forodha hadi asilimia 0 kutoka viwango vya awali vya asilimia 10 na asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa vifaa maalum vinavyotumika katika kupambana na ugonjwa wa Corona,"ameeleza kwenye hotuba yake.

Amevitaja vifaa hivyo ni barakoa (Masks), kipukusi (sanitizer), mashine za kusaidia kupumua (ventilators) na mavazi maalum ya 85 kujikinga yanayotumiwa na madaktari na wahudumu wa afya (PPE).

"Natangaza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACCMA, 2004) ili kutoa msamaha kwenye dawa na vifaa muhimu vinavyotumika kupima, kukinga, kutibu na kupambana na mlipuko wa magonjwa.Kusamehe ushuru wa forodha kwenye zana zinazoingizwa nchini na watu au taasisi zinazohusika katika kilimo, kilimo cha mbogamboga, kilimo cha maua pamoja na ufugaji wa samaki,"amesema.

Amefafanua lengo la kutoa msamaha huo ni kuchochea na kuhamasisha ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na kuvutia uwekezaji mpya katika sekta ndogo ya ufugaji wa samaki nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi  kwa mwaka 2020/2021  ambapo Serikali imepanga kukusanya na kutumia takribani  shilingi trilioni 34.9  kwa matumizi ya maendeleo na matumizi mengine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...