Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa eneo lilitengwa kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa Serikali lililopo mjini Dodoma, limetolewa kwa Wananchi kutokana na kila kiongozi wa Serikali anataka kuzikwa nyumbani kwao alipozaliwa.
Rais Magufuli ameyasema hayo alipotoa salamu za mwisho katika shughuli ya kuaga na Mazishi ya Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa shughuli iliyofanywa nyumbani kwao Lupaso, Wilayani Masasi Mkoani Mtwara.
"Nilimuuliza Mzee Mkapa kipindi yupo hai, Mzee unataka kuzikwa wapi pindi utakapofariki?, Mzee Mkapa alinijibu anataka kuzikwa Kijijini kwao Lupaso, mkoani Mtwara. Mzee Kikwete naye alisema anataka kuzikwa Kijini kwao Msoga, mkoani Pwani."
Niliogopa kuuliza kwa Mzee Mwinyi kwa sababu alikuwa na miaka 92, niliogopa kuona kama natabiri Kifo chake, hata mimi nasema nikifariki nataka kuzikwa nyumbani Chato", amesema Rais Magufuli.
Rais amesema Mzee Mkapa alikuwa na sehemu nyingi za kuzikwa lakini alichagua kuzikwa Kijijini kwao, Lupaso, Mtwara. "Angetaka kuzikwa sehemu yoyote, Dar es Salaam, Lushoto ana maeneo makubwa tu, lakini alisema anataka kupelekwa Masasi", ameeleza Rais Magufuli.
Pia amesema Jamii ya Watanzania inapaswa kujifunza kwa Mzee Mkapa kwa upendo aliouonyesha kwa Wananchi wote, amesema Kijiji cha Lupaso kimeacha alama kubwa kwa Taifa la Tanzania kutokana na kutoa Kiongozi Mzalendo na aliyependa Wananchi wake.
Rais Magufuli ameishukuru Kamati ya Maandalizi ya Mazishi iliyoongozwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Viongozi wote, Wananchi, Viongozi wa Dini zote sambamba na Waombolezaji walioshiriki bega kwa bega kuhakikisha safari ya mwisho ya Hayati Mzee Benjamin Mkapa katika makazi yake ya milele.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...