Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akitia saini katika kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa
Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar
es salaam, Juni 17, 2020. Wa pili kulia ni Balozi wa Burundi nchini,
Mhe. Abayeho Gervais.

Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akitoa heshima baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo ya
kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa
Burundi, Upanga jijini Dar es salaam, Juni 17, 2020. Wa pili kulia ni
Balozi wa Burundi nchini, Mhe. Abayeho Gervais.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Balozi wa Burundi nchini , Mhe. Abayeho Gervais baada ya
kutia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa
Burundi, Pierre Nkurunziza kwenye Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar
es salaam, Juni 17, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………….
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Juni 17, 2020 ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na kutoa pole kwa wananchi wa nchi hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli nimekuja hapa kutoa pole na salamu za rambirambi kwa Serikali na wananchi wa Burundi kufuatia kifo cha aliyekuwa rais wa nchi ya Burundi. Mheshimiwa Rais na Watanzania wote tumepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kifo chake.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 17, 2020) akiwa katika Ofisi za Ubalozi wa Burundi, Upanga jijini Dar es Salaam baada ya kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 9, 2020 kutokana na mshituko wa moyo.
Amesema Tanzania na Burundi ni nchi zenye historia ndefu na mshikamano wa muda mrefu, hivyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi wawe watulivu katika kipindi hiki cha majonzi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha umoja na mshikamano kati yake na Burundi.”
Awali, Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Balozi Abayeho Gervais ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Taifa hilo na kwamba anatarajia umoja na mshikano huo utadumu milele na milele.
“Tunamshukuru Rais wa Tanzania amepeleka ujumbe mkubwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Burundi kwa ajili ya kushuhudia uapishwaji wa Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye ambaye anatarajiwa kuapishwa kesho Juni 18.
Akizungumzia kuhusu kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Balozi Gervais amesema wamepokea kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alikuwa bado ni kijana akiendelea kufanya shughuli zake. “Hii yote ni mipango ya Mwenyezi Mungu na sote tupo safarini.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...