UZINDUZI wa upuliziaji wa viwatilifu kwenye madimbwi ya maji ili kuangamiza mazalia ya Mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria umefanyika katika kituo cha afya NASSA na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya, David Pallangyo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Godfrey Mbangali, watumishi wa Afya na Maafisa afya kutoka kata zote 15. Zoezi hilo litakalochukua siku nne kuanzia tarehe 17 hadi 20 Juni, 2020 litafanyika katika kata zote 15 na vijiji vyote 59 vilivyopo wilayani Busega.

Kaimu mkuu wa Wilaya ya Busega, David Pallangyo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kuacha fikra potofu juu ya zoezi hilo. Amesisitiza kuwa dawa zinazotumika katika zoezi hilo la kuua mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria hazina madhara yoyote kwa afya ya binadamu hivyo wananchi watoe ushirikiano ili kukamilisha kusudio la zoezi hilo.

Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Busega Dkt. Godfrey Mbangali, akimkaribisha mgeni rasmi amesisitiza kuwa zoezi hilo la kupulizia dawa kwenye mazalia ya mbu lililofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la T-Marc Tanzania wanaoshughulika na mradi wa badili tabia tokomeza Malaria kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto litafanyika kwenye kata zote 15 kwa siku nne, na litahusisha sehemu zenye maji yaliyotuama ambazo ndizo sehemu kuu za mazalia ya mbu wa malaria.
Ugonjwa wa Malaria ni moja ya magonjwa yaliyo na maambukizi makubwa wilayani Busega. Kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2018 hali ya maambukizi ya Malaria kwa jamii ya Busega ilikuwa ni 8.3% ambayo ilikuwa ya pili kimkoa kuwa na maambukizi ya juu, huku katika kipindi cha miaka mitatu maambukizi ya Malaria kwa wilaya ikiwa 45,719. Hivyo kuzinduliwa kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza maambukizi ya malaria wilayani Busega.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...