Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya
Jamii Dkt. John Jingu akisikiliza maelezo kuhusu kituo cha ubunifu kilichopo
Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai kutoka kwa Mkufunzi na Msimamizi wa Kituo
hicho Clara Mwinami wakati alipotembelea Chuo hicho kujionea shughuli za
mbalimbali zinazofanywa.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii
na Wizara ya Viwanda na Biashara inakusudia kuwekeza katika kituo cha
ubunifu kilichopo katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai, Mkoa wa
Tanga ili kukiwezesha kutoa elimu yenye tija kwa wahitimu na jamii kwa ujumla
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika Chuo cha Maendeleo ya
Jamii Mabughai kujionea shughuli za mbalimbali zinazofanywa na Chuo hicho.
Katibu Mkuu Dkt. John Jingu amesema kuwa amefanya mazungumzo na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe ili
kukiwezesha Chuo cha Mabughai kutoa mafunzo ya ubunifu endelevu kwa jamii.
Alisema Mpango wa maboresho ya miundombinu na teknolojia ya Chuo
hicho utashirikisha Shirika la Viwanda Vidogo nchini(SIDO) chini ya Wizara ya
Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Chuo cha Mabhughai kilichoko chini ya
Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
"Teknolojia imebadilika sana mimi na Profesha Shemdoe
tumekubaliana kufanya maboresho katika Chuo hiki tuone namna ya kukiwezesha
kuwanoa wabunifu ili elimu inayotolewa iweze kuwa na tija kwa walengwa wetu
ambao ni wanachuo na wananchi wa maeneo jirani" alisema Dkt. Jingu.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inalenga
kuwawezesha Wanafunzi kuwa na uwezo wa kujiajiri kupitia maarifa wanayopata na
kuanzisha mtandao wa ajira kwa wahitimu ambao watafanya kazi kwa vitendo na
hivyo kutengeneza fursa zaidi za mafunzo kwa wengine.
Katibu Mkuu Jingu amesema mpango wa maboresho kwa Chuo cha
Mabughai utaanza hivi karibuni baada ya kukamilisha taratibu za maandalizi kwa
ushirikiano wa SIDO na ni hatua mojawapo ya kushiriki katika Ujenzi wa Uchumi
wa Viwanda.
“Tumeshuhudia jitihada za Serikali zilivyotuwezesha kuingia
katika Uchumi wa Kati miaka mitano kabla ya muda uliotarajiwa,wakati
tukiendelea kujivunia hatua hii muhimu kushiriki kwa vitendo katika mabadiliko
ya teknolojia” alisema.
“Kuna baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, Mfano kuna
mbunifu ametoa ajira kwa watu zaidi ya 100, hii ni hatua mojawapo ya mafsnikio.
Tunataka kukiwezesha Chuo hiki cha Mabughai kutengeneza wabunifu zaidi”
alisema.
Alifafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya
Maendeleo ya Jamii na Wizara ya Viawanda na Biashara inakusudia kuwawezesha
vijana kupata ajira zitakazotokana na ubunifu kwa wahitimu na pamoja na wakazi
wa maeneo jirani na Chuo.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo
ya Jamii iko katika hatua za mwisho kuanzisha Kampuni ya ulinzi itakayomilikiwa
na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mabughai ili kuwapa nafasi kuwapa nafasi
wahitimu kujiajiri wanapotoka chuoni hapo.
“Tunataka kuanzisha kampuni ya chuo ambayo itakuwa inamilikiwa
na chuo kama ilivyo SUMA JKT ili kuwapa fursa zaidi za ajira kwa vijana”
alisema
Akiwa chuoni hapo Dkt. Jingu ameweza kutembelea maeneo
mbalimbali ikiwemo kituo cha ubunifu cha kidijitali kinacholenga kuwasaidia
wanafunzi hao kubuni na kuendeleza maarifa wanayopata chuoni hapo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...